Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema chama hicho kinaridhishwa na urafiki na uhusiano wake na Chama cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV), na kipo tayari kuendeleza ushirikiano kati ya pande hizo mbili utakaoongeza fursa kwa Tanzania kunufaika zaidi, hasa kupitia nyanja za sayansi na teknolojia, kukuza uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, maeneo ambayo Vietnam ina uzoefu mkubwa.
Chongolo amesema kuwa kupitia uhusiano wa kihistoria yaliyopo kati ya CCM na CPV, kisiasa, kijamii na kiuchumi, vyama hivyo vitaimarisha zaidi misingi itakayotumiwa na Serikali za nchi zote mbili, Tanzania na Vietnam, katika kubadilishana uzoefu na mikakati sahihi ya kubadili hali za maisha ya watu, kupitia sekta ya uzalishaji, ambayo ni hatua muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Amesema hayo alipokutana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CPV, Prof. Le Hai Binh, leo, kwenye mazungumzo ya kikazi yaliyofanyika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Komredi Prof. Le Hai Binh, amesema kuwa thamani ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali yake na nchi ya Tanzania kwa ujumla mbele ya CPV na Vietnam, ni kubwa mno, kwa sababu za kihistoria, ambapo vyama hivyo na nchi zote mbili zina mtazamo mmoja wa itikadi ya kisiasa na kiuchumi, na historia imewapitisha katika ushirikiano wa mapambano wa watu wanyonge kujikomboa.