Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yawaita viongozi CHADEMA waliokimbia nchi

1b5d1a3797a9d30aa37aa75da3ad3a91 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni

Wed, 8 Jun 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali imewataka Watanzania waliokimbia nchi kwa sababu mbalimbali wakiwamo viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kurejea nchini na kutumia fursa zilizopo kiuchumi kwa kuwa Tanzania ipo salama.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni wakati wa kutoa majibu ya swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega (Chadema) baada ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuagiza wizara itoe majibu ya swali hilo.

Katika swali lake, Tendega alisema ameona Rais Samia Suluhu Hassan akifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani kwa maana ya kuleta maridhiano na mshikamano wa nchi.

“Je, Serikali haioni ni muda mwafaka sasa wa kueleza na kuwasihi wananchi Watanzania waliopo nje ya nchi ili waweze kurejea hapa nchini na kushiriki ujenzi wa nchi yetu?”

Kutokana na swali hilo, Dk Tulia alitoa muda kwa wizara hiyo kuja na majibu ya swali hilo ambalo ni la msingi na kuwa limekuwa likizungumzwa.

“Waheshimiwa wabunge swali la msingi linahusu upatikanaji wa vitambulisho vya taifa, lakini swali lililoulizwa hapa ni la msingi sana, sina uhakika una majibu hapo, labda nikupe muda,” alisema Tulia.

Baada ya kupitishwa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2022/23, Dk Tulia alitoa nafasi kwa Masauni ambaye alisisitiza kuwa nchi ipo salama na hakuna tishio lolote la usalama.

“Hakuna sababu yoyote kwa Mtanzania yeyote aliyepo popote pale, ikiwamo viongozi wa Chadema waliopo nje ya nchi kutokurejea nchini, ili tu siyo waweze kutumia fursa nyingi ambazo nimezieleza za maendeleo makubwa ya kiuchumi, kisiasa yaliyopo, bali kushiriki kikamilifu kutoa michango yao kwa maendeleo ya nchi zao kwenye nyanja zote kwani hapa ni nyumbani kwao,” alisema Masauni.

Alisema serikali itaendelea kuhakikisha hali ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi iliyopo nchini inaendelea kudumu kwa maslahi mapana ya Watanzania.

Alisema Rais Samia amefanya jitihada kubwa za kuimarisha mazingira ya kisiasa nchini ikiwamo kukutana na viongozi wa upinzani mara kadhaa.

“Tumeshuhudia viongozi hao wakipongeza na kumsifia Rais hadharani kwa jitihada hizo, lakini ameshakutana na viongozi wa vyama vya siasa mmoja mmoja kwa mfano amekutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Tundu Lisu ambaye ni Makamu Mwenyekiti,” alisema Masauni.

Alisema Rais pia amekutana na Mwenyekiti wa chama cha ACT- Wazalendo, Juma Duni na kushiriki kwenye hafla mbalimbali za kijamii na kibinafsi zinazohusiana na viongozi wa vyama vya siasa.

Alisema pia amekutana na viongozi wa vyama, umoja wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, Baraza la Vyama vya siasa na kuunda timu ya viongozi wa CCM na Chadema inayolenga kushirikiana na kukabiliana na vikwazo vya kisiasa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz