Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shaka azindua kitabu cha Upekee wa Rais Samia

43e70e039f5c0c4fd5c701a5a4c06a42 Shaka azindua kitabu cha Upekee wa Rais Samia

Mon, 14 Mar 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ametaka Watanzania kuendeleza uzalendo wa kutangaza mazuri yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani.

Pia amewataka washiriki kikamilifu katika sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka huu, kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na wananchi kwa ujumla.

Shaka alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachoitwa Upekee wa Rais Samia, kilichoandikwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Kata ya Chamanzi, Nasri Mkalipa.

Alisema Rais Samia ameleta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali nchini, hivyo zinatakiwa kusemewa vizuri.

“Haya yaliyofanywa ndani ya mwaka mmoja ni majaribio kwa kuwa atazidi kufanya mengi zaidi, ambayo yataweka historia katika Taifa letu," alisema.

Alisema Rais Samia ameleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo madini, uvuvi, kilimo, ujenzi, makundi ya bodaboda, wamachinga, wajasiriamali yote hayo ni jitihada za kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM.

"Rais Samia ameimarisha mzunguko wa fedha kote nchini, ukilinganisha hali ya sasa na siku za nyuma mambo ni tofauti kabisa, hivyo tuna kila sababu ya kumuunga mkono kwa kutangaza mazuri yote yanayofanywa, ambayo yana tija katika ukuaji wa uchumi," amesisitiza.

Amesema mzunguko huo umechagizwa na jitihada za Rais Samia za kuweka fedha anazozipata za ujenzi wa miradi mbalimbali zikiwemo za mikopo, kuhakikisha zinaingia katika mzunguko.

Alisema Rais Samia amefanya vizuri katika kuimarishaji uhusiano wa kimataifa, amejipambanua katika diplomasia ya uchumi kwa kutembelea mataifa mbalimbali, hali iliyochochea ukuaji wa uchumi.

Katibu hiyo alimtaka kila Mtanzania kutumia ujuzi wake kwa kutangaza mema yaliyofanyika kwa njia mbalimbali, ikiwemo uandishi wa kitabu kama alivyofanya Mkalipa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, aliwataka Watanzania kuendelea kumuombea Rais Samia ili aendelee kuleta maendeleo zaidi.

Naye Mkalipa alimpongeza Shaka kwa kumuunga mkono katika jitihada zake hizo za kuandaa kitabu hicho kinachoeleza sifa za Rais Samia.

Chanzo: www.habarileo.co.tz