Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shaka aagiza ukaguzi mradi wa maji uliogharimu Tsh. Milioni 560

Shaka Hamdu Shaka Shaka aagiza ukaguzi mradi wa Tsh. Milioni 560

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza serikali wilayani Bukoba ichunguze na kuwachukulia hatua waliohusika kuisababishia serikali hasara ya shilingi milioni 590 katika mradi wa maji Katale.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alitoa agizo hilo alipokuwa kwenye ziara ya uimarishaji wa chama na ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020-2025.

Mradi huo ulikamilika na kukabidhiwa lakini hautoi maji.

Shaka alisema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuitekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinafikiwa na huduma ya maji safi na salama.

Aliwataka wanaohusika na utafiti wa vyanzo vya maji, wanaofanya makadirio ya ujenzi na wakandarasi ujenzi wa miradi ya maji wawe waadilifu, wazalendo na wafanye kazi kwa weledi ili kuepuka hasara.

"Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ibara ya 100 imetoa maelekezo kwa serikali ya kuwafikishia wananchi wengi zaidi huduma ya maji safi na salama kwa kuongeza utafiti wa kubaini vyanzo stahiki vya maji, kufanya makadirio ya ujenzi pamoja na kuikamilisha miradi ili kutoa huduma…”

Shaka alisema miradi inayotumia fedha nyingi bila kutoa huduma inashusha heshima ya chama na kwamba CCM na Rais Samia hawapo tayari kuona hilo likitokea.

"Kukosekana kwa maji safi na salama ni kuongeza umaskini. Wananchi wanatumia muda mrefu kutafuta maji kuliko kushiriki shughuli zao za kiuchumi pamoja na kutumia fedha nyingi kujitibu maradhi yatokanayo na matumizi ya maji ambayo sio salama," alisema.

Shaka aliahidi kuwa CCM itatoa msukumo kwa Wizara ya Maji ipeleke shilingi milioni 50 kwa ajili ya kurejesha huduma ya maji Katale.

Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza alisema ni miaka miwili sasa wananchi wa Katale wanatembea umbali mrefu kufuata maji ambayo si salama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live