Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la Ma-DED Uchaguzi Mkuu laibuka upya Bungeni

Bunge Pic Data Sakata la Ma-DED Uchaguzi Mkuu laibuka upya Bungeni

Tue, 30 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pendekezo la Serikali ya Tanzania la kutaka wakurugenzi wa halmashauri (DED) waendelee kusimamia uchaguzi linaonekana kuwa kaa la moto, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuja na pendekezo jipya juu ya suala hilo.

Wakurugenzi wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya kupendekezwa na muswada wa sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa 2023 kuendelea kusimamia uchaguzi, limeibua mvutano kwa wadau wa demokrasia.

Baadhi ya vyama vya siasa kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ndicho chama kikuu cha upinzani nchini humo, wanaharakati, wanazuoni, viongozi wa dini wanapinga kundi hilo kusimamia uchaguzi.

Sababu kubwa inasababisha wanaopinga kubisha hodi mahakamani kuomba tafsiri ya Mahakama, ni kwamba hao huteuliwa na Rais kuwa wakurugenzi na baadhi wanatajwa kuwa ni makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mbali na hoja hiyo, baadhi ya wadau wa demokrasia wanaona si sahihi mtu aliyeteuliwa na Rais ambaye kwa sasa ni mwenyekiti pia wa CCM kinachoshiriki uchaguzi, kusimamia uchaguzi kwa madai kuwa hauwezi kuwa huru na haki.

Juni 13, 2023, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, ilitoa hukumu ya kupiga Ma-DED kusimamia uchaguzi na kuipa Serikali ya Tanzania miezi 12 kupeleka ripoti ya utekelezaji wa amri hiyo.

Mei 2019, jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu lilibatilisha kifungu 7(1) cha sheria ya uchaguzi kilichokuwa kinaipa NEC mamlaka ya kuwafanya Ma-DED kusimamia uchaguzi, uamuzi uliotenguliwa na mahakama ya Rufani Oktoba 2019.

Hata hivyo, wadau walikuwa na matumaini muswada huo wa sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2023, ungezingatia maoni yao juu ya swala hilo, lakini uliposomwa kwa mara ya kwanza, hakukuwa na mabadiliko.

Hii ndio ilikifanya Chadema kutaka miswada hiyo pamoja na muswada wa sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani uondolewe bungeni na hili likawasukuma kufanya maandamano ya amani wiki iliyopita, Jijini Dar es Salaam.

Leo Jumanne, Januari 30, 2024 kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameandika kuwa maoni yao na ya wadau yamepuuzwa na kueleza kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, miswada hiyo aliyodai ni mibovu utajadiliwa.

Hata hivyo, baada ya miswada hiyo kusomwa kwa mara ya pili Bungeni Jijini Dodoma leo Jumanne Januari 30, 2024 na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge na Uratibu, Jenister Mhagama, kamati ya Bunge imewasilisha maoni yao ambayo yana maoni tofauti juu ya suala hilo.

Taarifa iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama ilieleza kamati ina maoni kwamba sheria isiweke ulazima kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kusimamia uchaguzi.

Badala yake, imeshauri kuwepo na masharti ya mtumishi wa umma mwandamizi ama mtu mwingine yoyote mwenye sifa kuteuliwa kuwa msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi.

Kamati hiyo imesema Serikali iliona upo umuhimu wa wakurugenzi watendaji kutajwa kwenye sheria kwa kuwa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu ziliona hazikiuki masharti ya Katiba.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, inaona hakuna ulazima wa sheria kuweka sharti kwa mkurugenzi wa jiji, manispaa, mji na wilaya kuwa wasimamizi wa uchaguzi au wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kama kifungu hicho cha 6 (1) kinavyoeleza.

Kamati hiyo imesema hiyo ni kwa kuwa uzoefu unaonyesha wapo wakurugenzi kwa sababu mbalimbali wanapoteza sifa za kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Kwa hoja hiyo, kamati hiyo ikalieleza Bunge imeandaa jedwali la marekebisho ya kamati ya kuwatumia watumishi wa umma waandamizi ama mtu yoyote mwenye sifa kwa lengo la kuendesha uchaguzi katika jimbo au kata.

Awali, akiwasilisha maelezo ya Serikali, Waziri Mhagama amesema sheria inayopendekezwa katika muswada wa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani unakusudia kuunganisha sheria mbili zinazohusiana na masuala ya chaguzi.

Sheria hizo ni sheria ya uchaguzi sura ya 343 na sheria ya uchaguzi ya serikali za mitaa, sura ya 292 ambapo waziri Mhagama amesema hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba masharti ya sheria hizo mbili za uchaguzi yanafanana.

“Kutungwa kwa sheria ambayo itaunganisha masharti yote katika sheria moja kutarahisisha usimamizi na utekelezaji wa masharti hayo ikizingatiwa kuwa sheria hizo hutekelezwa na mamlaka moja ambayo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi,”amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live