Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi kesi ya viongozi wa Chadema asema aliamrisha askari kupiga risasi hewani

52854 Pic+chadema

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Ofisa oparesheni mkoa wa kipolisi wa Kinondoni ambaye ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi( SSP), Gerald Ngichi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa yeye ndiye aliyeamuru askari polisi kupiga risasi hewani kutawanya waandamanaji waliokuwa katika makutano ya barabara ya Kawawa na Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Waandamanaji hao walikuwa wakitokea katika viwanja vya Buibui vilivyopo kata ya Mwananyamala kwenda katika ofisi za mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni.

SSP Ngichi  ameeleza hayo leo mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati akitoa ushahidi wake.

Ngichi ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ya kufanya mkusanyiko usio halali inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwamo  mwenyekiti wake , Freeman Mbowe.

Ngichi  alieleza alitoa amri hiyo baada ya amri tatu za kuwakataza waandamanaji  kufanya mkusanyiko huo kushindikana.

"Nililazimika kutumia njia ya mwisho ya kutumia silaha za moto kupigwa hewani kutoka na waandamanaji kutotii ilani tatu nilizozitoa katika umati huo wa waandamanaji kwa kutumia kingo'ra nikiwa katika gari la  polisi," alidai Ngichi.

Alidai kabla ya kutumia njia ya mwisho ya kuamuru askari wake wa vikosi vya doria kupiga risasi juu, aliamuru kikosi cha askari walikiwapo katika eneo hilo kupiga mabomu ya moshi kwa ajili ya kuwatawanya waandamanaji hao waliokuwa wanaongozwa na viongozi wa chama hicho.

Alidai wakati askari wake wakiendelea kurusha mabomu ya moshi kwa waandamanaji hao, hawakufanikiwa vizuri kutokana na moshi wa mabomu hayo kuelekea  upande walipo askari hao.

"Zoezi la  kupiga  mabomu waandamanaji hao lilikuwa  hafifu kutokana na moshi kuelekea  upande walipo askari badala ya kwenda kwa  waandamanaji kutokana na  upepo uliokuwapo eneo hilo hali iliyopelekea waandamanaji kutosambaratika" alidai Ngichi.

Alidai katika harakati za kurusha mabomu kwa waandamanaji hao,  askari polisi wawili ambao ni PC Fikiri na Koplo Rahim waliokuwapo eneo la tukio walijeruhiwa kwa mawe na kuanguka chini.

"Baada ya kuanguka chini askari hao niliamuru askari wengine watoe msaada kwa majeruhi hao kwa kuwaondoa katika eneo hilo na niliamuru kikosi cha mabomu kirudi  nyuma na kikosi cha risasi kisonge mbele ili kukabiliana na waandamanaji hao," alidai.

Alidai askari wenye silaha walisogea mbele na kupiga  risasi hewani ili kuwatawanya waandamanaji waliokiwa wanataka kuchukua silaha baada ya askari wake wawili kujeruhiwa na kuanguka chini.

"Risasi zilivyopigwa hewani kishindo kulikiwa  kikubwa hali iliyopelekea watu wengi kukimbia akiwamo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, sikujua  kama mheshimiwa Mbowe anajua kukimbia namna hiyo," alidai Ngichi ambaye aliajiriwa na Jeshi la  Polisi tangu mwaka 2000.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni  Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko;   Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu;  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe,  Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa 13, ambapo wote wanadaiwa kuwa Februari 1 na 16 mwaka jana Dar es Salaam waliku?a njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Endelea kufuatilia mitandao yetu, kesi hii bado inaendelea mahakamani.



Chanzo: mwananchi.co.tz