Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za Mbunge kujiuzulu Ubunge Pemba

216cfd6690f6075246e5b86abaeab559.png Sheha Mpemba Faki

Wed, 4 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

ALIYEKUWA Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sheha Mpemba Faki, amesema amelazimika kujiuzulu baada ya kupokea vitisho kutoka kwa watu mbalimbali ikiwa na madai kuwa wapinzani wanataka kumdhuru na familia yake.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Msuka Mkoa wa Kaskazini Pemba, alisema baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza kuwa mshindi katika uchaguzi mdogo wa hivi karibuni jimboni Konde, amekuwa akipokea vitisho vingi vikiwemo vya kutaka kumuua.

Alisema mashambulizi zaidi ya kauli yamekuwa yakielekezwa kwa familia yake akiwemo mama mzazi.

Alisema kutokana na vitisho hivyo, ameona ni bora kujiuzulu ili kuepusha shari au matukio ya hujuma kulielekezwa kwa familia yake na zaidi baada ya mama yake mzazi kumtaka kuachia nafasi hiyo.

‘’Nimelazimika kujiuzulu kwa kuwasilisha barua yangu katika Chama Cha Mapinduzi baada ya kupokea vitisho vingi kutoka kwa watu mbalimbali ikiwemo wapinzani wetu ambapo mama yangu alinitaka kuachia nafasi hiyo kwa usalama wangu,” alisema.

Faki aliibuka mshindi katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Konde baada ya kupata kura 1,796 na kumshinda mgombea kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Muhammed Sais Ilyasa aliyepata kura 1,375.

Hata hivyo ushindi wa mgombea wa CCM ulipingwa na chama cha ACT- Wazalendo kwa madai kwamba, wameporwa ushindi wao.

Baadhi ya wananchi wakiwemo wapigakura wa jimbo hilo, wameelezea kusikitishwa na kitendo cha mbunge mteule huyo kujiuzulu.

Walisema walikuwa wamejenga matumaini makubwa ya kushirikiana naye katika kufanya kazi ili kuleta maendeleo ya jimbo hilo.

Mkazi wa Msuka jirani na anapoishi mbunge huyo aliyejiuzulu, Mselem Haji, alisema wapigakura waliojitokeza kwa wingi kumchagua mbunge huyo wamesikitishwa kwa sababu walitumia nguvu kubwa ikiwepo kuwapeleka kupiga kura watu mbalimbali ikiwemo wagonjwa.

‘’Kauli ya kujiuzulu kwa Mbunge Mteule Faki imetusikitisha sana na tumeipokea kwa maoni tofauti maana wapo wanaosema amepokea agizo kutoka kwa chama chake na wapo wanaosema ni vitisho vya wapinzani wanaosema jimbo lao limeporwa,” alisema.

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema wamepokea barua ya kujiuzulu kwa Mbunge Mteule Sheha Mpemba Faki baada ya kupata changamoto za kifamilia ambazo ni kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yake kuwatumikia wananchi.

Baadhi ya wanachama wa CCM Zanzibar walielezea kusikitishwa na kauli ya kujiuzulu kwa mbunge huyo kwa sababu za kutishiwa maisha yake kuwa hazina msingi wala mantiki. Mkazi wa Mikunguni Unguja, Haji Iddi alisema sababu alizotoa kuhusu uamuzi wake ni nyepesi.

‘’Sijaridhishwa na sababu za kujiuzulu kwa mbunge mteule kwa sababu suala la kutishiwa maisha kwa wabunge na wawakilishi kutoka CCM ni jambo la kawaida katika Kisiwa cha Pemba,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz