Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Safari Katiba mpya kuanza tena

Katibapic Data 1140x640 Safari Katiba mpya kuanza tena

Sun, 26 Mar 2023 Chanzo: Mwananchi

Safari ya Watanzania kuipata Katiba mpya imeanza tena baada ya Serikali kutangaza kuongeza takribani Sh9 bilioni katika bajeti ijayo ya Wizara ya Katiba na Sheria ya mwaka 2023/2024.

Kutengwa kwa bajeti ya kuukwamua mchakato huo hata hivyo kumepokewa kwa hisia tofauti, ikiwemo pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliahidi kuuendeleza.

Mchakato huo ulikwama Aprili 2, 2015 kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutangaza kuahirisha kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyokuwa ifanyike Aprili 30 mwaka huo hadi itakapotangazwa tena.

NEC ilitoa sababu ya kutokamilika kwa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa njia ya kielektroniki (BVR). Baada ya Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli kuingia madarakani Novemba 5, 2015 hakuonyesha kusudio la kuuendeleza, licha ya wadau mbalimbali kumtaka kufanya hivyo. Februari 2018, Rais Magufuli akiwa katika kongamano la kujadili siasa na uchumi lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema hakukuwa na fedha za kuugharimia mchakato wa Katiba Mpya. “Tusitumie hela kuwalipa watu wakae vikao. Ni bora tukajenge reli. Kwa sasa sitegemei kutenga hela kwa ajili ya kuwapeleka watu kujadili Katiba na kama kuna mtu anataka kutupa hela kwa ajili hiyo, azilete tutajengea reli,” alisema Rais Magufuli ambaye Machi 17, 2021 alifariki dunia. Juni 28, 2021 akizungumza na wahariri na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan aliomba apewe muda aifungue nchi kiuchumi, kwani umeshuka na baadaye mchakato huo utafuatia. ‘‘Mchakato wa Katiba ni wa maana, maana sana. Ninawaomba nipeni nchi niisimamishe kiuchumi, halafu tutashughulikia mengine, tutashughulikia Katiba, mikutano ya hadhara na mengine,” alisema Samia ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba. Tayari Rais Samia amekwisha ondoa zuio la mikutano ya hadhara lililowekwa na hayati Magufuli mwaka 2016 na sasa vyama vya siasa vinafanya mikutano maeneo mbalimbali nchini.

Kufufua mchakato Kwa nyakati tofauti, Rais Samia amekuwa akieleza kuufufua mchakato huo wa Katiba na kauli hiyo ilipata nguvu kwa Halmashauri Kuu ya CCM ambayo yeye ni Mwenyekiti, kuishauri Serikali kuufufua mchakato huo. Machi 8 mwaka huu, akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Rais Samia alisema anakusudia kutangaza kamati itakayopitia na kushauri jinsi ya kuukwamua mchakato huo. Februari 2020, akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema mchakato huo ni lazima ukamilishwe. “Lazima tutakamilisha mchakato wa Katiba, mchakato huwa ni mrefu, ilichukua miaka 10 hadi 13 kupata Katiba mpya baada ya Muungano. Tumeanza mwaka 2013, mimi ninaamini kazi kubwa imeshafanyika ya kufikia Katiba Mpya,” alisema Jaji Warioba.

…safari yaanza Jana, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro ndio kama alitangaza kuanza kwa safari ya mchakato huo, wakati akifungua baraza la wafanyakazi la wizara hiyo, kwa kueleza bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao itaongezeka kwa Sh9 bilioni. Ongezeko hilo linakwenda kugharimia utekelezaji maagizo ya Rais Samia, ukiwemo mchakato wa Katiba mpya na marekebisho ya sheria zinazohusiana na demokrasia. Pia, siasa na uchaguzi, ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya kikanda na Kiafrika, kidunia ya haki za binadamu na kampeni ya kutoa elimu na msaada wa kisheria. Waziri Ndumbaro alisema katika utekelezaji huo, watakwenda kuomba kuidhinishiwa na Bunge katika bajeti ya 2023/2024 Sh36 bilioni ikiwa ni ongezeko la takribani la Sh9 bilioni. “Tujipange inawezekana Sh9 bilioni isitoshe kwa hiyo lazima tujipange kuweza kuomba suplimentary (nyongeza) ya bajeti. Hivyo ikifika Septemba hadi Oktoba tuwe tumejipanga,” alisema. Waziri Ndumbaro alisema usimamizi wa utekelezaji wa maagizo hayo utakuwa chini ya Naibu Waziri, Pauline Gekul na naibu katibu mkuu akishirikiana na kikosi cha wataalamu watakachokiunda. “Hitaji la Katiba Mpya ni hitaji la Watanzania na wizara yenye jukumu ni hii, sasa jukumu hili ni zito sana linataka kujipanga ipasavyo. “Linataka rasilimali ya kutosha ndio maana nimewaomba wawe mstari wa mbele na sisi tutakuwa tunawashauri na kuwaelekeza tukipata mrejesho kutoka kwenu,” alisema. Hata hivyo, alisema wasipopata rasilimali za kutosha hawataweza kulitekeleza na wasipolitekeleza jukumu hilo, Watanzania hawatawaelewa na kuwa jukumu lao ni kuwatumikia Watanzania.

Walichokisema wadau Mara baada ya kauli hiyo ya Waziri Ndumbaro, gazeti hili lilizungumza na wadau mbalimbali, akiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye alisema: “Ni jambo jema kama wametenga fungu na wanaishi kwa vitendo yale tunayozungumza; ni hatua muhimu na ya lazima.” Mbowe alisema mazungumzo ya maridhiano yanaendelea na wiki ijayo watakutana kuendelea na mazungumzo aliyodai yanaleta tija kwa Taifa. Kwa upande wake, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alisema baada ya kutengwa fedha, hatua muhimu zinapaswa kufuatwa kukwamua mchakato wa Katiba mpya kama ilivyopendekezwa kwenye kikosi kazi. Mchakato huo, alitaka uanze na kuhusishwa kwa sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ili kuweka taratibu za kisheria kupata Katiba mpya. “Kuundwa kwa timu ya wataalamu kuwianisha rasimu za Katiba zilizopo, yaani ya Warioba (Jaji Mstaafu Joseph) na pendekezwa na mchakato uanze sasa,” alisema. Kwa mujibu wa Zitto, mkutano wa kitaifa unahitajika kufanyika ili kupata mwafaka wa masuala yaliyokwamisha mchakato wa awali wa mwaka 2014. Maoni hayo yaliungwa mkono na Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe akisema: “Kwanza kuwepo majadiliano ya pamoja na marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. “Pili, kuwe na kamati ya wataalamu itakayooanisha rasimu ya Jaji (Joseph) Warioba na Katiba inayopendekezwa ili kupata yale mambo ya msingi, kisha yarudishwe kwa wananchi,” alisema. Hata hivyo, aliitaka Serikali kuhakikisha fungu hilo linapatikana. “Kumekuwa na utaratibu wa kutenga fedha kwenye bajeti, lakini hazifikishwi zote, kwa hiyo tunachotaka ni utekelezaji.” Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema hiyo ni hatua muhimu inayotakiwa kukamilishwa. “Kusingetengwa bajeti ningeshangaa, kwa sababu Rais Samia amesharuhusu mikutano ya hadhara, kilichobaki ni mchakato wa Katiba ambao kwa vyovyote vile tulitegemea utafuata. Naye mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Revocatus Kabobe alisema kauli hiyo ni ishara kwamba Serikali imesikia kilio cha wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba tangu mwaka 1992.

Chanzo: Mwananchi