Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaja na mikakati kukabili athari za corona kiuchumi

101704 Serikali+pic Serikali yaja na mikakati kukabili athari za corona kiuchumi

Wed, 8 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema katika kukabiliana na madhara ya kiuchumi yanayotokana na ugonjwa wa corona nchini, Serikali imeunda kikosi kazi cha kufanya uchambuzi wa kina wa athari zake.

Akichangia kwenye mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Mpango alieleza kikosi kazi hicho kitaundwa na wajumbe watakaotokea Tanzania Bara na Zanzibar itatoa watu wake.

Mapema bungeni jana, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alishauri kuundwa kwa kikosi kazi cha Taifa kwa ajili ya kuangalia athari za uchumi zitakazotokana na ugonjwa huo na kusitisha baadhi ya mipango ili kukabiliana kwanza na janga hilo.

Baadaye Bunge lilipitisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2020/21 ya Sh312.8 bilioni kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge.

Katika mchango wa kufafanua baadhi ya hoja, Dk Mpango alieleza uchambuzi wa kamati hiyo unatakiwa kufanyika kwa umakini ili kupatikana msingi wa kuandaa programu ya kiuchumi ya kukabiliana na janga la corona.

Dk Mpango alisema Tanzania tayari imeshaanza kupata madhara kama zilivyo nchi nyingine na athari zimeanza kujionyesha kwenye uchumi.

Pia Soma

Advertisement
Alitoa vidokezo vya mikakati kadhaa imechukuliwa na kuandaliwa ikiwemo ugharamiaji wa mahitaji ya msingi ya vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa corona.

Vingine ni ujenzi na uboreshwaji wa miundombinu ya kutolea huduma ya afya ikiwemo vituo vya kutolea huduma na tiba za dharura.

Hata hivyo alisema lengo kubwa ni kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa hiyo serikali inafanya jitihada za upatikanaji wa vifaa kinga kama barakoa na pia kuboresha mazingira ya kazi ya wahudumu wa afya na madaktari.

Alisema Serikali pia inaendelea kushauriana na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB) kuhusu namna wananchi wanavyoweza kufaidika na programu za dharura za taasisi hizo katika kukabiliana na janga la corona.

Hatua nyingine alisema ni kupunguza mdororo wa hali ya kiuchumi hasa katika sekta ambazo zimeshaanza kuathirika.

Alizitaja hatua zilizoanza kuchukuliwa kuwa ni pamoja na kuhifadhi chakula cha kutosha nchini na hatua za kibajeti kama kupunguza matumizi na kuongeza nguvu katika kukabiliana na corona.

Alitaja hatua nyingine ni kukarabati miundombinu ya usafiri ili wananchi waweze kufikiwa hasa waliopo vijijini na wataongeza kasi ya kulipa madeni.

Alitaja hatua nyingine za kuchukua ni za kikodi na mapato ili kutoa haueni kwa sekta binafsi.

Hatua ya tatu ni kuilinda sekta ya fedha na lengo ni kuhakikisha mabenki yanaendelea kuwa na ukwasi wa kutosha, akiba ya fedha ya kigeni ya kutosha, kudhibiti ongezeko la mikopo chechefu hususani kutoa unafuu kwa mabenki ili yaweze kurekebisha ratiba za ulipaji mikopo.

“Hatua mojawapo ya kuhakikisha mambo yanakwenda sawa ni kusaidia mabenki kwenye suala la ulipaji wa mikopo,” aliongeza.

Waziri aliyekataa karantini

Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Konde (CUF) Khatib Said Haji aliiomba Serikali kumchukulia hatua Waziri wa Ardhi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Salama Aboud Talib aliyekataa kukaa kwenye karantini na kusababisha maambukizi kwa watu wawili wa familia yake na kuwa kuna daktari mwingine naye ameng’ang’ania hapo.

“...matokeo yake akatolewa kwa nguvu kuwekwa kwenye karantini baada ya kuona jambo hili limekuwa kubwa,” alisema.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihitimisha hotuba ya bajeti yake ofisi alikiri waziri huyo kuondolewa kwa nguvu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja wakati na kuhimiza watu kuheshimu karantini.

Chanzo: mwananchi.co.tz