Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sintofahamu Uchaguzi Mkuu

83590 Pic+uchaguzi Sintofahamu Uchaguzi Mkuu

Thu, 14 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chadema na ACT-Wazalendo kujitoa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kumeibua sintofahamu.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa, wanaona hali iliyotokea sasa huenda ikawa ishara ya athari kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kutokana na vyama hivyo viwili kutaka kusimamisha wabunge, madiwani na rais bila kuwa na msingi wa viongozi wa ngazi za chini.

Pia ikiwa madai ya vyama hivyo ya kujitoa katika uchaguzi huu hayatashughulikiwa ina maana mvutano huo unaweza kuvuruga mchakato wa uchaguzi mkuu .

Vyama hivyo viwili vya upinzani vimesema wazi havina imani na vyombo vinavyosimamia uchaguzi kwa sasa.

Si mara ya kwanza Chadema kutoshiriki uchaguzi, imewahi kufanya hivyo katika chaguzi ndogo kadhaa za ubunge hivi karibuni na CUF imewahi kususia uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar, Machi mwaka 2016.

Chadema iliyotangaza uamuzi wa kujitoa juzi kabla ya kufuatiwa na ACT- Wazalendo jana, wametaja sababu za kujitoa kuwa ni figisufigisu zilizofanyika katika uchukuaji, urejeshaji wa fomu za kugombea na uteuzi wa wagombea wao.

Vyama hivyo vimedai vimeamua kutokata rufaa kutokana na kukosa imani na kamati za kushughulikia suala hilo.

Hali hiyo itatoa mwanya kwa wagombea wa CCM katika maeneo mengi nchini kupita bila kupingwa na kushika madaraka serikali za mitaa maeneo karibu yote nchini.

Pia uamuzi wa vyama hivyo kujitoa ni pigo kwa wananchi kwani utawakosesha haki ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Hali hiyo inaweza kusababisha tatizo la uongozi katika serikali za mitaa kwa kuwa viongozi watakaopita bila kupingwa wanaweza wasiwajibike kwa wananchi kwa sababu hawakuchaguliwa kwa kura.

Chadema ambao katika uchaguzi mkuu wa urais 2015 walipata kura milioni sita wanaweza kuwa na wakati mgumu kwa wapiga kura wake hao kama bado walikuwa wamebaki na chama hicho.

Kama mchakato wa kujiandikisha ulivyokuwa wa kusuasua na kuhitaji msukumo wa ziada kwa wananchi kutojitokeza, huenda pia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, ikashuhudiwa idadi ndogo ya wapigakura kutokana na ‘sarakasi’ walizoziona kwenye maeneo yao.

Maoni ya wadau

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema wananchi wameshuhudia figisufigisu zilizotokea kwenye mchakato wa uchaguzi wa mitaa “tunajipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Faraja Kristomus alisema hali inayoshuhudiwa katika uchaguzi huo itawakatisha tamaa wananchi kuelekea 2020 na watapoteza imani na mifumo ya uchaguzi, hali ambayo ikiendelea inaweza kuzua chuki na vurugu.

“Sitaki kuamini kwamba wale wagombea wa CCM ndio wanaojua kanuni kuliko wa vyama vingine. Ili kuondokana na hali hii tunatakiwa kuongeza kasi ya kutoa elimu ya uraia kuhusu uchaguzi na kuhusu uongozi,” alisema Kristomus.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema hali ilipofikia sasa inakatisha tamaa wananchi kushiriki katika shughuli za kisiasa kwa sababu hawana imani na mifumo ya usimamizi wa demokrasia.

“Chadema na ACT-Wazalendo wana sababu za msingi za kususia uchaguzi huo kwa sababu CCM hawataki ushindani wa haki ndiyo maana wamefungia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara ili wasipate kukutana na wananchi. Natarajia siku ya uchaguzi ushiriki utakuwa hafifu,” alisema Profesa Mpangala.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk John Masalu alisema haitakiwi kujadili kama vyama hivyo vipo sahihi au la bali kama hoja wanazitoa zina ukweli na nini kifanyike.

Alisema suala la demokrasia linaanzia kwa wananchi kwa sababu wao ndiyo chanzo cha mamlaka yote ya nchi.

“Mimi nadhani wana hoja za msingi za kujiondoa kwenye uchaguzi huo kwa sababu wameenguliwa karibu nchi nzima, hivyo, wakisema wanashiriki, ushiriki wao utakuwa wa namna gani wakati hawana wagombea,” alihoji Dk Masalu.

Naye wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke ameonya kuwa kitendo cha Chadema na ACT-Wazalendo kususia uchaguzi inamaanisha kuwa kote nchini hawatakuwa na wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji wala wajumbe na inaweza kuwaathiri kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani.

“Viongozi wa mitaa wanahusika na shughuli za wananchi, sasa vyama hivi vinaweza kujikuta vikipoteza viti vingi vya ubunge katika uchaguzi mkuu,” alionya.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) Dk Frank Tilly alionya kujitoa kwa Chadema na ACT-Wazalendo katika uchaguzi kuwa hakuleti picha nzuri kwa nchi ya demokrasia na mfumo wa vyama vingi vya siasa kwani kunafanya chama kimoja kusimama katika uchaguzi kinyume na matarajio.

“Lakini wao pia wanapaswa kutambua kuwa kama hawatakuwa na viongozi wa mitaa itakuwa ngumu kwao kufanya vizuri uchaguzi 2020 kwa sababu viongozi wa chini ndiyo wahamasishaji,” alisema..

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema kujitoa katika uchaguzi huo halikuwa suluhisho kwani kunaweza kuwaathiri huku akibainisha kuwa hakuna chama kilichowahi kujitoa katika uchaguzi na kikaendelea kuwa imara.

“Kwa mfano Zanzibar, CUF ilijitoa katika uchaguzi wa marudio 2015 na kuwafanya kutetereka. Hivyo vyama vinapaswa kujua kuwa uchaguzi ni kama vita vinapaswa kujipanga na wajue kuwa hujuma na figisu ni lazima viwepo,” alisema Dk Mbunda.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Luisulie ameonya kuwa vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo kujitoa katika uchaguzi huu kuna uwezekano vikajitoa katika uchaguzi wa mwaka 2020 kama madai wanayolalamikia hayatafanyiwa kazi.

“Sijui wahusika wa chaguzi hizi wataamua nini, lakini hali hii ikiachiwa itakuwa na athari uchaguzi wa 2020,” alisema.

Naye wakili wa kujitegemea, Faraja Mangula alisema miongoni mwa sababu za Chadema kujitoa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa ni kukosekana kwa tume huru hivyo ni vyema wakahakikisha inapatikana kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020.

“Tume iliyopo wanasema siyo huru hivyo wakati uliobaki ndiyo wanapaswa kuutumia kikamilifu ili kuhakikisha kilio chao kinasikilizwa,” alisema Mangula.

Chanzo: mwananchi.co.tz