Moshi. Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini amejiuzulu wadhifa wa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania kutokana na kutotambulishwa rasmi kwa uongozi wa Bunge tangu ateuliwa miaka miwili iliyopita.
Selasini ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa siasa za mageuzi nchini humo, amelithibitishia Mwananchi usiku huu wa leo Januari 13,2020 kuandika barua kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi Bungeni (KUB), Freeman Mbowe juu ya uamuzi huo.
"Hiyo barua inayosambaa social media (mitandao ya kijamii) ni ya kwangu na nimeshamkabidhi mwenyekiti (Mbowe) kupitia kwa sekretari wake na nakala nimemkabidhi mheshimiwa Spika Ndugai (Job). Tangu niteuliwe sijatambulishwa kwa uongozi wa Bunge," amesema Selasini.
Selasini amefafanua amekuwa akiulizwa mara kwa mara na Katibu wa Bunge juu ya barua ya kumtambulisha ili aweze kuhudhuria vikao vya kikanuni, lakini mwenyekiti hajawahi kuliandikia Bunge," amesisitiza Selasini.
Selasini aliteuliwa kukaimu wadhifa huo miaka miwili iliyopita, kufuatia aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Tundu Lissu kuwa katika matibabu nje ya nchi baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 nyumbani kwake Jijini Dodoma.
Tangu ashambuliwe kwa risasi, Lissu ambaye alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki, hakuweza kurejea nchini ambapo mwaka 2019, Bunge lilitangaza kuwa amepoteza sifa ya kuwa Mbunge kwa kushindwa kujaza taarifa za mali na madeni na Spika wa Bunge, Job Ndugai kutojua mahali alipo.
Barua ya Selasini kujiuzulu wadhifa huo ilianza kusambaa katika mitandao usiku wa leo Januari 13,2020 na kuibua hisia tofauti miongoni mwa wachangiaji kuwa pengine mambo hayako sawa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Jitihada za kumpata Mbowe zinaendelea kujua kwa nini hakumtambulisha kama anavyodai Selasini.
Jitihada za kumtafuta Mbowe kuzungumzia hatua hiyo ya Selasini hazikuweza kuzaa matunda, na gazeti hili linaendelea kumtafuta Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na Mbunge wa Hai kuzungumzia suala hilo.