Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia: Sina mashaka Tutashinda

4bc1ae6c592d0317120d6ce3b77c6484 Samia: Sina mashaka Tutashinda

Mon, 12 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA mwenza wa urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan amesema, kwa kuzingatia kazi iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano hana mashaka kuwa chama hicho kitashinda Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Ameyasema hayo jana wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Muze wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.

“Ndugu zangu sina wasiwasi na jimbo hili la Kwela lakini uungwana unasema tuje na tuombe kura. Mmetusikia tunazinguka Tanzania nzima.Mheshimiwa Rais anazunguka kwake, Waziri Mkuu anazunguka kwake, mimi nazunguka kwangu. Kwa kazi tuliyoifanya Tanzania hatuna wasiwasi tungeshinda lakini uungwana ni kuja kukuoneni na kuomba. Tunaomba mtuamini tena”

Katika mkutano huo Mama Samia alimuombea kura mgombea urais wa Tanzania John Magufuli, mgombea ubunge jimbo la Kwela, Deus Sanga na wagombea udiwani.

“Mkituacha nje hatuwezi kuyatimiza, mkutupa kura tena kwa wingi tunakwenda kuyatimiza”alisema Mama Samia.

Alitoa mfano wa miradi mikubwa kuwa ni ya kuzalisha umeme ili wananchi wote wapate nishati hiyo.

Alisema, Tanzania inatarajia kuwasha umeme katika vijiji vyote ifikapo mwaka 2023 kutokana na miradi endelevu iliyoainishwa katika ilani ya CCM kwa ajili ya utekelezwaji katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025.

Alisema kutokana na miradi mikubwa ya umeme inayoendelea kutekelezwa na serikali ya CCM mipango ya kusambaza umeme nchi nzima itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu tangu.

Mbali na miradi mikubwa ya kufua umeme ya Kinyerezi I na II, serikali chini ya Rais John Magufuli inaendelea kujenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa njia ya maji wa Julius Nyerere katika mto Rufiji unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115.

Alisema, kutokana na dhamira ya Rais Magufuli kuwafikishia umeme wakazi wa Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla, Tanesco wamejitahidi kutandaza nguzo katika jimbo la Kwela na maeneo mengine.

“Pamoja na jimbo hili kuwa na jiografia ngumu iliyotengenezwa kwa kiasi kikubwa na milima lakini serikali ya CCM haikukata tamaa na kuwatelekeza Wanakwela, nilipokuwa napita kwa helkopta nimejionea jinsi kazi ya kusambaza umeme huku ilivyofanyika katika mazingira magumu hasa kupitisha nguzo na nyaya milimani,” alisema Mama Samia.

Alisema pamoja na mambo mazuri yaliyokwishafanywa na serikali ya CCM, bado serikali ina ya kuwasaidia wananchi wa Kwela na Rukwa kwa ujumla.

Mama Samia alisema serikali ya CCM inatarajia kujenga kwa kiwango cha lami barabara zote zinazoliunganisha taifa na nchi jirani ikiwemo barabara inayounganisha jimbo la Kwela na nchi jirani ya Zambia.

Mgombea ubunge katika jimbo la Kwela, Sanga aliishukuru serikali kwa kurahisisha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya jimbo hilo ambalo ni kubwa kuliko yote mkoani Rukwa.

Alisema kutokana na ugumu wa jiografia ya jimbo hilo hasa kuwasiliana na makao makuu ya wilaya ya Sumbawanga, serikali imejitahidi kufungua milango katika mikoa mitatu kutokea katika jimbo hilo.

“Ni rahisi sana kutoka hapa Kwela kwenda Kigoma kuliko kutoka hapa kwenda Sumbawanga ambako ndio makao makuu ya Mkoa wetu wa Rukwa. Tunaiomba serikali yetu sikivu itusaidie kutufungulia njia katika mikoa hii mitatu,” alisema Mgombea Ubunge wa Kwela.

Sanga alimhakikishia Makamu wa Rais kuwa katika jimbo hilo lenye idadi ya watu wanaofikia 187,000 na kata 27 zote zitaichagua CCM na kura za mafuriko zitapelekwa kwa Magufuli.

Chanzo: habarileo.co.tz