Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia ataka viwanja CCM viboreshwe

D6f7dcbe74561dbab6a311e6919c341d Samia ataka viwanja CCM viboreshwe

Wed, 16 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, amekitaka chama hicho kufanya maboresho ya viwanja vyake na kuiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kujenga vituo vya michezo mikoani.

Akizungumza jijini Mwanza jana kwenye mkutano wa vijana, Rais Samia alisema viwanja vingi vinavyomilikiwa na CCM hali yake hairidhishi, hivyo kwa vile fursa imetoka ya punguzo la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa nyasi bandia chama hicho kinapaswa kuvitengeza.

Kauli ya Rais Samia imekuja siku chache tangu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba azungumzie suala la ubovu wa viwanja na punguzo la VAT kwa nyasi bandia katika hotuba yake ya Bajeti Kuu ya Serikali aliyoitoa hivi karibuni bungeni, Dodoma.

“Nizungumze na Chama changu cha Mapinduzi, viwanja vingi vinamilikiwa na wao lakini hali yake hairidhishi, sasa niombe vitengenezwe, viwekwe nyasi bandia ili vijana wetu watumie kujiendeleza kimichezo, lakini na wao walipe thamani ya ile pesa wanayoitoa kutumia viwanja hivyo.”

“Namtaka Naibu Katibu Mkuu (wa CCM) kuandaa programu ya kuviboresha na kama hawawezi watafute mwekezaji ili viwanja viwekwe nyasi za bandia kwani michezo ni ajira,” alisema.

Rais Samia alisema pia serikali imechukua hatua za kuimarisha usimamizi wa hatimiliki za wasanii, hivyo kuanzia Desemba, mwaka huu wasanii wataanza kulipwa mirahaba yao kutokana na kazi zinazotumiwa kwenye runinga, redio na mitandaoni.

Alisema pia serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ili kuziandaa na kuzisaidia timu za taifa.

Kuhusu vituo vya soka, Rais Samia alimwagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa kuanza kufikiria kujengwa mikoani.

“Nimesikia kuna jambo kubwa utakalolijenga lakini lile litakuwa kwenye mkoa mmoja kati ya Dar es Salaam, Dodoma au popote mtakapoamua,” alisema na kuongeza kuwa ikiwa vituo vya michezo vitajengwa mikoani vitasaidia kukuza vipaji vingi.

Awali, Bashungwa alizungumzia mambo mbalimbali akisema upande wa sanaa wizara hiyo ipo katika jitihada za kuleta mageuzi makubwa.

Alisema hapo nyuma Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Bodi ya Filamu na Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota), wasanii walikuwa wanapata shida kufika katika ofisi zao lakini sasa wameanza kuziunganisha ili ziwe sehemu moja.

Sambamba na hilo alisema ameshatoa maelekezo kwa Cosota ishirikiane na TCRA kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mirahaba ya kazi za wasanii.

Pia, alisema mwaka huu wanatarajia kurudisha utoaji wa tuzo kwa wasanii wa sanaa zote na zitatolewa mwishoni mwa mwaka huu.

Alitoa wito kwa vijana nchini kuwa, pamoja na kupenda taaluma katika shule za msingi, sekondari hadi vyuo, wasisahau vipaji ambavyo wamepewa na Mwenyezi Mungu kwasababu katika maisha hawajui kipi kitawapa ajira.

Bashungwa alisema pia wizara hiyo imetenga fedha kwa ajili ya kupata mshauri wa ujenzi wa arena ya michezo ‘Sports and arts Arena’ nchini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz