Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Spika Tulia aliamsha PHD za Heshima; ‘hizi zinatolewa kama pipi haikubaliki’

Spika Tulia Katulia Spika Tulia aliamsha PHD za Heshima; ‘hizi zinatolewa kama pipi haikubaliki’

Thu, 9 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sakata la watu kupewa udaktari wa heshima limeibuka leo Februari 9, 2023 Bungeni jijini Dodoma ambapo Spika Tulia Ackson alitaka kuwepo na msimamo kama Taifa juu ya PHD hizo za heshima.

Suala hilo liliibuliwa na Mbunge wa Mlalo, Rashid Abdallah Shangazi ambaye aliomba mwongozo wa Spika kutaka kujua vigezo gani vinatumika ili mtu aweze kupewa udaktari wa heshima na kwa kiasi gani vyuo vinavyotoa udaktari huo vinatambulika na Serikali.

“Mheshimiwa Spika katika Bunge lako tukufu, wabunge wanatambulika kwa taaluma mbalimbali. Kabla ya kutaja jina lake, linatangulia jina hilo la taaluma yake. Katika Bunge la 11 nakumbuka mheshimiwa Rita Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, alitunukiwa udaktari wa heshima na alileta cheti na mheshimiwa Spika alimtangaza kama daktari.

“Naomba mwongozo wako, wapo baadhi ya wabunge wamepewa udaktari huo wa heshima tena ni wa muda mfupi je, vyuo vinavyotoa udaktari ni kiasi gani vinatambulika. Je ni vigezo gani vinatumika ili kutunukiwa. Na kwa kiasi gani mamlaka za elimu zinatambua udaktari huu,” aliomba mwongozo Shangazi.

Kabla ya kutoa maelezo ya ziada, Spika Tulia alimsimamisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda atoe ufafanuzi wa mwongozo huo ambapo alieleza jinsi udaktari unavyopatikana na kwamba, wao kama wizara wanaweza kuhakiki endapo wataulizwa na wasipoulizwa hawaingilii.

Baada ya majibu hayo, Spika Tulia ndipo alipokazia kwa kusema anakubaliana na majibu ya waziri lakini kama Taifa lazima kujua nini tunataka kwani athari zake zinaweza zisionekane sasa zikaja kuonekana baadaye.

“Ananapopewa udaktari wa heshima Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamefanya utafiti kuhusu kazi alizozifanya sio tu alipokuwa Rais tangu aanze kufanya kazi. Wamezitazama hizo kwa pamoja, wakazikusanya, wakazipima kwa vigezo walivyoweka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba katika vigezo hivi tunaweza tukamtunuku digrii ya Falsafa hiyo ambayo amepewa.

“Sasa tutafika mahali ambapo wale wanaopewa kwa heshima wanayostahili hawana tofauti na hawa wanaolipa pesa ili wapewe. Sisi kama taifa lazima tufahamu utaratibu upi tunataka kwenda nao kwa sababu tusipofanya hivyo tunajipoteza wenyewe.

“Sisi kama viongozi lazima tuoneshe mfano. Mtoto wako umempeleka shule ili asome atie bidii leo wewe kama mzazi unalipa pesa ili upewe digrii ya heshima unampa mfano gani yule kijana aliyeko shule unaomkazania kusoma? Kwamba wewe tafuta pesa ukishatafuta pesa kalipe utapewa digrii ya heshima,” alisema Spika Tulia.

Spika Tulia aliongeza; “…hizi zinazoletwa na wageni kuuzwa kama pipi haikubaliki. Tunajivunjia heshima kama taifa hasa kwenye eneo la elimu. Vyuo vinavyotambulika duniani havitoi digrii kila wiki kila wiki kila mwezi kila mwaka.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live