Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali njiapanda rufaa ya kina Mbowe

Zitto Pic Mbowe Mbowe Serikali njiapanda rufaa ya kina Mbowe

Tue, 30 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hukumu ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) imeiacha Serikali njiapanda ikukuna kichwa juu ya nini cha kufanya baada ya rufaa yake kutupwa.

Serikali ilikata rufani kupinga hukumu ya EACJ iliyotolewa Machi 25, mwaka jana ikiitaka Serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, kwa kuwa inakiuka mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kufuatia hukumu hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Eliezer Feleshi alisema jana kuwa wameupokea uamuzi huo lakini ni mapema mno kueleza nini kinachofuata.

Alisema masuala ya hukumu hasa kwenye sheria yanahitaji uchambuzi ikiwemo kusoma, ndiyo kutafakari cha kufanya baadaye.

“Ni mapema mno kusema tutakachokifanya baada ya uamuzi huo, angalau zingekuwa zimepita wiki mbili au tatu. Ni kweli tunajua kuhusu uamuzi lakini kwa sasa siwezi kusema lolote ni mapema mno,” alisema Dk Feleshi.

Wakati Dk Feleshi akisema hayo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul aliiambia Mwananchi kuwa Serikali ina mpango wa kufanya marekebisho hiyo ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

“Ni kweli tunarekebisha lakini nitumie hivyo vifungu vilivyotajwa kwenye kesi ili nivione kisha nitakueleza kwa kina,” alisema Gekul ambaye baadaye hakupatina.

Rufaa hiyo ilikatwa dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe.

Wengine ni katika shauri hilo ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na aliyekuwa mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.

Wadau watia shaka

Wakati Serikali ikikuna kichwa, wadau mbalimbali wa sheria wameshuku utekelezwaji wa hukumu hiyo kutokana na EACJ kutokuwa na chombo cha kukazia hukumu, hivyo utekelezwaji kubaki ni hiari ya Serikali husika.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwanasheria mwandamizi Dk Rugelemeza Nshalla alisema baada ya uamuzi huo, Serikali bila kupepesa inapaswa kutekeleza.

Ingawa uamuzi wa utekelezwaji wa hilo ni hiari ya Serikali, alieleza ili kuonyesha heshima kwa utawala wa sheria na haki Serikali mara moja inapaswa itekeleze.

“Udhaifu wa EACJ ni kukosa chombo cha kukazia hukumu yake, hii imesababisha mara kadhaa Serikali isitekeleze uamuzi unaotolewa nayo, lakini kiungwana inapaswa kutekeleza,” alifafanua.

Kulingana na Dk Nshalla, kuchelea au kupuuza utekelezwaji wa maamuzi ya mahakama hiyo, kunaifanya Serikali ipoteze uaminifu wake ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Ipo mifano ya maamuzi ya mahakama hiyo dhidi ya Tanzania na hadi sasa hayakutekelezwa, alitaja kesi ya mgombea huru na mgombea binafsi.

“Kwa kufanya hivi ukienda nje kwenye ripoti za Umoja wa Afrika Mashariki (EAC) unaonekana mchafu kwenye siasa na kwamba wewe ni mkorofi, hata wanasiasa wanaposimama jukwaani kusema Serikali (ya Tanzania) imepuuza uamuzi fulani, inachafuka,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Revocatus Kabobe alisema hukumu hiyo itakuwa silaha muhimu ya wapinzani ingawa utekelezwaji wake unahitaji utashi wa kisiasa, hasa kutoka CCM.

“Hukumu hii ni silaha muhimu ya kutumiwa na wapinzani ili kupeleka ajenda zao kwenye majukwaa ya kisiasa. Kwa lugha nyingine inawapa wapinzani nguvu ya kushambulia washindani wao CCM.

“Pamoja na kuwa nchi imesaini mkataba wa kuwa mwanachama wa mahakama hiyo, bado Serikali zetu zina nguvu ya kuamua chochote linapokuja suala ya mahakama za nje kutoa maagizo mbalimbali,” alieleza Kabobe.

Suala la mahakama za Afrika Mashariki kutegemea uwezeshaji kutoka kwa nchi wanachama, linatajwa na Kabobe kuwa ndiyo chanzo cha kukosa meno dhidi ya mataifa hayo.

“Ni lini mahakama za Afrika na hata Afrika Mashariki ziliwahi kuwa na meno? Zinabanwa tu na nchi wanachama wake, maana hazina fedha ya kujiendesha zinategemea hisani za nchi wanachama.

“Kwa hiyo hata zenyewe wakati mwingine zinakutana na changamoto ya kumhukumu anayekulisha," alifafanua.

Kisiasa, alisema hukumu hiyo itawapaisha wapinzani wakizichanga vema karata zao kwenye majukwaa ya kisiasa hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, lakini kwa upande mwingine utekelezaji wake ni mgumu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live