Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri mpya wapinzani kuhamia CCM yatajwa

39945 Pic+siri+mpya Siri mpya wapinzani kuhamia CCM yatajwa

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amesema uamuzi wa CCM kuwateua madiwani waliotoka upinzani kugombea tena nafasi hizo ulikuwa ni moja ya mikakati ya ushindi uliolenga kurejesha kata zilizokuwa upinzani kuwa mikononi mwa chama hicho tawala.

Kauli hiyo ya Kasesela imekuja wakati ambapo Watanzania walielezwa kuwa kuhama kwa madiwani na wabunge wa upinzani ilikuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Mkuu huyo wa wilaya aliyasema hayo juzi katika kongamano la miaka 42 ya kuzaliwa kwa CCM lililofanyika mjini hapa, wakati akijibu hoja iliyoibuliwa na wajumbe ambao walidai kusikitishwa na uamuzi wa kuwapokea madiwani kutoka upinzani kisha kupitishwa kugombea tena nafasi hizo huku wao wakitoswa.

Mkoani Iringa zaidi ya madiwani watano walihama kutoka Chadema na kujiunga na CCM kisha kupitishwa kugombea tena nafasi zao ambapo waliibuka washindi.

Mwaka jana, hamahama ya wawakikilishi wa wananchi katika vyombo vya kutunga sheria ilikuwa nchi nzima ambapo iliwahusisha pia wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji waliojizulu na kuhamia CCM ambapo kwa nyakati tofauti walipitishwa kugombea tena.

Hata hivyo, Novemba 15, CCM ilifunga dirisha la kuwapokea wanaohamia ikiwa na jumla ya wabunge 10 kutoka Chadema na CUF, huku madiwani wakiwa zaidi ya 130 kutoka vyama tofauti.

Juzi, katika kongamano hilo, mwanachama wa CCM kutoka kata ya Ilala mjini humo, Elizabeth Mpogole alisema walipata wakati mgumu kuwapigia kampeni watu aliodai waliwahi kuwatukana wakiwa upinzani.

Alisema jambo hilo limekuwa likiwavunja moyo na kujiona hawapewi thamani na chama chao, ilhali kipaumbele wakipewa ‘wapinzani’ waliohamia na kisha kupewa nafasi za kugombea nafasi zilezile.

“Naomba tuwe tunakumbukwa hata kualikwa kwenye vikao hasa wanapokuja wageni ili na sisi tupate nafasi ya kushiriki katika chama na sio kusahaulika kwa sababu tulianguka katika chaguzi na kuonekana hatufai tena,” alisema Mpogole.

Akijibu, Kasesela ambaye pia ni kada wa chama hicho alisema, “Tuliamua waliohamia CCM kutoka upinzani wagombee ikiwa ni moja ya makubaliano ya wao kuhamia na tulikubali kwa sababu ulikuwa ni mpango wa chama kuhakikisha kata zote zinarudi CCM.”

Kasesela alisema wana-CCM wanapaswa kujua kuwa kila kitu kilikuwa kwenye makubaliano na wote waliogombea tena nafasi zao ilikuwa ni mkakati wa wao kujivua na kukubali kuhama.

Alipoulizwa kwa simu iwapo huo ndio ulikuwa mkakati wa kuwachukua madiwani nchini nzima, katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Ngemela Lubunga alisema hawezi kusema chochote kwa kuwa hakuwepo kwenye mkutano huo. “Mimi kwa sasa niko Mwanza kwenye ziara, nisubiri nirudi kesho au keshokutwa nitafuatilia kilichosemwa kwenye huo mkutano,” alisema.

Akizungumza katika kongamano hilo, mlezi wa CCM mkoani Iringa, ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema baada ya wana CCM kuonyesha uchungu dhidi ya wapinzani na kutaka kurejesha ubunge Jimbo la Iringa Mjini, atafanya ziara kuhakikisha linarudi mikononi mwa chama hicho mwakani.

Jimbo hilo kwa sasa liko chini ya mchungaji Peter Msigwa wa Chadema.

Nyongeza na Elias Msuya.



Chanzo: mwananchi.co.tz