Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shibuda amshukia Msajili kuwabana zaidi wapinzani

Shibudapic Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya siasa, John Shibuda

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya siasa, John Shibuda amesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inafanya kazi ya upekuzi wa vyama kujua vinafanya nini ili wajue ni namna gani ya kuvichanganya.

Shibuda alieleza hayo jana, alipozungumza kwenye kikao cha kamati kuu ya NCCR Mageuzi kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili changamoto kuelekea miaka 60 ya Uhuru.

Alisema jicho pevu la duru za siasa ni kwamba vyama vya siasa vya pinzani vijipange na vitambue samaki uwezo wake huanzia kichwani na kuambukiza sehemu zote za mwili.

“Vyama vya siasa vitambue kwamba kichwa cha wadau wa siasa ni Baraza la Vyama vya Siasa na siyo sauti ya rufaa kwa maumivu ya wadau wa vyama, Baraza la vyama vya siasa si baragumu kwa vilio vya huzuni,” alisema Shibuda.

Alisema Tanzania Baraza la Vyama vya Siasa ni itifaki ya kuduwaza taswira ya kimatafa kuhusu kuwepo chombo cha kuinua na kukweza demokrasia kupitia vyama vingi.

“Msajili ni chama gani amekitengenezea maarifa na weledi kitaaluma, ili kiweze kuwa na nguvu za kisiasa na werevu wa kuweza kushindana na CCM, kila siku ofisi ya msajili inafanya kazi ya upekuzi kujua vyama hivi vinaendeleaje, wanajipanga vipi ili tuweze kuwachanganya.

“Hawa ni Watanzania, mimi sijawahi kuona Mufti anazuia watu kwenda madrasa ili waje kuwa masheikh, ambao ni werevu, au sijawahi kuona baba askofu hataki vijana waende seminari wakihofia kuwa watakuja kuwa mapadri watampindua uaskofu,” alisema.

Shibuda, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha Ada Tadea alisema hali ya kisiasa ipo katika kupagawisha kwa kuwa ushwari wa juu ya mto ni utulivu wa msukumo wa maji wa chini ya mto.

“Hali ya kisiasa Tanzania ipo kama bahari, kuna nyakati huchafuka kwa mawimbi makubwa ya kifani na dhoruba na kusababisha vyombo kupoteza mwelekeo na kwenda mrama na mabaharia huwa hawapotezi mwelekeo, hivyo vyama vyote vilivyoko baharini nashauri msiruhusu kukata tamaa,” alisema.

Aidha, Shibuda alisisitiza vyama vyote vya upinzani kufuata somo la ustahilivu na subira, huku wakitambua kuwa Taifa halina fikra sahihi ya kunufaisha matamanio ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere na hayati Karume walioacha usia kwamba tuishi kwa haki na usawa pamoja na maridhiano.

Alipotafutwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuzungumzia kauli hiyo ya Shibuda alisema kilichozungumzwa hajakisikia kwa kuwa hakuwepo kwenye mkutano huo, hivyo hawezi kuzungumza chochote hadi atakapopata taarifa ya mkutano huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru, chama hicho kimeandaa kongamano litakaloshirikisha wadau mbalimbali wa demokrasia, ili kutathmini na kujadili changamoto zinazolikumba Taifa, yakiwamo malengo ya dunia.

Chanzo: mwananchidigital