Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia: Viongozi tendeni haki!

432e0617886b0462264c8034279ab3cc Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Sun, 13 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wote nchini wenye uwezo na nafasi ya kusikilizwa na jamii kuwa mfano wa kutenda haki na waache kunyoosheana vidole kama wajibu huo ni wa mtu mmoja.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene katika Mkutano wa tano wa maombi jana ulioandaliwa na Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya Kingdom Leadership Network of Tanzania (KLNT), Rais Samia alisema kila mtu anatakiwa kuwa mfano wa kutenda haki.

“Kila mtu katika jamii anayeweza kusikilizwa anatakiwa kuwa mfano wa kutenda haki, asiwe na wajibu wa kunyooshea wengine vidole. Haki ikitendwa katika jamii kwa kujali sheria bila kujali ni kiongozi wa aina gani, nchi itakuwa salama na maombi tunayoomba yatabarikiwa sana,” alisema.

Alisema viongozi wa dini, wa wafanyabiashara, wanasiasa na hata viongozi wa serikali, wakionesha mfano nchi itastawi na itasimama na kusonga mbele.

Samia alipongeza ushirikiano wa taasisi za Kikristo ambazo zimeshiriki katika mkutano huo kama TEC, CCT, SDA, CPCT pamoja na za Kiislamu na kuahidi kwamba serikali itatembea pamoja na taasisi za dini na taasisi nyingine katika kudumisha ushirikiano huo.

Alisema serikali inadumisha utawala bora, haki za binadamu na kwa kuzingatia utawala wa sheria, kwani huo ndio msingi wa uchumi hasa wa viwanda ambao unajengwa sasa na lengo ni kutimiza kanuni za utawala bora ili kuhakikisha uchumi unakuwa wa kati na juu.

“Tutumie silaha tulizobakiza kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati wa juu. Moja ya silaha hizo ni amani na hiyo itakuja kama kutakuwa na haki. Hivyo viongozi tuwe wadau wa kushabikia amani…mtu wa Mungu anayesamehe anaomba baraka za Mungu, lakini akitaka kumtenda mwenzake sababu ametendewa, sheria hiyo imefanya mataifa mengi duniani kuanguka, Tanzania ikitaka isianguke watu wake wanatakiwa kusameheana,” alisema.

Rais Samia alisema serikali inaamini katika maombi yanayolenga kuhimiza utawala bora na uadilifu na imekuwa ikitunza maadili kwani ni miongoni mwa tunu za taifa.

Akitoa maoni yake katika mkutano huo, Waziri Simbachawene alisema madai ya kutaka kutungwa Katiba mpya si ya muhimu kwani iliyopo ni nzuri kwani yote waliyosema viongozi wa dini yamo ndani yake.

Simbachawene alisema kwenye maombi na sala zilizotolewa asubuhi na viongozi wa dini zimehimiza haki za binadamu, uhuru wa watu lazima, vyote hivyo vimesemwa vipo ndani ya Katiba.

Alisema inawezekana kuna upungufu katika baadhi ya vifungu, lakini hivyo havilazimishi kutunga katiba mpya kwani mambo ya msingi yanayohusu haki za binadamu walizozungumza viongozi wa dini yapo ndani ya Katiba hiyo.

Mwakilishi wa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Mbunge wa Nsimbo, Anna Lupembe alisema kuanzia mwakani mhimili wa Bunge utakuwa ukishiriki kikamilifu katika mkutano huo ambao unalenga kuwatia moyo vijana katika kutumia fursa na hasa uhamasishaji wa amani katika nchi yetu.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk Barnabas Mtokambali alisema mkutano huo umeongeza ari kama viongozi mbalimbali wanatakiwa kuongoza kwa haki na uadilifu kwa namna Mungu anavyotaka.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Tanzania, Mark Walya Malekana alisema Tanzania ina makabila zaidi ya 120 pamoja na viongozi wa dini na viongozi wa serikali, hivyo wanatakiwa kuungana pamoja kudumisha haki na kutekeleza wajibu katika kuleta uhuru wa kiuchumi baada ya kupata uhuru wa kisiasa.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk Frederick Shoo alisema vijana wakitaka kufanikiwa katika maisha yao na hasa kuja kushika madaraka baadaye, wanatakiwa kuwa waadilifu na kumcha Mungu.

Mlezi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Kingdom of Leadership Netwok Tanzania (KLNT), Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alimshukuru Mungu kwa kufanikisha mkutano huo wa tano ulioandaliwa na taasisi hiyo na akasema hakuna utawala unasimama bila kumtegemea Mungu hivyo vijana wakitaka kufikia ngazi ya uongozi wa juu wanatakiwa kuwa waadilifu, wachapakazi, wazalendo kwa nchi yao na hasa kumtegemea Mungu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz