Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shaka: CCM haitakubali ubadhirifu

A074d494561e91628413e2326b12221f Shaka: CCM haitakubali ubadhirifu

Wed, 17 Aug 2022 Chanzo: Habari Leo

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakiko tayari kuona wala kusikia mtendaji wa ngazi yoyote wa serikali aliyebainika kufanya ubadhirifu akiendelea kulelewa kwa kutochukuliwa hatua za kinidhamu.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Shaka Hamdu Shaka alisema CCM haiwezi kuvumilia kuona wananchi wakiendelea kunyonywa wakati wanashiriki shughuli za maendeleo.

Shaka alitoa kauli hiyo jumanne mbele ya wananchi wa Kijiji cha Ibambo, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora baada ya kusimamisha msafara wake ili kutoa kilio chao cha fedha ambayo waliichanga kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika shule ya sekondari kijijini hapo.

Wananchi hao walidai kuwa walichanga Sh 995,000 wakampa Mtendaji waliyemtaja kwa jina moja la Mnyaga.

Shaka alisema haiwezekani wananchi wanachanga fedha kwa ajili ya maendeleo halafu kuna mtu anachukua hiyo fedha halafu linaonekana jambo la kawaida tu.

Aliagiza mtendaji afuatwe huko aliko na kisha alipe fedha aliyochukua na kwamba lazima vitendo hivyo vikome.

“Huyu mtu amekula hizo fedha za wananchi na baada ya kula hizo fedha ofisi ya Mkurugenzi ikamhamisha, ikampeleka kijiji kingine ili kusudi akaendeleze huo ubadhirifu. Haiwezekani,” alisema na kuongeza:

“Yaani ameharibu sehemu moja amechukuliwa akaharibu sehemu nyingine, akaumize wananchi wa chini kabisa, hiyo ni haki? Kama amekula fedha za wananchi mmejiridhisha na wananchi wenyewe wanalalamika, mnaondoa tatizo sehemu moja mnapeleka sehemu nyingine.

Shaka alisema si dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona wananchi wananyonywa na kuwekewa mazingira magumu ya kufanikisha miradi ya maendeleo.

“Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitamvumilia mbadhirifu yeyote awe kwenye kijiji, kitongoji, kata, wilaya, halmashauri, mkoa au awe taifani. Rais alishasema mkitaka kujua rangi yake halisia chezea fedha za umma.

“Kabla ya kuondoka kwenye huu Mkoa wa Tabora nisikie hatua zimechukuliwa na tunamfuatilia na mimi nimeanza kumfuatilia tangu nimetoka Dar es Salaam,” alisema Shaka.

Pia alisema wanafuatilia mifumo ya utoaji fedha za serikali ambayo inadaiwa kuwa chanzo cha kukwamisha miradi ya maendeleo.

Chanzo: Habari Leo