Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu zatajwa mafuriko ubunge

37206469ac1e7f45f99a3e2ea4c821b0 Bunge

Sat, 18 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UTENDAJI kazi mzuri wa Rais John Magufuli, unaozingatia utu, haki, usawa na demokrasia, ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), umetajwa kuwa miongoni mwa sababu za watu wengi kujitokeza, kuomba kugombea nafasi za ubunge na udiwani ndani ya chama hicho.

Kwa mara ya kwanza ndani ya historia ya Tanzania, wanachama wengi wamejitokeza kuomba ridhaa ya kuwakilisha CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, hususani katika nafasi za ubunge. Wachambuzi wa siasa nchini wamesisitiza kuwa mvuto wa chama hicho kwa sasa, unachangiwa na utendaji thabiti wa Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM. Sababu zingine ni maslahi ya kisiasa na kiuchumi na kutafuta nafasi zaidi za vyeo.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Sayansi ya Siasa, Dk Richard Mbunda alisema moja ya sababu za mafuriko hayo ya wagombea ndani ya CCM ni mvuto wa chama hicho.

“Kabla ya Rais Magufuli hajaingia madarakani mwaka 2015, CCM kukubalika kwake kulishuka sana kiasi cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahaman Kinana kupita mikoani kukiuza chama hicho...” Alisema, “Kuna kipindi ilifikia hadi akagombana na mawaziri na wengine aliwaita mawaziri mizigo. Lakini alipoingia Rais Magufuli chama kilianza kuwa na mvuto tena.”

Alisema mvuto huo ulianza kuonekana kupitia alichoita gharika la madiwani na wabunge kutoka upinzani kujiunga na CCM, jambo lililochangia wananchi kujenga nasaba na chama hicho. Aidha, alisema sababu nyingine ya wanachama wa CCM kukimbilia kuchukua fomu za kuwania ubunge, udiwani na uwakilishi ndani ya chama hicho ni umaarufu na maslahi, pindi wasifu wao utakaobainishwa mbele ya viongozi wakuu wa nchi.

Alifafanua kuwa huenda hali hiyo, ilichangiwa na mtindo alioutumia Magufuli mwaka 2015 wakati akiunda timu yake ya kazi, ambapo watendaji wake wengi walitokana na wanachama wa CCM waliogombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu.

“Hata hivyo, mazingira ya 2015 ni tofauti na ya mwaka huu kwani mwaka 2015 Rais alikuwa akipanga timu yake lakini sasa inawezekana tayari timu anayo, hivyo wengi wanaweza wachaguliwe au wasichaguliwe,” alifafanua Dk Mbunda.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala alisema hajawahi kuona wimbi la wananchi waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika maisha yake kama mwaka huu. Alisema kwa mtazamo wake, sababu kubwa huenda ikawa ni mwamko mkubwa wa kisiasa na kizalendo miongoni mwa Watanzania, kutaka kutumikia nchi yao vizuri kwa kuingia katika ngazi za uongozi.

Alitaja sababu nyingine ni maslahi, akisema kwa kuwa binadamu yeyote hutafuta kwanza maslahi anufaike na awe na maisha mazuri. “Inatokea katika nchi yetu na nchi nyingine duniani mambo yenye maslahi ni biashara kubwa na siasa. Mfano tu kwenye siasa nafasi ya ubunge pekee kipindi cha miaka mitano mtu anaweza kutengeneza hela itakayomsaidia maisha yake yote,” alisema Profesa Mpangala.

Alisema katika ubunge, maslahi anayopata ndani ya kipindi hicho cha miaka mi tano ni pamoja na mshahara mnono na posho mbalimbali. Pia baada ya kipindi chake cha miaka mitano, anapata kiinua mgongo ambacho sasa kinafikia hadi Sh milioni 400.

“Kuna watu na elimu zao wanafanya kazi maisha yao yote hawapati kiasi hicho cha fedha. Pamoja na maslahi lakini ubunge pia unaleta heshima katika jamii,” alisema. Alisema sababu nyingine inayovutia wanachama wengi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kupitia CCM mwaka huu, uwapo matarajio ya kushinda kuliko upinzani.

“CCM wagombea wake katika ngazi zote wanashinda ndio maana watu wanakimbilia huko kwa kuwa fursa ya ushindi ni kubwa,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Chirongo Keregero alisema sababu nyingine ni namna ambavyo kumekuwa na msingi wa haki, utu, usawa na uongozi bora katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Magufuli, hali iliyovutia wengi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

“Kwa jinsi watu wengi walivyojitokeza kutia nia na kugombea nafasi mbali mbali ndani ya CCM, implications yake ni kuwa watu wanaamini haki kama msingi uliojengwa katika miaka mitano iliyopita,” alisema Keregero. Juzi wakati wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu Chamwino jijini Dodoma, Rais Magufuli alisema kwa takwimu alizonazo mpaka jana yake, jumla ya wanachama wa CCM 8,205 walichukua fomu za kuomba ridhaa ya chama hicho kukiwakilisha katika nafasi za ubunge na uwakilishi nchi nzima.

Rais Magufuli alisema wingi huo wa wanachama waliojitokeza, ni dalili nzuri kwamba chama hicho kinapendwa. Aliwataka wanaCCM kuzingatia nidhamu na maadili ya chama.

Chanzo: habarileo.co.tz