Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Singida Mashariki waeleza jinsi wanavyomkosa mbunge wao

16223 Pic+singida TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Singida. Tarehe kama ya leo, Septemba 7 mwaka jana itaendelea kukumbukwa kwa miaka mingi. Ni siku ambayo Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alimiminiwa risasi zaidi ya 30, huku 16 zikiingia mwili mwake.

Kufuatia tukio hilo, wakazi wa jimbo lake lake la Singida Mashariki wameeleza jinsi wanavyomkosa kama mhamasishaji wa shughuli za maendeleo.

Wanavyomzungumzia

Mkazi wa Kijiji cha Ikungi, Jingu Jackson alisema Lissu aliaminiwa na watu wa jimbo lake na Watanzania wengi kwa sababu ametoa maisha yake kuwatumikia wanyonge.

“Tarehe 7 Septemba, nchi hii iliwekewa doa la kuuana mchana kweupe. Na inadaiwa wauaji ni watu wasiojulikana. Watu wengi wameingiwa na hofu,” anasema Jingu.

Jingu ambaye ni diwani wa Kata ya Iseke alisema kutokana na hofu hiyo ndio sababu ya baadhi ya viongozi waliopo upinzani kuhama vyama vyao.

“Wabunge na madiwani wa upinzani wa vyama vya upinzani, walitambua Lissu ni kiongozi jasiri lakini baada ya kuona kiongozi huyo kushambuliwa wamepata hofu kuwa sasa zamu yao imefika,” alidai Jingu.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ikungi, Omari Toto alisema jaribio la kumuua Lissu limewavunja moyo wananchi katika kujiletea maendeleo binafsi na ya jimbo lao.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni diwani wa Ntuntu, anasema tangu Lissu ashambuliwe wananchi wamekosa mhamasishaji wa maendeleo.

Mkazi kijiji cha Ighuka, Athumani Kidimanda alisema Mungu amewajalia Watanzania kuweka pembeni tofauti zao za itikadi, dini au matukio mabaya kama lililomtokea na sasa wako pamoja.

“Kwa kifupi, kwa matukio ya raha kama harusi kuzaliwa, vifo, majanga huwa tunakuwa kitu kimoja, namwombea ndugu yangu Lissu apone na akirudi jimboni afuate nyayo za wenzake waliorejea CCM,” anasema Kidimanda ambaye ni mwana CCM.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikungi, Msandae Sambe anadai kuwa kutokuwapo Lissu kumechangia jimbo la Singida Mashariki ‘kukomolewa’ kimaendeleo.

Anafafanua kuwa hakuna uwiano mzuri katika utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo kati ya Singida Mashariki na Singida Magharibi wakati majimbo yote yako wilaya moja ya Ikungi.

Soma zaidi: VIDEO: Niliyoyaona siku Tundu Lissu aliposhambuliwa

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu anasema mgao wa fedha za maendeleo katika wilaya hiyo yenye majimbo mawili ya Singida Mashariki na Singida Magharibi unazingatia usawa na mahitaji halisi ya miradi.

“Haya majimbo mawili ni yetu na yote, tunayatendea haki stahiki. Mfano hai ni kwamba mwaka jana halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, imepeleka mamilioni ya fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji katika vijiji vya Ntewa na Ntuntu. Hakuna jimbo linalobaguliwa. Hata fedha za mfuko wa jimbo zinasimamiwa na kamati maalumu kama kawaida,” anafafanua.

Maandalizi kumpokea

Wakati haifahamiki Lissu anarejea lini kutoka Ubelgiji, Toto anasema wameshaanza mikutano kwa ajili ya kuweka mipango mizuri ya kumpokea Lissi atakaporejea jimboni.

“Maandalizi ya mapokezi yake yameanza mapema kwa sababu tunatarajia kupokea ugeni mkubwa kutoka ndani na nje ya mkoa,” alisema.

Kaka yake Lissu, Alute Mughway alisema kwa sasa hawajui tarehe wala siku ndugu yao huyo atarudi nyumbani, ingawa ametoka hospitali na kila siku wauguzi wanamhudumia akiwa kwenye nyumba aliyofikia huku akiendelea na mazoezi.

Soma zaidi: VIDEO: Lissu asimulia mwaka mmoja nje ya Bunge

Chanzo: mwananchi.co.tz