Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia aomba kura kumalizia kazi

347726ba39a9b33d2918bbc94e1f5fa4 Samia aomba kura kumalizia kazi

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Jimbo la Momba mkoani Songwe kuendelea kukiamini chama hicho ili waweze kutatuliwa changamoto ya barabara na madaraja ambayo hufanya wajawazito kujifungulia nyumbani.

Alisema hayo jana katika kata ya Chitete wilayani Momba akiwa kwenye kampeni za kuwanadi mgombea urais, wabunge na madiwani mkoani Songwe.

Alisema mikakati ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inaboresha sekta ya afya kwa kuboresha barabara na madaraja ambayo huunganisha vijiji na kata ambako huduma za afya hupatikana.

Alisema anatambua kuwa miundombinu ya usafirishaji kwa jimbo la Momba ina changamoto kubwa, hali ambayo husababisha wananchi wa eneo hilo kukosa huduma za kijamii hasa wajawazito kushindwa kusafiri kwenda kujifungulia hospitalini.

“Mpango wa serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati na kila kata inakuwa na kituo cha afya, tayari tulishaanza, tupeni miaka mitano mingine, ndani ya miaka mitatu tuhakikishe tunamalizia na kutatua changamoto ya wajawazito kutembea umbali mrefu kufuata matibabu,” alisema.

Aliongeza kuwa pia wanatambua kuwa licha ya mito mingi inayozunguka jimbo la Momba kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji na kufanya wananchi kukosa maji safi na salama.

Kuhusu elimu, Samia alisema ndani ya miaka mitano uandikishwaji watoto kuingia darasa la kwanza imeongezeka na kufanya idadi ya watoto wanaotoka kaya masikini kuongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Kwa upande wake mgombea ubunge jimbo la Momba, Condester Sichalwe alisema kukatika kwa vivuko na madaraja kipindi cha masika husababisha baadhi ya akinamama kujifungulia njiani.

Alisema jimbo la Momba lina kata 12 na vijiji 72, ambavyo vyote pamoja na changamoto zake anazijua hivyo aliwaomba wananchi wa Momba kumuunga mkono na CCM ili waweze kupata maendeleo na kukuza uchumi wao.

Chanzo: habarileo.co.tz