Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shaka: Watanzania zindukeni kujua malengo ya Rais Samia

6612085aadc3adba38d48b9e98526045.jpeg Shaka: Watanzania zindukeni kujua malengo ya Rais Samia

Wed, 1 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema iwapo kila Mtanzania atawajibika na kufanya kazi kama yalivyo malengo, mipango na mikakati ya Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania itapaa na kuwa nchi yenye uchumi unaojitegemea.

Kimesema uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita kuendeleza kaulimbiu ya ‘kazi iendelee’ ni kumtaka kila mtu anayeishi mjini na kijijini atambue wajibu wa kujituma, kufanya kazi, kuzalisha mali na kuitumikia nchi yake.

Hayo yalielezwa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alipokutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Wafanyabiashara hao, walifika ofisini hapo kwa ajili ya kujitambulisha baada ya uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya.

"Siku moja ikitokea Watanzania tukayaelewa malengo ya kisera na kimkakati ya Serikali ya Awamu ya Sita, yanayotaka watu kujituma, ndipo tutakapoondokana na kadhia ya umasikini. Binadamu anapoamini kufanya kazi ni kama adhabu au utumwa huo ni mtazamo hasi usiofaa kufuatwa," alisema Shaka.

Alifafanua kuwa, katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Samia ameakisi mambo yaliyokuwa yakitamaniwa na jamii yatokee, sauti ya Rais Samia imetoa mwangwi ili kuwazindua waliotaka kukata tamaa ambapo fikra, akili na mioyo ya Watanzania imepata ratiba mpya kwa kuzingatia mambo ya msingi yanayotamaniwa na kutoa uamuzi wa haki.

"Tulipopata uhuru na kufuzu Mapinduzi ya Zanzibar, kaulimbiu za marais na waasisi wa taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume, ilimtaka kila mtu afanye kazi. Ikaelezwa kazi ni kipimo na thamani ya utu wa mtu. Tafsiri ya uhuru ni kufanya kazi. Watu walishiriki kwa pamoja kufanya kazi za maendeleo, leo hii Rais Samia anaendeleza maono ya waasisi wetu hasa katika suala la uchumi wa kipato kwa Watanzania," alisisitiza.

Shaka alisema CCM inaridhishwa jinsi wananchi wanavyofanya shughuli zao za uzalishaji na kuipongeza Serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kuboresha huduma za kijamii na miundombinu ya kiuchumi ili kuharakisha maendeleo katika kukuza uchumi wa nchi kukiwa na amani na utulivu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho, viongozi wa jumuiya hiyo walisema kilichowapeleka hapo ni kuimarisha ushirikiano, kwa kuwa CCM ndicho Chama chenye ilani inayotekelezwa na serikali.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Martin Masawe alisema jumuiya hiyo inaamini katika uhusiano mzuri na serikali pamoja na CCM, ili kutengeneza misingi mizuri ya ushirikiano wa karibu utakaorahisisha kutatua changamoto mbalimbali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz