Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Spika azidi kubanwa kauli ya mikopo

1302425d7839d94a60fbf9959e6c3b7f.jpeg Job Ndugai, Spika wa Bunge

Sat, 1 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM-Taifa), Shirika la Ulingo Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na Mwandazi wa matamasha ya Krismasi nchini wamemjia juu Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kauli zake za kukosoa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kutafuta maendeleo kupitia mikopo.

Hivi karibuni Spika huyo alinukuliwa na mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari akikosoa mikopo inayochukuliwa na serikali kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.

Katika taarifa yake hiyo, Ndugai alizungumzia mkopo uliopokelewa na serikali kutoka Shirika la Fedha Duniani (IFM) wa Sh trilioni 1.3 ambazo zimeelekezwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, vituo vya afya na huduma nyingine.

Msimamo wa UVCCM

Akitoa msimamo wa UVCCM jana mara baada ya kukagua ujenzi wa madarasa mawili kwa fedha hizo katika

Shule ya Sekondari Kihesa, mjini Iringa, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Kenani Kiongosi alisema:

“Vijana hatutakubali na kumvumilia mtu yeyote anayemvunjia heshima Rais na yeyote anayetaka kumkwamisha Rais. Anayeamini yeye ni mkubwa kuliko CCM aseme hadharani kwamba yeye ni mkubwa kuliko chama ili chama kiweze kuchukua hatua.”

Alisema UVCCM katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja huo kilichofanyika hivi karibuni mjini Dodoma, wametoka na ajenda ya kusimama na Rais Samia na kumsaidia kutekeleza majukumu yake.

Shirika la Ulingo

Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika hilo Ulingo kitaifa, Dk Ave-maria Semakafu aliiomba CCM kupitia Kamati yake ya Maadili kumuita Ndugai na kumhoji kama wengine wanavyohojiwa kwa kuwa ni kada wa chama hicho na Mbunge wa Kongwa.

“Ndugai amemkosea Rais kwa kauli yake kuhusu mikopo ambayo serikali inakopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na mbaya zaidi ameonyesha utovu wa

nidhamu pale aliponukuliwa akisema mama apunguze kukopa kwani nchi itapigwa mnada, Samia Suluhu Hassan ni Mkuu wa nchi na akikopa imekopa serikali hata serikali zilizopita zilikopa chamno ni kipi,” alihoji.

Dk Ave-maria aliongeza kuwa ajenda yao kwa sasa ni asilimia hamsini kwa hamsini na ni wakati muafaka wakina mama kuungana na kuwa kitu kimoja katika kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwani wanawake nchini wapo asilimia 53 ni wengi zaidi ya wanaume hivyo wasikubali kunyanyaswa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika hilo Kitaifa, Anna Abdallah akizungumza kwa njia ya simu akiwa Ukerewe alisema ni wajibu wa kila Mtanzania kutetea maslahi mapana ya nchi kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.

“Kwa mantiki hiyo yatupasa kuheshimiana, haki ya kumiliki rasilimali zetu ni haki yetu sote, Ndugai ameteleza ni binadamu aombe radhi maisha mengine yaendelee,” alisema.

Kauli ya Alex Msama

Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama amesema maendeleo

makubwa katika nchi yoyote ile hayawezi kufanyika bila kukopa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Msama alisema kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo inapaswa kuungwa mkono na kupongezwa.

Alisema ni vigumu kufanya maendeleo makubwa bila kukopa, hivyo Rais Samia Suluhu Hassan asiogopeshwe na maneno yanayozungumzwa na baadhi ya watu wasiolitakia mema taifa la Tanzania, achape kazi kwa namna inavyofaa.

“Tunapohitimisha mwaka 2021 hii leo (jana), katika mwaka 2022 tunapaswa kuwa na kaulimbiu yetu ya ‘Twende na Mama Samia’ hii itachochea ari ya utendaji kazi kwa Rais wetu mpendwa ambaye amefanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi,” alisema Msama.

Msama alisisitiza kwamba zipo nchi nyingi zenye maendeleo makubwa ambayo yametokana na mikopo yenye tija kama anayochukua Rais Samia hivyo alitaka asitishike na maneno ya kumkatisha tamaa.

Kauli ya RC wa Simiyu Mkuu wa Mkoa Simiyu, David Kafulila amesema weledi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia uchumi na mikopo unatambulika duniani kote na hana sababu ya kutishwa na maneno yoyote yale.

Alisema hayo akiunga mkono serikali kuendelea kukopa kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Alisema usimamizi wake umeiwezesha nchi kuwa na deni himilivu na lenye kutoa mwelekeo wa taifa katika kukuza uchumi wake na kwamba hata taasisi za kimataifa zinatambua hadi kwenye tafiti zake.

“Ndio sababu Taasisi ya Kimataifa (Moody’s Report 30, August 2021) inayopima uimara wa uchumi kuweza kukopesheka ukaipa Serikali ya Awamu ya Sita daraja la ( B2-Stable), ambalo ni daraja la juu kulinganisha na nchi za Kenya, Ghana, Senegal, Ivory Coast, Mauritius, Namibia, Afrika Kusini na Msumbiji)..” alisema Kafulila.

Alisema kama Moodys ambayo ni taasisi inayoongoza duniani kwa kufanya tathmini za uimara wa uchumi wa Serikali na makampuni

makubwa duniani inaonesha uimara kiasi hiki kwa Serikali ya awamu ya sita, ni kwamba rais yuko katika njia sahihi.

“ Hii taasisi ni mamlaka kwa weledi wa eneo hilo maana inamiliki asilimia 45 ya biashara hii ya kupima uimara wa chumi za Serikali na makampuni makubwa duniani, hivyo ni vema wakosoaji wakawa wanarejea tafiti za kiuchumi badala ya maelezo ya jumlajumla,” alisema Kafulila.

Kafulila alisema hayo wakati akifunga kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) jana, kikao ambacho pamoja na wadau wengine kilishirikisha Benki Kuu ya Tanzania waliotoa tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Kanda ya Ziwa.

Hata hivyo, siku za karibuni Rais Samia alisema kwa namna yoyote ile serikali itaendelea kukopa fedha nje kukidhi mahitaji ya miradi mbalimbali.

“Kwa hiyo kwa njia yoyote kwa vyovyote tutakopa, tutaangalia njia rahisi zitakazotufaa za kukopa kwa sababu fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala kwenye kodi tunazokusanya ndani,” alisisitiza Rais Samia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live