Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Silinde asema Dk Mpango atafungwa, atoa ombi kwa Ndugai

61140 Pic+silinde

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Momba (Chadema) David Silinde amemuomba Spika wa Bunge, Job Ndugai kuunda timu ambayo itapitia mapango wa maboresho ya biashara ‘blue print’ na kuishinikiza Serikali kuitekeleza.

Ameyasema hayo leo Jumatatu Juni 3, 2019 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango 2019/2020.

“Tukiwa wajumbe wa kamati (Bajeti) kila taasisi inayokuja wamepelekewa bango kitita, taasisi zote hakuna inayoridhika. Tunaweza kusema propaganda lakini uchumi hauna propagranda,” amesema.

Amesema Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyekuwa Tume ya Mpango wakikutana na Dk Mpango wa leo ni vitu tofauti na kwamba wanatofautiana kwa kila kitu.

“Wizara inafanya reallocation (kuhamisha fedha) ya fedha bila ridhaa ya Bunge nilisema mwaka jana na leo wamelirudia hilo hilo,” amesema.

Amesema zaidi ya Sh353 bilioni ambazo Bunge halijapitisha na wala hazipo katika vitabu vya kuhamisha fedha (reallocation).”

Habari zinazohusiana na hii

Hata hivyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na  Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amempa taarifa kuwa kifungu 28  cha sheria ya bajeti imempa uwezo wa kuhamisha kiasi kisichopungua asilimia tisa na kwamba Sh353 bilioni ni asilimia moja ya kiasi alichopewa mamlaka.

Akiendelea kuchangia, Silinde amesema hayo yamo ndani ya sheria na kwamba baada ya kumaliza muda wake wa uongozi watakutana mahakamani.

“Wasikudanganye utafungwa kwa mambo haya. Criminal (jinai) haifi, watu wanaokushangilia sana usiwafurahie kuliko wale wanaokuambia ukweli,” amesema.

Aidha, amesema wizara hiyo imeshindwa kusimamia sera zake na kwamba sheria walizonazo lazima ziendane na malengo ya nchi.

“Ukiangalia sera ya fedha, sera ya biashara, sera ya kilimo zinatofautiana kabisa. Tunajadili uchumi wa viwanda lakini ukienda kuangalia sera ya fedha, biashara na kilimo zinatofautiana unafikiaje malengo? amehoji.

Amesema Serikali ikaja na blue print hakuna hata mmoja aliye tayari katika kutekeleza na kwamba kuna mikanganyiko kibao.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Angella Kairuki alimweleza kuwa amepotosha na kwamba blue print itaanza kutekelezwa Julai 2019.

“Hakuna anayepinga hilo na hata sekta binafsi wanasikiliza. Na ukiangalia baadhi ya maeneo umeanza kutekelezwa,” amesema Kairuki.

Akiendelea kuchangia, Silinde amemuomba Spika aunde timu ambayo itapitia blue print na kushinikiza Serikali katika utekelezaji wake.

Chanzo: mwananchi.co.tz