Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwasili mkoani Mara Ijumaa kwa ajili ya kushiriki sherehe za miaka 45 tangu kuzaliwa kwa chama hicho tawala.
Akizungumza na vyombo vya habari mjini Musoma jana, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ali Hapi alisema akiwa mkoani humo, Februari 6 na 7 Rais Samia atazindua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
"Atazungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali katika Wilaya za Musoma, Butiama pamoja na Bunda," alisema Hapi.
Alisema miradi itakayokaguliwa na kuwekewa mawe ya msingi na Rais Samia ni mradi wa maji wa Mugango Kiabakari – Butiama na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kwangwa. Mingine ni kuweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Ujenzi wa Chujio la Maji Bunda Mji na Mradi wa Ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Wilaya ya Butiama.
Alisema Rais Samia pia atatembelea ujenzi wa Chujio la Maji Bunda unaogharimu Sh bilioni 10.6, mradi wa maji wa Mugango Kiabakari – Butiama unaogharimu Sh bilioni 70.863 na mradi wa ujenzi wa ofisi za makao makuu ya wilaya ya Butiama unaogharimu Sh bilioni 3.265.
Alisema Rais Samia atazungumza na wananchi wa Musoma Vijijini, Manispaa ya Musoma na kwamba akiwa Butiama pamoja na kuzungumza na wananchi pia atakwenda kuzuru kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Hapi alitoa wito kwa wananchi mkoani humo kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais Samia katika maeneo yote atakayopita, tangu atakapoingia mkoani humo kuanzia kwenye mpaka wa mkoa huo na Mwanza, Bunda, Butiama, Kyabakari mpaka kwenye makao makuu ya mkoa mjini Musoma.
Aliwataka wananchi wa wilaya zote za mkoa huo na maeneo mengine kushiriki shughuli zote zitakazofanywa na Rais Samia akiwa mkoani humo.
Alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha kunakuwa na usalama wa kutosha kabla na baada ya ujio wa ugeni huo wa kihistoria mkoani Mara.
"Niwahakikishie Watanzania kwamba tumekubaliana na watoa huduma mbalimbali zikiwamo za vyakula, malazi na usafiri kwamba watatoa huduma kwa saa 24 kuanzia Februari 3, wageni wataweza kupata chakula hata usiku wa manane," alisema.
Hapi aliwaomba wakazi wa Mara wajitokeze kwa wingi kumsikiliza Rais Samia na pia wafanyabiashara wachangamkie fursa hiyo kuongeza vipato vyao kwa kuwa kutakuwa na wageni wasiopungua 5,000.