Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sirro: Wanasiasa zingatieni sheria

4438d110b280a3114d30175521654eb8.jpeg Simon Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini

Wed, 29 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanasiasa nchini wametakiwa kuitumia vizuri haki yao ya kuandaa mihadhara na mikutano ya kisiasa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa bila kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani na inapotokea wamezuiliwa kwa sababu yoyote itakayotajwa kama hawajaridhika wana haki ya kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na si kutunisha misuli.

Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni nchini juzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi

(IGP), Simon Sirro alisema jeshi hilo limekuwa likifanyakazi kwa mujibu wa sheria kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza katika hotuba yake wakati wa mkutano wa vyama vya siasa ulioandaliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba mikutano hiyo inapaswa kufanyika kwa kufuata taratibu za kisheria.

“Kuna watu wanasema tunazuia mikutano, bahati nzuri Rais amesema Watanzania wote wamesikia kwamba sheria zipo, taratibu zipo, tufuate sheria. Wanasiasa wafuate sheria na sisi tusimamie sheria, kwa hiyo

tumemuelewa na tumekuwa tukifanya hivyo siku zote na tatizo kubwa limekuwa likijitokeza pale ambapo OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) anapokuwa ametoa sababu zake za kuzuia, sheria iko wazi kabisa, wanatakiwa wakate rufaa kwa Waziri (Mambo ya Ndani) na mimi huwa nawaambia, lakini hawakati rufaa,” alisema.

Akizungumzia tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwa Jeshi la Polisi ikiwamo malalamiko ya uonevu, ubambikaji kesi, rushwa na lugha chafu, Sirro alisema Watanzania ni lazima

waelewe kuwa polisi ni binadamu waliolelewa na kupita katika malezi na makuzi tofauti, hivyo hawawezi kukosekana wasiokuwa na maadili lakini wamekuwa wakiwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria huku akiwataka raia kusimama katika nafasi zao bila kuleta ushawishi au kusababisha matendo hayo kutokea.

“Kesi ni ushahidi, kama ingekuwa watu wote wanabambikiwa kesi basi kusingekuwa na watu wanaofungwa wangeachiwa na mahakama, lakini pia wapo watu ni wahalifu wameachiwa wapo mtaani kwa sababu

tu ushahidi ulikuwa hafifu kuwatia hatiani. Nakubali kuwa wapo askari wasio na maadili ambao wanafanya hivyo lakini tunapowagundua tunawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Aidha, Sirro aliwataka wazazi kuwa makini katika malezi ya watoto wao ili kuwa na taifa lenye maadili na kuleta tija katika maendeleo ya nchi na usalama kwa ujumla.

“Nitoe rai kwa wazazi wote wahakikishe wanapoona watoto wao wanaonesha hali ya mabadiliko hasi wajaribu kuwafuatilia nyendo zao, kama watagundua tatizo lolote au tishio la kiusalama wasisite kutoa taarifa kwetu ili tuweze kuwasaidia kuwapa ushauri nasaha.”

“Sisi tunapomchukua kijana si kwa ajili ya kumfunga, tunalo dawati kwa ajili ya kuwasaidia kuondokana na mawazo ya uhalifu na kuwafanya warudi katika hali ya kawaida,” alisema Sirro na kutolea mfano wa kijana mmoja wa Tanga aliyetaka kuacha shule na kuingia katika makundi ya uhalifu, wazazi wake walipomgundua wakatoa taarifa Polisi akapata msaada na kurudi katika maisha ya kawaida.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live