Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shaka awapiga ‘kijembe’ wanaopinga Rais Samia kusifiwa

Shakaakakakakaka Shaka awapiga ‘kijembe’ wanaopinga Rais Samia kusifiwa

Thu, 24 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka amesema kwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan imewatoa nyoka pangoni kuja kuota jua la maendeleo.

Amesema kipaji cha uongozi cha Rais Samia ni chachu ya maendeleo endelevu huku ubunifu wake ukileta ari mpya ya kusukuma maendeleo ya nchi.

Shaka amesema hayo jana Jumatano, Novemba 23, 2022 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Babati mjini, Mkoa wa Manyara katika sehemu za shughuli za Rais Samia akikamilisha siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara. Kwa sasa Rais Samia yupo ziarani Mkoa wa Arusha.

"Mheshimiwa Rais na Watanzania msishangae kwa mambo makubwa yanayofanyika nyoka aliyoko pangoni atakuja juu, atakuja juu kutafuta jua ili akauke na kupata matumaini.

“Mambo makubwa anayoyafanya Rais Samia Suluhu Hassan ameua ndoto, ameua matumaini ya watu...ndio imekwisha hiyo tena, tuombe uhai na uzima, tunaye kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu umoja wetu na mshikamano wetu habari 2030 penye uhai," amesema Shaka

Shaka amesema Rais Samia ni kioo kinachoakisi utu na thamani ya Watanzania huku kipaji chake cha siasa na uongozi imekuwa chachu ya maendeleo.

Amesema ubunifu wa Rais Samia umeleta ari mpya ya kusukuma maendeleo katka nchi hivyo Watanzania waendelee kumuunga mkono.

"Ndugu zangu mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Rais Samia umeleta mageuzi makubwa katika nchi hii. Hatukuwa na mazoea kukaa kwenye mikutano hii...jamani nini mnachokitaka," amesema.

Shaka amesema chama kinaridhishwa na kazi nzuri inayotekelezwa na Rais Samia katika kuwatumikia wananchi.

"Kwa chama ni faraja na matumaini makubwa kwamba kumbe Rais wetu mambo yake si mabaya, mambo yake ni mazuri sana," amesema

Shaka amesisitiza kuheshimiwa na kuenziwa kwa utamaduni wa kupongeza pale kiongozi anapofanya vizuri na kukosoa kwa heshima na staha pale mambo anapokuwa hayakwenda sawa.

"Tukajikumbusha utamaduni wa waafrika, pia tukajikumbusha utamaduni wa Watanzania tangu enzi za uhai wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere utamaduni wetu Watanzania ukifanya vizuri unapongezwa, unapewa shukurani na unatiwa moyo ili ufanye vizuri zaidi.

“Lakini utamaduni wetu pale ambapo hufanyi vizuri au mambo hayaendi vizuri Watanzania tumekuwa na utaratibu mzuri wa kukosoana kwa staha na heshima," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live