Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Spika Tulia awaasa viongozi wa CCM Mbeya

Tulia Ackson Mn.jpeg Spika Tulia awaasa viongozi wa CCM Mbeya

Sat, 24 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amewataka viongozi wa CCM kutokubali chama kuwaharibikia mikononi mwao katikati ya safari ya kuelekea uchaguzi mkuu 2025.

Dk Tulia ametoa wito huo leo Jumamosi Desemba 24, 2022 wakati akizungumza na wajumbe wa CCM mkoa wa Mbeya akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2021/22 katika sekta za elimu, afya, maji na miundombinu.

Amesema miongoni mwa ahadi zilizotekelezwa ni pamoja na miradi ya afya, elimu na miundombinu na bado utekelezaji unaendelea kwa lengo la kuhakikisha mwaka 2025 ahadi zote zinatekelezeka.

“Mwenyekiti wa chama taifa, Rais Samia Suluhu Hassan ametekeleza ilani ya uchaguzi kwa kuboresha miradi ya maendeleo na isitokee watu wachache waliopewa dhamana, chama kikawaharibikia mikononi mwao badala yake waunge mkono juhudi za Serikali,” amesema.

Dk Tulia amesema michakato mbalimbali inaendelea ya kuboresha miradi ya kimkakati na kwamba lengo la Serikali ni kuona wananchi wanapata huduma safi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

“Tunatamani hapa mjini hata kama lami itachelewa miundombinu ya barabara za pembezoni ziboreshwe ili ziweze kupitika sambamba na ujenzi wa vivuko vya muda,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amesema ni wakati sasa wanachama wa CCM kuisemea vizuri Serikali kwa wananchi kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na unaoendelea kufanyika.

“Tunaona Serikali ya Rais Samia imefanya mambo mengi makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwepo sekta ya maji, afya elimu,” amesema Mahundi na kuongeza kwamba ni vyema viongozi waliopewa dhamana kuunga mkono jitihada za Rais.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sabasaba, Ally Mbika amesema Serikali ya awamu ya sita imewajengea mazingira rahisi ya utendaji wa kazi kutokana na utekelezaji wa ilani ya chama kwa kuboresha miradi ya maendeleo.

Chanzo: Mwananchi