Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Sio dosari ni hujuma’

82699 Hujuma+pic ‘Sio dosari ni hujuma’

Mon, 4 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimesema kasoro zinazolalamikiwa katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ni hujumu na si dosari.

Chama hicho kimemtaka Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo Suleiman Jafo kuchukua hatua dhidi ya vitendo ambavyo kimesema wanafanyiwa wagombea wa vyama vya upinzani wanapokwenda kuhukua fomu za kuwania uongozi wa ngazi hiyo.

Vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamikia vitendo vya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ambao hutoa fomu hizo, kukimbia ofisi wakati wagombea wa upinzani wanapokwenda, kutoa fomu zenye kasoro, kukubali watu wanaochukua fomu kwa majina ya vyama vya upinzani bila uthibitisho na wengine kufanyiwa fujo.

Uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa utakaohusisha wenyeviti wa mitaa, vitongoji na vijiji umepangwa kufanyika Novemba 24 na unasimamiwa na watendaji wa kata, ambao huapa kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi hiyo kuwahakikishia wanachi kuwa watasimamia haki.

Tayari Waziri Jafo ameshakiri kuwepo kwa vitendo hivyo na kuahidi kuchukua hatua, lakini ACT Wazalendo wanaona kuna hujuma na si dosari za kawaida, huku Chadema ikiwa imeandika barua mbili kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu kulalamikia kasoro tisa na nyingine kwa Jafo.

Jana, mratibu wa mawasiliano wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa ACT Wazalendo, Mbarala Maharagande alisema Waziri Jafo anapaswa kuwawajibisha watendaji wanaofanya hujuma kwa makusudi. Alisema wanachama wake wanaojitokeza kuchukua fomu hizo wanakumbana na vikwazo vinavyolenga kuwakatisha tamaa.

Alisema hujuma nyingine ni kukosekana kwa mihuri, kuchongeshwa mihuri ya bandia ya vyama na wasimamizi kuweka masharti ambayo hayapo.

Alitolea mfano wa Jimbo la Liwale ambako alisema wagombea wa upinzani wameshindwa kuchukua fomu kutokana na wahusika kutokuwepo kwenye ofisi zao.

“Katika jimbo la Liwale lenye kata 20 kwa kiasi kikubwa wagombea wa upinzani wamekosa fomu, baada ya kusukumana ndiyo jana zimetolewa katika kata tatu hii ni hatari,” alisema.

“Kuna maeneo wagombea wanatakiwa kutoa nakala ya fomu, sehemu nyingine ofisi za wasimamizi wa uchaguzi kufungwa, kukosekana mihuri, vitisho na kutekwa kwa wagombea na viongozi ni baadhi ya hujuma,” alisema.

“Waziri Jafo anapaswa kujua kuwa kuna tofauti kati ya hujuma, njama ovu na dosari na upungufu. Hujuma na njama ovu hizi zinafanywa dhidi ya vyama vya upinzani na wagombea wake pekee na hakuna lalamiko hata moja tulilolisikia na kushuhudia kutoka CCM.”

Pia Maharagande aliwataka viongozi wa dini na wastaafu kuzungumzia haki na si amani pekee.

Chadema, CCM watwangana

Wakati ACT ikieleza hayo, mkoani Morogoro wanachama wa CCM na Chadema wamepigana baada ya wafuasi wa Chadema kwenda nyumbani kwa mgombea wa CCM kuhoji sababu za kumtaka mgombea wao kujitoa kwenye uchaguzi.

Inadaiwa kuwa katika kata ya Chisano Wilaya ya Kilombero, mgombea uenyekiti wa kitongoji cha Mkuyuni wa tiketi ya CCM, Kassim Malawa alitoa maneno ya vitisho kwa mgombea wa Chadema, Pius Chitikitila.

Inadaiwa mgombea huyo wa CCM alimtisha mwenzake akitaka asigombee ili abakie peke yake.

Mwenyekiti wa Chadema wa wilaya, Shabani Mikongolo alisema vurugu hizo ziliibuka jana mchana baada ya viongozi wa Chadema kwenda kwa mgombea huyo kuhoji sababu za kumtishia mwenzao.

“Kabla ya mazungumzo lilitokea kundi la vijana ambao ni wa CCM na kuanza kuwashambulia viongozi wa Chadema, waliwapora fedha na simu,” alisema Mikongolo.

Alisema katika vurugu hizo, viongozi watatu wa Chadema walijeruhiwa na kwamba polisi walipofika eneo hilo waliwakamata wananchi na viongozi wa Chadema.

Alisema viongozi waliojeruhiwa ni katibu wa Jimbo la Mlimba, Tumaini Mwakalasya, mjumbe wa kamati ya utendaji ya jimbo hilo, Erasto Mwasajone na katibu wa tawi la Chinaso, Enesius Msoma.

Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Clarence Mgomba alisema wanachama wao si wakorofi akidai kuwa Chadema wamepata taharuki baada ya kuona wagombea wa CCM wanakubalika.

Alisema vurugu hizo zimefanywa na wanachama pamoja na viongozi wachache wa Chadema.

“CCM hakuna ugomvi wala vurugu kwa sababu tayari mgombea wetu ameshapatikana na anaungwa mkono na wanachama wote,” alisema.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Wilbroad Mutafungwa alisema hana taarifa zozote kuhusu vurugu hizo.

“Nipo Malinyi na mtandao uko chini hivyo mawasiliano yamekuwa ya shida,” alisema Kamanda Mutafungwa. “Nikifika mahali kwenye mawasiliano mazuri nitawasiliana na maofisa wangu ili wanipe hizo taarifa. Ila kwa sasa sina ninalojua kuhusu vurugu hizo.”

Chanzo: mwananchi.co.tz