Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Spika wa Bunge tumtakaye’

Spikaapic Data ‘Spika wa Bunge tumtakaye’

Tue, 25 Jan 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wanasiasa na wataalamu wa sayansi ya siasa nchini wamebainisha sifa na misingi ambazo Spika ajaye wa Bunge anapaswa kuisimamia katika utekelezaji wa majukumu.

Wamesema ili Bunge lifanye kazi zake ipasavyo, linapaswa kuwa na kiongozi atakayeisimamia Serikali na mchakato wa utungwaji wa sheria makini za nchi na atakayehimili mabadiliko mbalimbali bila kuathiri utendaji wake wa kazi.

Hayo yameelezwa katika mjadala wa kitaifa kuhusu uchaguzi wa Spika wa Bunge na matarajio ya wananchi kwa Spika ajaye, uliofanyika Jumamosi kupitia mtandao wa Zoom.

Majukumu matatu

Naibu Makamu Mkuu wa wa Chuo (Utafiti) UDSM, Profesa Bernadetha Killian alisema moja ya vigezo vya kupima uimara wa taasisi yoyote ni kiasi gani inaweza kuhimili mabadiliko mbalimbali bila kuathiri utendaji wake.

Advertisement Profesa Killian alisema Bunge lina majukumu matatu ya msingi ambayo ni kuwakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia Serikali, ambayo yanasimamiwa na Spika.

Soma zaidi: Hawatausahau moto wa Ndugai

Alisema pia Bunge lina kazi ya msingi ya ujenzi wa demokrasia ya nchi na ni kama daraja linalowaunganisha wananchi na Serikali kupitia wabunge wao.

“Ni taasisi muhimu sana. Spika ana kazi kubwa kuhakikisha hili jukumu la msingi la ujenzi wa demokrasia ya nchi yetu analiendesha vizuri kwa kuimarisha kazi ya Bunge kama taasisi.

“Tunapompata spika si yule tu ambaye anaongoza vikao pale kama ambavyo tumezoea, bali ana wajibu wa kuwa mtawala kiongozi na kuifanya taasisi iende mbele,” alisema Profesa Killian.

Alisema Spika anapaswa kuhakikisha kuna kanuni na taratibu ambazo zinafanya Bunge liangalie kazi zake bila kupendelea upande wowote.

“Spika anatakiwa asipendelee mbunge yoyote akiamini wote hawa ni wawakilishi wa wananchi, pili weledi, kazi ya spika kuhakikisha wafanya kazi wapo professional na kufanya kazi kwa weledi na tatu kuangalia resources ambazo linazo, kwa kuangalia jinsi gani linaweza kutumia Tehama na masuala ya dijitali ili kuwasiliana na watu wake,” alisema.

Alisema Bunge linatakiwa liwe na utaratibu mzuri katika mawasiliano, spika ajae anatakiwa aangalie ni kwa kiasi gani Bunge linakuwa la kidiitali na mawasiliano na wananchi, linawasiliana vipi na wananchi, taarifa zinawafikiaje wananchi.

Alitoa angalizo kwa wabunge kupeana vijembe ndipo wawasiliane na wananchi bali lazima kuwe na utaratibu mzuri wa mawasiliano.

“Nafahamu sasa hivi Bunge lina majukwaa mbalimbali ya kuhakikisha wananchi wanatembelea, watoto wa shule lakini kulikuwa na jukwaa la Bunge linarusha live zile shughuli za Bunge live na zilitoa fursa ya kila Mtanzania kujua kila kinachoendelea bungeni. Spika anayekuja akalifikirie vile vikao vya Bunge vikaonyesha live ili wananchi tunaona tunajua kinachoendelea bungeni,” alisema.

Aligusia pia utendaji wa kamati, kwamba Bunge linatakiwa kufanya mawasiliano na kuongeza ushiriki wa wananchi katika kuchangia masuala ambayo yanapelekwa bungeni ilim kuhakikisha kinapatikana kitu cha msingi.

Mtu makini

Akizungumza kwenye mjadala huo, Mbunge wa Mvumi na Mjumbe wa NEC, Livingstone Lusinde alisema Dk Tulia ni mtu makini, anayefuatilia mambo na haitakuwa ajabu kama itatokea hali ya kuwaweka kikaangoni mawaziri wazembe.

Alisema kwa misimamo yake, mawaziri watapaswa kuwa makini hasa katika kujibu maswali sawasawa kwa sababu wanaweza wakajikuta wanapoteza uwaziri wao kwa njia moja au nyingine.

“Dk Tulia yuko makini sana. kupitia ushauri wa huyohuyo Spika kama watashindwa kujibu maswali kwa usahihi, kama watashindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo huyu tunayekwenda kumpata ni mzuri sana katika ufuatiliaji,” alisema Lusinde.

Akizungumzia taswira ya Bunge katika mtazamo wa kuibana Serikali katika kuleta maendeleo, alisema aina ya Spika anayetarajiwa ataamsha morali ya Bunge kwenye kufanya kazi za kuisimamia Serikali na kuleta maendeleo.

“Kwa hiyo ukitizama kimsingi, masaa aliyofanya kazi Spika wa Bunge tunayemtarajia akiwa Naibu Spika, ameweka rekodi ya kufanya kazi na kuwa naibu spika wa kwanza aliyekalia kiti cha uspika kwa saa nyingi kuliko mwingine,” alisema Lusinde.

Akifafanua, alisema Dk Tulia aliwahi kukaa kwenye kiti cha uspika bila kukosekana kwa miezi miwili, yaani siku 60. Kwa hiyo ukichukua siku 60 unapata saa 360, hivyo ana uhakika spidi yake inakwenda kuamsha morali ya Bunge zima, kuisimamia Serikali kuleta maendeleo.

“Huyu (Dk Tulia) anakuwa wa nne kutoka nafasi ya unaibu spika, kwa hiyo nina uhakika ataziba ufa na mianya yote kwa sababu ana uzoefu. Ni mtu mkali na mwenye kuelekeza pale inapobidi.

Mihimili

Kuhusu mihimili, Profesa Killian alisema Rais ni sehemu ya Bunge hivyo lazima kujengwe mahusiano makubwa ya kiutendaji, kimaadili na kiusimamizi kuhakikisha mihimili yote iko vizuri ili umoja wa kitaifa ubaki salama.

“Kama mihimili ikiwa haiko sawa basi umoja wa kitaifa hauwezi kupatikana. Rais ni sehemu ya Bunge, sheria ikipitishwa bila yeye kusaini haiwezi kufanya kazi, bajeti ya Bunge. Lazima kuna mipaka ya kufanya kazi ili mashirikiano yawepo,” alisema.

Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima alisema nchi imepita kwenye misukosuko, ukungu na tufani na baadaye ikatokea hakuna spika lakini kutokana na kuwapo Katiba imara, nchi inaweza kusonga.

Alisema katika dhana ya nidhamu na utalawa bora ili Bunge liwe huru, linatakiwa kwanza liwe linaisimamia Serikali kwa kupitisha bajeti yake, Bunge na Spika wanatakiwa kuwa macho kuhakikisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma inazingatiwa.

Pamoja na hayo, Gwajima alisema Bunge linatakiwa kuhakikisha Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG anakuja kusoma ripoti kwenye Bunge ili wabunge waone uhalisia kati ya bajeti iliyopitishwa na matumizi ya fedha za Serikali, suala lenye mahusiano makubwa na Bunge.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Afya Zanzibar na kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed alisema jambo la msingi ni kutambua uwakilishi wa Watanzania wote upo bungeni, hilo lazima kiongozi wa muhimili huo alitambue.

Alisema Spika anatakiwa kuhakikisha anaulinda umoja wa tunu za taifa. Kama spika akiweza kumuachia mbunge akaharibu tunu atakuwa amekwenda kinyume na majukumu yake ya msingi.

Alisema Bunge pamoja na mambo yake mengine ya kutunga sheria, lazima lifuate misingi, hivyo kazi ya Spika ni kuhakikisha sheria hizo zimeshirikisha pande zote mbili ili ikipita kusiwe na vikwazo, likiachiwa linaweza kubomoa maadili na umoja wa nchi.

“Jambo lingine katika kupitisha bajeti ya Serikali lazima iangaliwe inahusisha pande zote mbili, hili jambo nalisema kwasabbau limechangia kwa kiasi kikubwa kuvuruga umoja wetu. Ni vizuri aelewe kwa undani kabisa, chochote kinachopita bungeni ni kwa maslahi ya Watanzania wote. Na kama kuna kasoro anauwezo wa kuhoji.

“Yeye anasimamia mabadiliko ya sheria mbalimbali hivyo aangalie inajenga uhusiano mzuri na Taifa letu, kamati za bunge pia asimamie ziwe zinafanya kazi vizuri,” alisema.

Hoyce Temu amzungumzia Dk Tulia

Naibu mwakilishi wa Tanzania jijini Geneva, Uswizi, Balozi Hoyce Temu alisema, “Dk Tulia alikuwa kiongozi wangu chuoni, nilimjua nilisoma naye, nafahamu uwezo wake wa kujua mambo na siku zote ni kiongozi anayefanya mambo kwa manufaa ya watu anaowaongoza. “Wanawake tuna wajibu kuonyesha imani ya Rais kwa wananchi kwamba tunaweza,” alisema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz