Dhana ambayo Hayati John Magufuli aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alianza nayo, kwamba yeyote anaweza kuwa kiongozi CCM, tena akatamba kupitia uvumi kuwa Bashiru alikuwa mwanachama wa Cuf, kwa sasa inaonekana kuchukua sura mbaya. Hivi sasa sekretarieti ya CCM inaundwa na wajumbe ambao hawajulikani. Watakiuzaje chama?
Hivi karibuni aliyekuwa Katibu Mkuu CCM, Daniel Chongolo, alijiuzulu wadhifa wake kwa kashfa ya mambo binafsi ya kijamii. Hata ungemrejesha Chongolo leo ofisini, bado humwoni kama alitosha kupimana ubavu na viongozi wa kariba yake waliopo upinzani.
Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika, kiongozi wa idara za chama kwa muda mrefu. Akawa Naibu Katibu Mkuu, mbunge vipindi viwili kabla ya kuwa Katibu Mkuu.
Chongolo, alikuwa msaidizi binafsi wa Nape, alipokuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, akawa mkuu wa wilaya, kisha katibu mkuu. Je, unaweza kuwalinganisha Mnyika na Chongolo?
Naibu Katibu Mkuu Bara, Anamringi Macha, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Hamid, Katibu wa Oganaizesheni, Issa Gavu, Katibu wa Uchumi na Fedha, Frank Haule, wana msuli wa kuiuza CCM au wao ndiyo wanaotegemea chama kijenge wasifu wao wa kisiasa?