Dodoma. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema vituo vya afya vinavyojengwa nchini Tanzania vinakabiliwa na uhaba wa vifaa na wataalam licha ya kuwa madaktari wenye sifa kuwepo wengi mitaani.
Sugu aliyedai kwa miaka mitano madaktari hawajaongezewa mshahara, ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 6, 2020 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa taarifa ya kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Amesema mbali ya kujenga vituo vya afya na zahanati kuna tatizo la vifaa tiba na dawa.
“Tunajisifu kujenga majengo lakini hatuna watumishi wa afya. Taarifa zinaeleza kuwa kuna upungufu wa asilimia 52 na hii ni kwa sababu hatuajiri kabisa,” amesema, kubainisha kuwa wanaohitimu shahada za udaktari wapo wengi, hawana kazi, “mbaya hata wale waliopo ambao ni asilimia 48 kama ilivyo kwa watumishi wengine, nao kwa miaka mitano hawajaongezewa mishahara.”
Amesema awali madaktari walikuwa wanagoma lakini kwa sasa hawawezi licha ya kuwa hawaridhiki.
“Mfano ni Lwakatare (Wilfred- mbunge wa Bukoba Mjini) amekaa hospitali miezi minne hajanyanyuka, amepelekwa India amekaa siku tano siku ya sita amenyanyuka leo tuko naye bungeni,” amesema.
Pia Soma
- Wakili kizimbani kwa madai ya kujipatia fedha kwa udanganyifu
- VIDEO: Alichokisema Membe baada ya kuhojiwa kwa saa tano
- VIDEO: HII HAPA KAULI YA MEMBE BAADA YA KUHOJIWA CCM
Kuhusu matibabu kwa wananchi, Sugu amesema yana gharama na kushauri wakati wanajipanga ni vyema wasiache watu wafe.
“Uzuri mnajipambanua kama wajamaa, wajamaa gani? Mnakataa kutibu watu. Hata Uingereza ambako sio wajamaa wanatibu watu chini ya mfumo wa bima, mnawezaje kutoa elimu bure mshindwe matibabu bure,” amehoji Sugu.