WABUNGE wa Bunge la Tanzania kutoka Mkoa wa Kigoma wameipongeza serikali kwa kutekeleza miradi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Walitoa pongezi hizo kwenye kikao Cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa Kigoma baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda alisema ameridhishwa na kazi iliyofanywa na serikali katika miradi ambayo imeleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na mkoa.
Mbunge wa Buyungu wilayani Kakonko, Deodatus Kamamba alisema miradi ya barabara, elimu na ujenzi wa masoko hasa soko la mpakani na Burundi kwenye Kijiji Cha Muhange yamekuwa chachu ya mapinduzi ya kiuchumi kwa wilaya hiyo na mkoa kwa jumla.
Hata hivyo Kamamba alisema bado upo usimamizi dhaifu unaofanywa na viongozi na wataalamu unaosababisha baadhi ya miradi kutekelezwa kinyume na maelekezo na ubadhirifu wa fedha.
Andengenye alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita mkoa ulipokea kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya wananchi ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
Alisema serikali imeona changamoto ya upungufu wa wahandisi kwenye halmashauri na kwa mwaka huu wa fedha halmashauri na TARURA zimeruhusiwa kuajiri wahandisi ili wasimamie utekelezaji wa miradi.