Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Spika bado ana nafasi ya kurejea uamuzi wake- Nassari

47121 PIC+NASSARI

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema atakwenda mahakamani kutafuta haki ya uwakilishi wa wananchi wa Arumeru baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kutangaza kwamba hana sifa za kuendelea na ubunge.

Hata hivyo, amesema Spika bado ana nafasi ya kurejea uamuzi wake ili wananchi wa Arumeru waendelee kuwa na mwakilishi katika Bunge.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumapili Machi 17, 2019, Nassari amesema mara ya mwisho alihudhuria mkutano wa Bunge wa Septemba lakini hakuhudhuria mkutano wa Novemba na Januari kwa sababu alikuwa anamuuguza mke wake huko Marekani.

"Nilifanya jitihada za kuwasiliana na Spika, nikamtumia ‘email’ (barua pepe) nikiwa Marekani kumjulisha hali ya mke wangu. Nasikitika kwa uamuzi alioufanya, nawapa pole wananchi wangu wa Arumeru, haki yao tutaitafuta kwenye vyombo vya sheria," amesema Nassari.

Akizungumza kwa huzuni, Nassari amesimulia jinsi alivyokuwa akimuuguza mke wake kutokana na matatizo aliyokuwa nayo na kusema alijaaliwa kupata mtoto wa kike Januari 27, siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge la Januari.

Amesema alikuwa njia panda kuamua kati ya kuhudhuria vikao vya Bunge au kukaa na mke wake ambaye alikuwa mgonjwa.

Amesema hajutii uamuzi wake wa kusimamia kiapo chake cha ndoa kwa kuamua kumuuguza mke wake.

"Pamoja na huzuni ya kuvuliwa ubunge, bado nina furaha ya kupata mtoto. Kuwa mbunge hakuondoi majukumu mengine ya kifamilia. Spika alihudhuria harusi yangu mwaka 2014, alikuwa anajua sina mtoto na nilimjulisha juu ya matatizo ya mke wangu. Alitakiwa kujiridhisha kwa kuniita na kunihoji badala ya uamuzi alioufanya," amesema Nassari.

Katika mkutano huo na wanahabari, Nassari hakuruhusu kupokea maswali kwa madai kwamba alikuwa amevurugwa (devastated), hivyo akaomba asipokee maswali.

Hata hivyo, kauli yake kwamba alihudhuria mkutano wa Bunge wa Septemba, inatofautiana na taarifa ya Bunge iliyotolewa Machi 14 ikieleza kwamba Nassari alikosa sifa za kuwa mbunge kwa kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Septemba, Novemba na Januari.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz