Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Spika ambana Katambi kutoa majibu mepesi bungeni

Katambi Tulia Spika ambana Katambi kutoa majibu mepesi bungeni

Fri, 20 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, amemshukia Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Petrobas Katambi, baada ya kutoa majibu kwamba vijana ambao hawapati mikopo inayotolewa na halmashauri huenda si Watanzania bali ni raia wa Kenya.

Amesema majibu hayo hayaleti picha nzuri na kwamba limewakera vijana wanaohangaika kutafuta ajira na mikopo, hivyo kumtaka arudie kulijibu.

Akizungumza jana bungeni jijini Dodoma Spika, alisema naibu waziri huyo alitoa majibu hayo juzi asubuhi wakati akijibu la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda.

Spika alisema naibu waziri huyo aliulizwa kuhusu mikopo inayotolewa kwa vijana kupitia halmashauri na wakati akijibu, majibu yake yaliashiria vijana wote wenye uhitaji wa mikopo wanapata.

"Majibu hayo hayana uhalisia na wakati akieleza hivyo alikwenda mbali zaidi na kueleza kwamba serikali inachukua hatua na akaeleza mambo ambayo serikali inafanya ili kuhakikisha vijana wanapata ajira pia wanaweza kujiajiri kwa maana alitoa maelekezo ya mafunzo mbalimbali," alisema.

Spika alisema swali hilo lilihusu mikopo na kwamba wako vijana ambao hawapati na serikali ina mpango gani.

"Wakati naibu waziri anajibu hapa alionyesha ishara kwamba vijana wote wenye uhitaji wa mikopo wanapata mikopo na kwamba wapo ambao hawapati mikopo pengine si Watanzania ni Wakenya.

"Waheshimiwa wabunge kwa sababu ni lugha ya mazungumzo inakuwa yale majibu si kwamba ameyaandaa kabla kwa sababu. Ni swali la nyongeza, lakini majibu haya hayajapeleka picha nzuri kwa vijana wetu ambao wanahangaika hapa na pale kujaribu kutafuta ajira lakini kutafuta hiyo mikopo kuboresha shughuli zao ambazo wamezianzisha pengine hawajaweza kuanzisha,” alisema.

Alisema majibu ya namna hiyo hayajajibu swali la mbunge ambaye alitaka kujua watasaidiwaje na kueleza kuwa linapaswa kujibiwa upya.

"Ili mheshimiwa waziri apate nafasi ya kurekebisha yale majibu yake aliyoyatoa awali, swali hili litajibiwa upya. Pamoja na kujibiwa upya maneno hayo yameashiria vijana ambao wamekosa mikopo ni wa Kenya si maneno mazuri pamoja na kwamba ni lugha ya mazungumzo,” alisema.

“Lazima waheshimiwa wabunge na waheshimiwa mawaziri tutumie lugha ambayo itapeleka ujumbe huko nje bila kuwakatisha tamaa vijana ambao wanajishughulisha na mambo mbalimbali," aliongeza.

Spika alisema hayo yamekuwa yakijitokeza bungeni ndiyo maana huwa wanasisitiza maswali ya nyongeza yaendane na swali la msingi ili kupata majibu mahususi.

Katika hatua nyingine, Spika Ackson alisema katika kipindi hicho cha maswali na majibu siku hiyo, Mbunge Viti Maalum, Husna Sekiboko naye aliuliza swali la msingi kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akitaka kujua ni hatua zinazochukuliwa kukomesha kuvuja kwa mitihani nchini.

"Katika swali la nyongeza Mheshimiwa Sekiboko aliuliza kwamba pamoja na hatua hizo zinazochukuliwa na serikali bado uvujaji unaendelea,” alisema huku akinukuu swali hilo: "Ni lini serikali inakwenda kukomesha tabia hii?"

Spika alisema pamoja na mambo mengine naibu waziri alieleza na kunukuu maneno yake: "Mheshimiwa Spika kwanza naomba nimhakikishie mheshimiwa mbunge suala la uvujaji mitihani halipo. Mara ya mwisho mitihani ilivuja mwaka 2008, ulikuwa mtihani mmoja wa somo la hisabati wa kidato cha nne, kutoka mwaka 2008 hakujawahi kutokea uvujaji wa mitihani.”

"Mheshimiwa Spika kinachotokea ni udanganyifu katika mitihani kwenye baadhi ya maeneo."

Spika Ackson alisema kutokana na majibu hayo Mheshimiwa Sekiboko aliomba mwongozo wa Spika na kueleza kuwa naibu waziri amejibu kuwa mitihani haikuwahi kuvuja tangu 2008, lakini Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipewa kazi na Spika kujadili taarifa iliyohusu tatizo la kuvuja mitihani Agosti na Septemba, 2021 ambayo ni mitihani ya vyuo vya afya ya kada ya kati inayosimamiwa na NACTE.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live