Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shirika lahimiza Watanzania kupiga kura

Aa745f63cc3250cf66b7139339e5e1cf.png Shirika lahimiza Watanzania kupiga kura

Tue, 1 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

S HIRIKA lisilo la Kiserikali (AFNET) limewahimiza Watanzania wenye vitambulisho vya kupiga kura, kujitokeza kupiga kura kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo kwa maslahi ya taifa.

Aidha, limewataka wananchi kutunza na kutumia vizuri haki yao ya kupiga kura kwa kutokubali kudanganyika au kurubuniwa kwa kununuliwa chakula, vinywaji, vitenge, kupewa fedha, khanga au rushwa yoyote ili kuwachagua viongozi wasio na sifa kwa kuwa hali hiyo itawagharimu kwa kuwapa viongozi wasiojali maslahi yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa AFNET, Sara Mwaga, alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kawawa katika Kata ya Msanga, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Walikuwa washiriki maombi maalumu yaliyoandaliwa na Kanisa la Kipentekoste la Sayuni Tanzania kijijini hapo kuliombea Taifa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu kuchagua rais, wabunge na madiwani.

Sara aliwahimiza wenye vitambulisho vya kupiga kura kutopuuza kutumia haki yao kuchagua viongozi kwa kuzembea kwenda katika vituo vyao kupiga kura kwani kutokupiga kura ni sawa na kuruhusu kupatikana kwa viongozi wabovu na wasiotakiwa.

“Haipendezi mwananchi una kitambulisho cha mpigakura halafu ukakaa nacho nyumbani siku ya upigaji kura; mjitokeze kwa wingi ili mtumie haki yenu ya kisingi ya kuwachagua viongozi mnaowataka wenyewe na msisubiri kuchaguliwa na wengine,” alisema Sara.

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Sayuni, Jonas Kabia alisema, wakati taifa likijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu halitegemei kupata viongozi watakaowagawa Watanzania kwa namna yoyote, bali kupata viongozi watakaochochea maendeleo, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Alisema maombi hayo maalumu yalilenga kumwomba Mungu awawezeshe viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kutekeleza ahadi watakazotoa wakati wa kampeni.

Kwa mujibu wa Mchungaji Kabia, wagombea wanatakiwa kunadi sera za vyama na kuepuka lugha za matusi na badala yake, waeleze sera zao na namna watakavyoshirikiana na umma kutatua changamoto za jamii.

Chanzo: habarileo.co.tz