Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siasa zisiwagawe wananchi Monduli

15671 Pic+siasa TanzaniaWeb

Wed, 5 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kampeni za uchaguzi wa mdogo wa jimbo la Monduli mkoa wa Arusha zimeanza kwa kasi huku vyama vinane vikichuana kuwania jimbo hilo.

Jimbo la Monduli lina historia ya kipekee nchini, kwani ndilo pekee ambalo limewahi kutoa wabunge wawili walioteuliwa kuwa mawaziri wakuu, Edward Sokoine na Edward Lowassa.

Katika kampeni hizi upinzani mkubwa kama ilivyotarajiwa, upo baina ya CCM na Chadema, ambavyo vina wafuasi wengi katika jimbo hilo. Vyama vingine vinavyochuana ni ACT- Wazalendo, Tadea, Demokrasia Makini, NRA, AFP na DP.

Uchaguzi wa Monduli unafanyika, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, Julius Kalanga kujiuzulu ubunge na kujiunga na CCM ambayo imemteua kugombea nafasi aliyojizulu.

Kwa sasa Kalanga anachuana vikali na jirani yake kutoka katika kata aliyozaliwa ya Lepurko, ambaye ni diwani wa kata hiyo kupitia Chadema, Yonas Laizer.

Hivyo mgawanyiko wa kisiasa katika uchaguzi wa Monduli, unaanzia nyumbani kwa wagombea hawa, kwani pia kabla ya Kalanga kugombea ubunge katika jimbo hilo, ndiye alikuwa diwani wa CCM katika kata hiyo.

Lakini pia uchaguzi wa Monduli, umemrejesha katika ulingo wa siasa, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 20 na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye sasa yupo Chadema.

Lowassa ndiye mwenyekiti wa kamati ya kampeni katika jimbo hilo na anasaidiwa na meneja wa kampeni, Patrick Ole Sosopi, wote kutoka jamii ya Kimasai.

Kwa upande wa CCM, Meneja wa Kalanga, William Ole Nasha, ambaye pia ana ushawishi mkubwa kwa jamii ya Kimasai.

Hivyo kwa muktadha huu, unaona ni jinsi gani kuna haja ya wanasiasa katika uchaguzi huu, kuwa makini na siasa zao ili wasiwagawe wananchi wa Monduli kwa misingi ya kiitikadi.

Kauli za kuwagawa wananchi, kuwajengea chuki baina yao na hata kuwashawishi kuvunja sheria siku ya uchaguzi na kabla ya uchaguzi zitakuwa na athari wakati huu na baada ya uchaguzi.

Athari hizi zitachangiwa pia na uelewa mdogo wa mambo ya kisiasa ya wananchi wengi wa Monduli, hasa vijana maarufu kama morani ambao wamekuwa wakiheshimu matamko ya viongozi wao, wakiambiwa piga mtu au fanya jambo lolote ni nadra sana kusita.

Kauli za kutokubali matokeo, kulinda kura kwa gharama yoyote, kauli kuwa lazima tushinde na mtake msitake tutashinda, nadhani zitakuwa na athari hata baada ya uchaguzi.

Ni muhimu wanasiasa wanaopanda majukwaani kutambua kuwa Monduli yenye amani, mshikamano na upendo ni bora zaidi kuliko vyama vyao vya kisiasa.

Lakini, pia wanasiasa katika uchaguzi huu, wanapaswa kujitenga na siasa za chuki, ubinafsi na matusi ambazo mwisho wake ni kugawa pia wananchi. Miaka ya nyuma Monduli ilikuwa ni moja ya wilaya tulivu kisiasa na hata kiuchumi na wananchi walikuwa na mshikamano katika shughuli mbalimbali za kijamii kuliko sasa.

Hivyo itoshe kuwataka wanasiasa ambao wanasimama majukwaani, kuomba kura kwa kutoa ahadi za maendeleo kwa wananchi, kujenga umoja na mshikamano badala ya kuhubiri chuki, mfarakano na siasa za kuwagawa wananchi.

Mussa Juma ni mwandishi wa mwananchi mkoani Arusha. Anapatikana kupitia 0754296503.

Chanzo: mwananchi.co.tz