Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sekretarieti ya CCM inavyopokelewa Dodoma

Ccm Ccm.png Sekretarieti ya CCM inavyopokelewa Dodoma

Fri, 12 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shamrashamra za mapokezi ya sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama cha CCM zinaendelea kwenye viwanja vya Makao Makuu ya chama hicho Jijini Dodoma.

Viongozi hao wa sekretarieti wanaopokelewa leo Ijumaa Aprili 12,2024 ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, John Mongella, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Amos Makalla, Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Mwegelo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Ally Hapi.

Viongozi hao waliteuliwa katika kikao kilichofanyika Aprili 4, 2024, kilichoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan na kuziba nafasi nne za wajumbe wa sekretarieti zilizokuwa zimeachwa wazi.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia alimteua aliyekuwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Pamoja na Makonda, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, Gilbert Kalima aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UVCCM, Fikii Lulandala aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro.

Pia Mongela alipokea kijiti cha Anamringi Macha ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Hata hivyo, katika uteuzi huo bado kuna nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) iliyoachwa wazi na Jokate.

Leo wana-CCM kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma tayari wamekusanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM maarufu kama ‘White House’ kwa ajili ya kuwapokea viongozi hao.

Miongoni mwa waliokusanyika wapo viongozi wa Jumuiya za CCM, madiwani na wanachama na wakereketwa wa chama hicho kutoka maeneo mbalimbali, wengi wamevaa sare za chama hicho wamepamba mapokezi hayo.

Kwa mujibu wa ratiba ya mapokezi hayo, shughuli hiyo itaongozwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa.

Aidha, wakati watu wakiendelea kuwasubiri vikundi mbalimbali vya burudani vilikuwa vikiendelea kutumbuiza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live