Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sarakasi uchaguzi wa madiwani Tunduma, watano wa Chadema hawajachukua fomu

11464 Tunduma+pic TanzaniaWeb

Mon, 16 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Wakati kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani katika kata 77 zikianza leo, wagombea watano wa udiwani wa Chadema katika Halmashauri ya Tunduma mkoani Songwe hadi jana saa 10 jioni walikuwa hawajachukua fomu za kugombea.

Mbali na wagombea hao kutochukua fomu, pia mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka alikamatwa na polisi pamoja na baadhi ya wagombea hao.

Sarakasi hizo zinajiri ikiwa ni siku chache tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itangaze tarehe ya uchaguzi huo mdogo utakaofanyika Agosti 12.

Pia, juzi NEC ilitangaza mabadiliko ya uchaguzi na iliongeza kata mbili mpya na kubadili tarehe ya uteuzi wa wagombea katika kata nne. Mabadiliko hayo yalifanya kubaki na kata 77 badala ya 79 zilizotangazwa awali.

Akizungumzia kukamatwa kwa Mwakajoka, mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga alisema mbali na mbunge huyo, pia katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) mkoani Songwe, Ayub Sikagonamo alikamatwa.

Haonga alisema miongoni mwa waliokamatwa ni baadhi ya madiwani, wanachama wa Chadema na walinzi wa chama hicho maarufu kama red brigade.

Saa chache baada ya viongozi hao kukamatwa, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alikwenda makao makuu ya NEC jijini Dar es Salaam kuonana na mkurugenzi, Athuman Kihamia ili kupata ufumbuzi wa masuala hayo. Muda mfupi baada ya hatua hizo, Chadema waliitisha mkutano na wanahabari, lakini baadaye waliuahirisha.

Akizungumzia ukamatwaji wa mbunge na wagombea hao, Haonga alisema Mwakajoka na Sikagonamo walikwenda ofisi za Halmashauri ya Tunduma kwa ajili ya kuchukua fomu za wagombea wa udiwani wa kata tano, lakini walikuta zimezingirwa na polisi.

“Sasa kutokana na hali hiyo, Mwakajoka akiwa na Sikagonamo aliona akienda kwenye ofisi hizo ataonekana kama amekwenda kufanya fujo, hivyo akaamua kwenda kituoni kuonana na mkuu wa kituo hicho (OCD) ili ampe ulinzi wa askari,” alisema Haonga. “Lakini cha kushangaza alipofika pale akaambiwa kuwa jana usiku (juzi) alifanya kikao na wenzake kwa lengo la kufanya maandamano, hivyo akawekwa chini ya ulinzi. Basi wamewekwa ndani hadi muda huu (jioni).”

Alisema hadi jana jioni hakukuwa na amani wala utulivu katika mji humo kwa kuwa wafuasi wao walikuwa hawaelewi kinachoendelea.

“Tunajua hizi zote ni jitihada za kuhakikisha hatushiriki kwenye uchaguzi ili wagombea wa CCM waweze kupita bila kupingwa,” alisema.

Alisema mpaka jana jioni hakuna mgombea udiwani wa Chadema katika halmashauri hiyo aliyechukua fomu za kugombea kutokana na alichokiita kuwa mizengwe wanayowekewa.

Alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange alisema atalizungunzia baada ya kupata taarifa kamili kwa kuwa muda aliowasiliana na gazeti hili alikuwa nje ya ofisi.

“Nitalizungumzia nitakapopata taarifa, kwa sasa sina taarifa kamili na sipo ofisini,” alisema.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Tunduma, Boniface Mwakabanje ambaye pia ni mgombea Kata ya Majengo, alisema wagombea walioteuliwa na uongozi wa Chadema kugombea udiwani na kata zao kwenye mabano kuwa ni Alice Mkorongo (Mpemba), Osiah Kibwana (Karoleni), Hitler Haonga (Mwaka kati), Elia Lonje (Sogea) na Boniface Mwakabanje (Majengo).

Chanzo: mwananchi.co.tz