Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siasa za Mbeya zitakavyotikisa CCM, upinzani uchaguzi 2020

97876 Pic+mbeya Siasa za Mbeya zitakavyotikisa CCM, upinzani uchaguzi 2020

Wed, 4 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wiki moja iliyopita madiwani 11 wa Chadema akiwamo aliyekuwa meya wa jiji hilo, Mchungaji David Mwashilindi na naibu wake, Fanuel Kyanula walitangaza kuhamia CCM, huku wakieleza wamekimbia ugomvi wa kila siku katika chama chao ambao unafanya mipango ya maendeleo kufeli.

Kuhama kwa wanasiasa hao si jambo geni, kwani katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa wanasiasa wengi wakiondoka katika vyama walivyokuwapo awali na kujiunga na vyama vingine.

Baada ya kuhama kwa madiwani hao alisikika Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akieleza kumtumia salamu mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu kwamba alimwahidi kuwasha moto, sasa kazi imeanza.

Hata hivyo, Sugu aliyeongoza jimbo hilo kwa vipindi viwili mfululizo alisema kitendo cha madiwani hao 11 kutimkia CCM hakiwezi kubadili mapenzi ya wananchi wa Mbeya kwa Chadema na kutaamba kuwa naye atagombea tena ubunge katika uchaguzi mwaka huu na ana uhakika ataibuka mshindi.

Kutokana na hali hiyo ni dhahiri kwamba katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu kutakuwa na ushindani mkubwa kati ya vyama hivyo.

Sasa kila chama kinajipanga kushika hatamu, Chadema kinaapa kulinda jimbo na kata zake na CCM wakiapa kunyakua jimbo hilo na maeneo ambayo waliyoyapoteza katika uchaguzi mkuu 2015.

Pia Soma

Advertisement
Itakumbukwa mwaka 2015, vyama vya upinzani vilijizolea nafasi nyingi za ubunge na udiwani katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa.

Baada ya madiwani hao 11 kutimkia CCM, sasa Chadema imebakiwa ni madiwani 19 pamoja na wa viti maalumu, huku CCM wakiwa na madiwani 17 pamoja na viti maalumu.

CCM wanafurahia kupokea madiwani hao wakiamini nguvu ya Chadema Mbeya mjini imekwisha na itakuwa mteremko kwao kushinda viti vingi vya udiwani na ubunge.

Hata hivyo, Chadema wanasema kitendo cha madiwani hao 11 kutimkia CCM hakiwezi kuwatetemesha na zaidi wanashukuru kuondoka kwao kwani walijijua wangedondoshwa katika uchaguzi ndani ya chama kwenye kura za maoni.

Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, John Mwambigija maarufu Mzee wa Upako anasema chama hicho bado kina nguvu kubwa tofauti na CCM inavyodhani.

Mwambigija anasema wameibana CCM Mbeya mjini na kuwa kuchukua madiwani hao hakuwezi kuwafanya washinde.

“Msiwazunguke wana Mbeya na dunia nzima kana kwamba hapa kuna ubovu, angalia madiwani hawa wamehama kutoka Chadema kwenda CCM mkadhani hiyo ndiyo tiketi ya ushindi.

“Sisi tunasema tuko imara kuliko jana na tangu lilipotokea jambo hili tumekaa na kutuimarisha kuwa wamoja zaidi na hakika tumesema tunarudisha nguvu ya mwaka 2010. Tuna mashine ambazo tulizitumia kupambana wakati ule tukawavuna hawa waliotoka,” anasema.

“CCM wamewachukua wapigiwa kura, lakini wapiga kura tunao sisi na tutakwenda kuwaeleza wananchi wetu na Mbeya ni waelewa wanaojitambua hawatababaika na hili jambo.”

Mwenyekiti wa CCM Mbeya mjini, Amphrey Msomba anasema CCM inapaswa kujipanga vilivyo ili kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.

Anaitaja mikakati ambayo CCM inapaswa kuisimamia na kuitekeleza Mbeya Mjini ili kujihakikishia ushindi kuwa ni lazima kuwepo uwiano sawa wananchama wa CCM na idadi ya wapiga kura, hivyo aliwataka viongozi kuanzia ngazi ya matawi kuhakikisha wanaingiza wanachama wengi wapya ndani ya chama hicho.

Mambo mengine ya kukiwezesha chama hicho kushinda ni kuongeza uhusiano mzuri miongoni mwa viongozi wa CCM na jumuiya zake, viongozi wa CCM taasisi binafsi, Serikali na viongozi wa CCM na wanachama.

Anasema mambo mengine ya kuzingatia ni kuongeza mshikamano miongoni mwa wana CCM na kutotanguliza masilahi binafsi, kutobagua watu kwa namna yoyote ile iwe kwa dini, ukanda, ukabila kwani kufanya hivyo kutakigawa chama na kujikuta wanapoteza ushindi.

Jimbo la Mbeya Mjini ambalo ni kati ya majimbo sita ya uchaguzi yaliyopo Mbeya, ndio jimbo pekee linaloongozwa na mbunge wa upinzani kwa vipindi viwili mfululizo na halmashauri yake kwa kipindi kimoja.

Majimbo mengine katika mkoa huo ni Kyela, Rungwe, Busokelo, Mbeya Vijijini, Mbarali na Chunya ambayo wabunge wake wanatokana na CCM.

Hata hivyo, CCM inalitolea macho jimbo hilo na viongozi wamekuwa wakikosa usingizi na wameapa kupambana ili kuliweka chini ya himaya yake.

Lakini Chadema nao wapo kwenye mikakati mizito ya kuhakikisha wanaandika historia ya kuliongoza jimbo hilo kwa vipindi vitatu mfululizo ikiwa ni pamoja na kunyakua kata nyingi na meya wa jiji hilo atoke Chadema.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CCM ilijikuta ikipokwa halmashauri na kwenda Chadema baada ya kupoteza kata 26 kati ya 36 na kujikuta ikiambulia kata 10. Ilianza kuwavuna taratibu baada ya madiwani wanne kufukuzwa Chadema kisha kujiunga na CCM na kushinda katika uchaguzi mdogo wa Novemba mwaka 2018.

Katika kuhakikisha CCM au Chadema inashinda hususani kwenye ubunge, vyama hivyo vinahitaji kusimamisha wagombea watakaouzika kwa wananchi, wenye ushawishi na uwezo wa kupambana kisiasa.

Chadema kete yao kubwa iliyopo ni kumrudisha Sugu kupeperusha bendera ya chama hicho, tayari mbunge huyo amewahakikisha wananchi kwamba atagombea tena uchaguzi ujao huku akijipa matumaini atashinda iwe kwa tume ya uchaguzi iliyopo au la.

“Ninagombea na tunaenda kushinda, tunashinda kuliko mwaka 2015 na tunashinda halmashauri na kata nyingi kuliko mwaka 2015, tulishinda kata 26, safari hii tunashinda zaidi ya 34 na tunawaachia kata mbili kwa faida ya demokrasia.

“Na hii iwe kwa tume huru au la. Na hili lazima tuelewane kwani mimi Mbeya sijawahi kupewa ushindi kwenye ‘Silver Plate’ (sahani ya fedha). Sisi tunapiga mtiti wa kufa mtu, tunapiga kura, tunalinda kura hadi mshindi atangazwe,” alisema.

Alisema anafahamu mazingira ya kisiasa yalivyobadilika kwa sasa, lakini hilo halimpi shida kwani uchaguzi huo utakuwa ni nchi nzima hivyo kila mtu atakomaa na eneo lake.

Wakati Sugu akieleza hayo, ndani ya CCM wapo makada wengi wamejimwaga mtaani ndani ya jiji hilo huku mienendo yao ikiwa ni kulinyemelea jimbo hilo na miongoni mwao ni Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

Dk Tulia anaonekana kufanya mikakati mbalimbali ikiwamo kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na kusaidia jamii kwenye sekta ya elimu, afya, kuandaa mashindano ya riadha inayojulikana ‘Mbeya Tulia Marathon’ kila mwaka.

Ingawa Dk Tilia ndiye anayeonekana katika harakati za kutaka jimbo hilo, lakini pia wapo wanaCCM wengine wana nia nia hiyo lakini kwa sasa wanabanwa kufanya hivyo kwa kuwa muda wa kampeni haujafika.

Julai 14 mwaka jana wakati anazungumza waandishi wa habari nyumbani kwake Uzunguni jijini Mbeya, Dk Tulia aliweka wazi nia yake ya kuwania kiti cha ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu lakini hakuweka wazi jimbo atakalogombea.

Swali la kujiuliza ni iwapio Dk Tulia na wanaCCM wengine wataweza kuwa wamoja na kumng’oa Sugu katika jimbo hilo katika uchaguzi wa Oktoba?

Mjadala wa suala hilo katika mitandao ya kijamii wachangiaji walieleza sababu za kuona kiongozi husika anafaa na anaweza kuibuka mshindi katika jimbo hilo.

Mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Swet-R anasema kuwa ukifanyika uchaguzi huru na haki Sugu atashinda asubuhi kweupe kwa kuwa watu wengi bado wana mapenzi naye hasa vijana.

Hata hivyo, mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Sanyambila alipingana na hoja hiyo akisema umefika wakati wana Mbeya kubadilisha mgombea kutoka chama hizo na kwa hao waliotajwa, Dk Tulia anaweza kufaa kwa maendeleo ya wana Mbeya.

“Huyo mtu usipime ni mashine nyingine serikalini kwa sisi tuliobahatika kufanya naye kazi. Tujivunie tutampata mtu mwingine mwenye maono makubwa kwa Mkoa wa Mbeya baada ya ProfesaMwandosya.

“Sugu tumpongeze kwa aliyoyafanya hadi alipofikia sasa tumepata jembe lingine Dk Tulia Ackson,” alisema na kuongeza:

“Adui mkubwa wa CCM Mbeya ni CCM wenyewe na wala siyo Sugu. Ubinafsi, ukabila na unafiki wa viongozi hao utakaomfanya Sugu aendelee kuwa rais wa jimbo hilo kwani wazee walisema ‘vita ya panzi ni sherehe kwa kunguru’”.

Chanzo: mwananchi.co.tz