Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Si Makonda, Chalamila pekee, wengi wanahitaji kunolewa

75880 Pic+makonda

Mon, 16 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Naomba nianze makala yangu haya kwa kurejea kwa kifupi maisha ya Dk Salim Ahmed Salim aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Tanzania na baadaye katibu mkuu wa OAU.

Dk Salim ambaye aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri akiwa ni kijana wa miaka 22 tu, alifanya kazi yake vizuri na hakuacha kujifunza kutokana na makosa aliyokuwa anayafanya. Lakini jambo la kutambua ni kuwa mbali na yeye kuwa kijana mdogo pia mamlaka ya uteuzi ilitambua kuwa bado ni kijana mdogo aliyehitaji kuvumiliwa na kuelekezwa mambo ya kujisahihisha.

Dk Salim aliwahi kusimulia miongoni mwa matukio anayomkumbuka akiwa Balozi wa Tanzania nchini Misri likiwamo la kuchelewa kufika uwanjani siku ya kuadhimisha sherehe ya Mapinduzi ya Misri. Alifika uwanjani wakati viongozi wote wa Afrika walishawasili na yeye kama Balozi alipaswa awe amefika mapema sana.

Tukio la pili analokumbuka ni lile la kubaki hotelini wakati Rais Nyerere amefanya ziara ya kitaifa nchini Misri. Alikuwa hajui lolote kuhusu masuala ya diplomasia wala protokali. Baadaye Nyerere akauliza aliko Balozi wa Tanzania maana hakumwona kwenye msafara wake.

Bahati mbaya Dk Salim alikuwa kapumzika hotelini na hakujua kama alipaswa kuwa kwenye msafara wa Rais wa Tanzania aliyekuwa ziarani Misri.

Kama ilivyotokea kwa Dk Salim, kipindi cha awamu ya tano cha urais wa Dk John Magufuli tumeshuhudia vijana wengi wakiteuliwa kwa nyadhifa mbalimbali nzito katika ngazi za wilaya, mikoa na hata wizara.

Pia Soma

Advertisement
Hata hivyo, changamoto iliyopo kwa sasa katika nchi yetu si suala la vijana kuwa viongozi, bali maandalizi na malezi ya kuwaandaa vijana wetu kuwa viongozi wazuri.

Kuna tofauti kubwa kati ya mkuu wa wilaya wa sasa wa Kinondoni ambaye amepitia ngazi tofauti za malezi ya uongozi ndani ya chama tawala na viongozi wengine ambao hawakubahatika kulelewa kiuongozi ndani ya chama tawala.

Kutokana na muktadha huo napenda katika makala yangu kujadili mwito wa Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally wa kuwataka wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya, Paul Makonda na Albert Chalamila kupewa nafasi ya kwanza ya mafunzo ya uongozi kwenye chuo cha mafunzo ya siasa na uongozi cha CCM.

Kwanini vijana wanahitaji mafunzo ya uongozi?

Kwa wale tunaomfahamu Dk Bashiru akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akifundisha siasa na utawala, tunamwelewa vizuri anapoumia kuona vijana hawa wawili wakitoa kauli za ajabu majukwaani zinazoweza kubomoa taifa.

Tunakumbuka jinsi Dk Bashiru alipoumia na kulazimika kuomba radhi kwa niaba ya Makonda kuhusu kauli yake aliyoitoa pale Karimjee kuhusiana na Reginald Mengi na wachaga. Hata hivyo Makonda hakuonyesha kujutia kauli yake ile.

Hata hivyo, naweza kusema kwa upande mwingine Dk Bashiru ameonyesha upendeleo katika kauli yake, kwani wapo viongozi vijana wengi sana waliolewa madaraka waliyopewa.

Kuna baadhi ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, manispaa na majiji wamekuwa wakilaumiwa kwa vitendo vya kuwanyanyasa wananchi.

Si hao tu, pia baadhi ya viongozi wa chama tawala kwenye kata, wilaya, na hata mikoa wamekuwa na tabia ya kuwanyanyasa na kuwasumbua watumishi wa umma na kuwafanya wafanye kazi kwa woga na wasiwasi.

Wengi tunalikumbuka lile tukio la katibu mwenezi wa kule Arusha aliyemlazimisha mkurugenzi wa jiji la Arusha kumwondoa kwenye cheo chake mganga mfawidhi wa kituo cha afya ambaye alienda kazini siku ya Ijumaa Kuu na kufanya kazi hadi jioni na baada alipoondoka viongozi wa chama tawala wakafika na kuanzisha zogo kwa kumtuhumu ana lugha chafu na kukosa adabu kwa viongozi wa chama.

Tunakumbuka kuwa Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru aliingilia kati na mganga mfawidhi yule kurejeshwa kazini. Ilikuwa ni bahati kuwa jambo lile lilisambaa kupitia mitandao ya kijamii. Wapo watumishi wa umma wengi ambao wamejikuta wanakuwa waathirika wa ubabe wa viongozi waliopewa dhamana ya kuwasaidia.

Kwanini haya yanatokea?

Rais John Magufuli ameonyesha imani kubwa kwa vijana na amewateua wengi katika nafasi mbalimbali nyeti. Ni jambo jema kufanya hivyo kwa kuwa tusipokuwa na viongozi vijana leo basi tutashindwa kuwaandaa vijana kuliongoza taifa huko mbeleni.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi hawa vijana wametokana na Chama tawala na wengine ni wale waliowahi kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama na za ubunge. Rais alionekana kuwa na imani nao nao kwa kudhani watakuwa wanaendana na kasi yake, lakini wao wamekuwa wakivuka mipaka ya utu katika kutekeleza majukumu yao.

Kumekuwapo na malalamiko kuwa baadhi yao wamekuwa wafuasi kindakindaki wa chama tawala na hivyo kufanya kila jambo kukitetea chama hata kwa masuala yanayoweza kuharibu ustawi na umoja wa kitaifa.

Na wengine kwenda mbali zaidi kwa kutoa kauli zinazoonyesha wanataka kuonyesha wao wanampenda sana Rais kuliko wengine.

Wengi tutaikumbuka kauli mojawapo ya mkuu wa mkoa wa Mbeya kuwa anatamani Rais aanzishe Chama Tawala cha Magufuli, yaani kwa Kiingereza ni Magufuli Ruling Party (MRP).

Maonyo ambayo Dk Bashiru amekuwa akiyatoa yamechelewa lakini aheri uchelewe kuliko kutofika kabisa. Kwa sababu ya siasa tulishafikia hatua viongozi wetu wa serikali waliotokana na chama tawala wanaona kwao bora kufia chama kuliko kulifia taifa. Kwao wanaona taifa watu wote bali ni watu wanaokipenda chama tawala pekee.

Tumefikia hatua ambayo hatuongelei tena maslahi mapana ya taifa pasipokuangalia siasa zetu bali baadhi ya viongozi wetu ambao kimsingi ni watumishi wa umma wamekuwa wakitubagua kwa misingi ya vyama.

Mafunzo ya uongozi yatolewe Mwaka 2010 CCM ilipoteza kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu ukilinganisha na mwaka 2005. Walifanya uchunguzi na pia waliambiwa kuwa kikulacho ki nguoni mwake. Ilikuja kubainika kuwa wananchi wengi walikuwa na chuki nayo kwa sababu viongozi wake walikuwa wabinafsi na walikuwa sababu ya wananchi kupata mateso mengi.

Mwaka 2015 Dk Magufuli alizunguka nchi nzima kutoa ujumbe wa matumaini kuwa CCM inataka kurejea kwenye misingi yake ili iwe chama cha ukombozi wa wanyonge.

Na wengi waliposikia uteuzi wa Dk Bashiru waliamini kuwa Dk Magufuli amedhamiria kukirejesha chama kwenye misingi yake.

Lakini imekuwa bahati mbaya sana baadhi ya viongozi walioteuliwa na Rais kumsaidia kwenye majukumu yake wamelewa madaraka.

Wamekuwa wenye kiburi na majivuno mno kiasi kwamba wamezidi kurejesha hasira za wananchi dhidi ya chama tawala kama ilivyokuwa huko nyuma na matokeo yake mvuto wa Rais unapotea kwa sababu ya watendaji wake.

Ni jambo sahihi sasa kufikiria kutoa mafunzo ya uongozi kwa viongozi vijana wengi ili watambue kuwa uongozi ni dhamana. Wajifunze mbinu bora za kuwasiliana na wananchi na wale walio chini yao.

Wajifunze kuwa wao wamebeba dhamana ya kuendeleza taifa hili ili lisife wala kupotea na kuwa madaraka siyo kitu cha kudumu na kila binadamu anastahili utu na heshima.

Wasitumie madaraka yao kuwanyanyasa walio chini yao bali watumie busara kutatua changamoto zilizo mbele yao.

Mwandishi wa makala anapatikana kwa 0787525396 kwa maoni na mawazo.

Chanzo: mwananchi.co.tz