Mnamo Oktoba 22, 2023, Chama cha Mapinduzi (CCM), kupitia kikao cha Halmashauri Kuu kilichoketi chini ya Mwenyeiti wake Samia Suluhu Hassan, kimemteua aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi wa chama hicho tawala nchini.
Makonda anachukua nafasi ya Sophia Edward Mjema ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais Masuala ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalum. Mjema pia aliwahi kuhudumu kama Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, pamoja na nyadhifa zingine alizowahi kuzihudumia.
Licha ya Makonda kutokuwa mtu pekee aliyetangazwa kwenye teuzi hizi za sasa, ni uteuzi wake ambao unaendelea kujadiliwa kwa shauku kubwa na Watanzania, huku wengine wakimtabiria kuchukua nafasi hiyo kabla ya hata uteuzi wake haujatangazwa.
Ifuatayo ni historia fupi ya safari ya kisiasa ya Paul Makonda ambayo inaangazia baadhi ya matukio muhimu yaliyochangia kwenye kutengeneza historia hiyo.
Julai 29, 2011: Rais wa wanafunzi wa Chuo cha Ushirika Moshi (MUCCoBS) amteua Paul Makonda kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi. Uteuzi huu wazua mjadala mkali katika Bunge la Wanafunzi, huku baadhi ya wabunge wakionesha kutokuwa na imani naye kwa sababu ya kuhairisha mwaka wa masomo chuoni hapo.
Septemba 27, 2011: Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) wamchagua Paulo Makonda katika nafasi ya Mwenyekiti, akiwashinda wagombea wengine kutoka vyuo vikuu vinne.
Oktoba 1, 2012: Makonda ajiuzulu nafasi ya uenyekiti TAHLISO Taifa kwa kile alichodai ni kuepusha mgongano wa kimaslahi kwa kuwa alipanga kushiriki uchaguzi katika chama chake cha siasa, Chama cha Mapinduzi (CCM).
Oktoba 24, 2012: Paul Makonda agombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) na kushika nafasi ya pili baada ya kupata kura 241 nyuma ya Mboni Mhita aliyepata kura 489 katika duru ya pili ya uchaguzi huo.
Makonda alilaumu vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo na kusema kwamba vinawanyima fursa watoto wa wakulima na watu masikini. Katika safu mpya ya uongozi wa UVCCM baada ya uchaguzi huu, Makonda aliteuliwa kuwa Katibu wa Hamasa na Chipukizi.
Februari 7, 2014: Rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete amteua Paul Makonda kuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba, akiwakilisha kundi la watu wenye malengo yanayofanana linalojumuisha wajumbe 14 kutoka Tanzania Bara.
Februari 19, 2015: Rais Kikwete ametua Paul Makonda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.
Machi 13, 2016: Rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli afanya mabadiliko na uteuzi wa Wakuu wa Mikoa 26. Katika uteuzi huo, amteua Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Machi 22, 2017: Kamati iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Habari Nape Nnauye kuhusu uvamizi katika kituo cha utangazaji cha Clouds yabainisha Paul Makonda alivamia kituo hicho mnamo Machi 17, 2017, majira ya usiku.
Kufuatia taarifa hiyo, wadau mbalimbali, ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilimtaka Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Makonda. Makonda hakutenguliwa.
Januari 31, 2020: Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani yatoa taarifa ya marufuku kwa Makonda na mke wake, Mary Felix Massenge, kutoingia nchini humo kwa madai ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Julai 15, 2020: Rais Magufuli amuondoa Paul Makonda katika nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Utenguzi huo ulihusianishwa na hatua ya Makonda kutangaza nia ya kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Kigamboni.
Julai 20, 2020: Makonda aibuka mshindi wa pili kwenye uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM kwa kupata kura 112, nyuma ya mbunge wa jimbo hilo anayemaliza muda wake, Faustine Ndugulile.
Juni 9, 2022: Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni yatupilia mbali kesi iliyokuwa ikimkabili Makonda na Mkurugenzi wa Mashitaka juu ya matumizi mabaya ya madaraka wakati wakiwa viongozi wa umma. Kesi hiyo ilifunguliwa na Said Kubenea aliyewahi kuwa Mbunge wa Ubungo.
Oktoba 22, 2023: CCM yamteua Paul Makonda kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi.