Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sifa za mgombea Serikali za mitaa kuwa kada CCM zagonganisha vichwa wabunge

63006 Pic+mgombea

Mon, 17 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unaweza kusema Alhamisi iliyopita Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alichafua hali ya hewa bungeni baada ya kueleza kuwa moja ya sifa ya wagombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba mwaka huu ni kuwa mwanachama wa CCM.

Dk Mpango alitoa kauli hiyo wakati akihitimisha kuwasilisha bajeti ya Serikali Kuu mwaka 2019/2020 na kusababisha wabunge wa upinzani na CCM kusimama kwa takribani dakika tatu huku kila upande ukitoa kauli.

Wakati wabunge wa upinzani wakipiga meza na kuimba “CCM, CCM, CCM”, wenzao wa CCM walishangilia kauli hiyo na kusababisha Dk Mpango kushindwa kuendelea na hotuba yake kwa dakika hizo.

Spika Job Ndugai alilazimika kutumia nguvu ya ziada kuwatuliza wabunge walioonekana kukerwa na kauli hiyo ambayo Dk Mpango alisisitiza kuwa ina baraka kutoka kwa Rais John Magufuli huku kaimu mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Joseph Selasini akiwatuliza wabunge wa upinzani.

Kauli za wabunge

Wakizungumzia kauli hiyo ya Dk Mpango, Selasini ambaye ni mbunge wa Rombo alisema, “Dk Mpango ni kama amebadili taaluma yake na kuidhalilisha wizara anayoiongoza na bajeti aliyokuwa akiisoma. Yeye si mkurugenzi wa uchaguzi, hana mamlaka yoyote ya kutoa au kuelezea sifa za wagombea wa uchaguzi katika ngazi zozote.”

Pia Soma

“Yeye si katibu mwenezi wa CCM na hakuwa na mamlaka ya kupiga debe. Alitumia muda wa Watanzania vibaya.”

Alisema kauli hiyo ni uvunjaji wa Katiba ya nchi inayoruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa, kwamba hata katika chaguzi mbalimbali vyama vinavyoshiriki ni vingi, si CCM pekee hivyo kueleza kuwa wagombea wa chama tawala ndio wanaofaa kuchaguliwa ni sahihi.

“Alichokifanya Dk Mpango ni mfululizo wa kuvunja sheria unaofanyika hivi sasa nchini kwetu. Ila kauli yake pia inaonyesha woga mkubwa wa kushindwa kwa sababu uchumi wa nchi umeanguka maana ukiangalia mzunguko wa fedha na utekelezaji wa maendeleo ni masikitiko makubwa.”

“Kauli yake inaashiria hofu. Hivi mwananchi ukimwambia habari ya ujenzi wa reli anakuelewa? Anataka aone dawa, huduma bora za hospitali. Maisha hayajabadilika na wameona kutumia muda ambao Watanzania wote wanawasikiliza (wakati wa kusomwa bajeti) ili waeleze hilo jambo kuwajengea hofu wananchi,” amesema Selasini.

Amewataka viongozi wa Serikali kufanya kazi kwa ajili ya wananchi wote si chama, “Ndio maana baada ya kauli yake ikaibuka zomeazomea. Sijawahi kuona wakati wa uwasilishwaji wa bajeti yanazungumzwa mambo kama haya. Hii haijawahi kutokea.”

Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali alisema, “Ni kauli ya ovyo sana na imechangiwa na uongozi wa Bunge kutotenda haki, kipengele kile kilitakiwa kufutwa na Bunge kama ambavyo walikuwa wakifuta hotuba za upinzani.”

Kwa mujibu wa Bobali, kama ambavyo Bunge lilikuwa likihariri maoni ya wapinzani kuhusu bajeti za wizara mbalimbali tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti Aprili 2 mwaka huu, ndicho kilichopaswa kufanyika katika hotuba hiyo ya bajeti kwa kuhariri eneo linaloeleza sifa ya anayepaswa kuchaguliwa ni kuwa kada wa CCM.

“Ile ni kampeni ya kabla ya uchaguzi na haipaswi kufanywa na mtu kama Dk Mpango, alifanya vile kwa sababu tukio lile lilikuwa ‘live’ sasa wamechombeza wakiwafanya Watanzania wajinga. Ilipaswa kuondolewa katika taarifa za Bunge.”

Mbunge wa Kasulu vijijini (CCM), Augustine Vuma amesema, “Yale ni maoni binafsi ya Dk Mpango na binafsi naona kauli yake ni kama iliyowahi kutolewa na Julius Nyerere aliyesema anang’atuka lakini ana amini Tanzania bila CCM imara itateteleka na kwamba rais anaweza kutoka chama chochote cha siasa lakini rais bora atatoka CCM.”

“Alichokisema Mpango ni kuvaa viatu vya Nyerere kwa mapenzi yake ndani ya CCM na jinsi anavyokijua chama katika weledi wake wa kupika viongozi. CCM ni chama ambacho kinawasaidia Watanzania, ndio maana akawashauri Watanzania kuwa kiongozi bora wa Serikali za mtaa atoke CCM, yupo sahihi kabisa.”

Mbunge wa Mafinga mjini (CCM), Cosato Chumi alisema, “Nilivyoielewa hii kauli ni kwamba CCM kuanzia misingi ya kuanzishwa kwake, muundo wake na uendeshwaji wake huwa ni kwa vikao na ratiba zilizonyooka si kwa nadharia za ubabaishaji.”

“Maana yake hata upatikanaji wa wagombea hupitia katika michujo hivyo ukipata mgombea wa mtaa au kijiji anakuwa amepita kati tanuru limemuivisha kustahili kuwa mgombea ndio maana ya ile kauli.”

Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Salehe alisema, “Kauli ya Dk Mpango ni kama mtu aliyemuweka inzi katika pilau. Kaeleza masuala mengi yatakayofanywa na Serikali mwaka 2019/2020 lakini mwishoni akaharibu.”

“Hakuwa na haja za kutoa sifa za wagombea wa uchaguzi maana yeye (Dk Mpango) ni waziri wetu wa fedha, alipaswa kutueleza Serikali ilivyojipanga kifedha kwa ajili ya uchaguzi huo.”

Salehe alisema kauli hiyo ya Dk Mpango huenda ikaibua hali ya sintofahamu kuanzia kesho wabunge watakapoanza kujadili bajeti hiyo.

“Ameharibu kiasi ambacho ‘mood’ za wabunge bungeni kuanzia Jumatatu (kesho) itakuwa mbaya sana na Spika siku ile (Alhamisi iliyopita) alitumia busara sana mpaka jambo hilo likapoa. Tunakwenda katika bajeti ambayo itakuwa ya kisiasa badala ya kujadili masuala ya msingi,” alisema Salehe.

Alichokisema Mpango

Wakati akihitimisha kuwasilisha kusoma bajeti hiyo, Dk Mpango aligusia uchaguzi huo na kuwataka Watanzania wenye sifa zifuatazo ndio wachaguliwe.

“Sifa ya 10 awe anatoka ndani ya chama cha siasa kinachotetea maslahi na haki za wanyonge na chama hicho ni CCM, “ alisema Dk Mpango.

Baada ya kauli hiyo ambayo Dk Mpango aliirudia mara tatu, wabunge wa upinzani walisimama na kuibuka hali ya sintofahamu bungeni.

Ndugai alitamka zaidi ya mara tatu kuwataka wabunge kukaa ili Dk Mpango amalize kusoma hotuba hiyo ya bajeti lakini wawakilishi hao wa wananchi hawakuwa wepesi kutii agizo hilo.

Kwa upande wake Selasini alilazimika kusimama na kuwageukia wabunge wa upinzani na kuwanyoooshea mikono akiashiria waketi jambo ambalo baada ya dakika tatu lilitekelezwa na wabunge hao.

Dk Mpango alipopewa nafasi ya kuendelea kuwasilisha amesema alichokisema kina baraka ya Rais John Magufuli.

Chanzo: mwananchi.co.tz