Juzi nchi ilifanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini mitaa mingi haikuwa na dalili za kufanyiwa kwa uchaguzi huo.
Wananchi katika baadhi ya maeneo walionekana kuendelea na shughuli zao za kila siku, hakukuwa na hamasa yoyote kuhusu uchaguzi huo ambao ni wa ngazi ya chini ambapo wananchi walichagua wenyeviti wa kijiji, wenyeviti wa mitaa, wajumbe wa halmashauri ya kijijiji na wajumbe wa kamati za mitaa.
Hamasa hiyo pia ilikosekana kwa viongozi, hawakuuchangamkia uchaguzi kama ilivyozoeleka na kuhamasisha wananchi kwenda kushiriki katika uchaguzi huo.
Hali kama hii haijapata kutokea katika uchaguzi wowote uliofanyika katika miaka ya hivi karibuni. Kwa ujumla uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu ulipooza na hata baadhi ya watu hawakukumbuka kuwa juzi kulikuwa kunafanyika uchaguzi.
Inawezekana hali hiyo imetokana na karibu asilimia 90 ya wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupita bila kupingwa, hivyo maeneo husika kutokuwa na hekaheka za ushindani katika uchaguzi.
Mfano katika vitongoji vitatu vya Paris, Rahaleo na Ruheya katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara vilishindwa kufanya uchaguzi baada ya wagombea kushindwa kujitokeza kuchukua fomu, hivyo msimamizi wa uchaguzi, Ahmed Seleman kuahirisha hadi Desemba 15.
Siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alikaririwa akisema uchaguzi ungefanyika mikoa mbalimbali nchini isipokuwa Katavi, Ruvuma na Tanga ambako wagombea wake walipita bila kupingwa.
Uchaguzi huo ulifanyika huku vyama vya upinzani vya Chadema, UMD, CCK, NCCR-Mageuzi, NLD, ACT-Wazalendo, CUF na Chauma vilitangaza kujitoa kwa madai ya kufanyiwa mchezo mchafu na wasimamizi wa uchaguzi.
Walidai wagombea wao wengi walifanyiwa hujuma wakati wa kurudisha fomu, wasimamizi wa uchaguzi kuzikimbia ofisi na kuondolewa katika kinyang’anyiro kwa sababu zisizo na mashiko.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alisema wagombea wao waliochukua fomu na kurudisha ni asilimia 60 kati ya 85, huku asilimia 25 walioteuliwa na chama walinyimwa fomu.
Mbowe alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam Chadema walikuwa na wagombea 570, lakini waliopitishwa walikuwa 24, hivyo akasema kushiriki uchaguzi huo ni kuhalalisha ubatili.
Kwa chama cha ACT-Wazalendo kilisema wagombea wake zaidi ya 200 waliondolewa, huku baadhi yao
wakiambiwa chama chao hakijasaliwa na msajili wa vyama vya siasa.
Hata hivyo, vyama vya ADC, TLP, AAFP, DP na Ada Tadea vilishiriki uchaguzi, huku Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akisema malalamiko ya vyama vya upinzani vilivyojitoa yalitokana na uzembe wa viongozi wao.
Pamoja na wagombea wa maeneo mbalimbali kutangazwa kupita bila kupingwa. Je tunajifunza nini kutokana na hali halisi iliyoonekana juzi? Inafahamika kuwa kufanyika kwa uchaguzi huo ni matakwa ya kikatiba na demokrasia. Hali hii inamaanisha nini kidemokrasia?
Huu si uchaguzi wa kwanza kufanyika nchini chini ya mfumo wa vyama vingi nchini, lakini hali kama hiyo haijapata kutokea katika miaka ya nyuma. Tumejikwaa wapi? Kama taifa, tunapaswa kuangalia kasoro zilizojitokeza na kuzirekebisha ili hali kama hiyo isijitokeze tena.
Nchi inakuwa na afya kwa wagombea katika uchaguzi viongozi wanapochaguliwa kutokana na ushindani ulivyo na si kupita bila kupigwa. Kiongozi wa aina hii ni vigumu hata kukosolewa na wananchi kwa kuwa hawakushiriki kumchagua.
Pia anaweza asiwajibike ipasavyo kwa wananchi kwa kuwa hakuchaguliwa kutokana na kura zao, bali alipita.
Ni muhimu kasoro zilizoibuliwa zikafanyiwa kazi sasa ili mwakani tutakapoingia katika uchaguzi mkuu wa kuchagua urais, wabunge na madiwani ufanyike kwa amani, uwazi na bila kuwapo figisu zozote.
Tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi huo kulikuwapo na malalamiko ya kutokuwapo kwa uwazi hasa kuhusu kanuni za uchaguzi pamoja na tarehe ya kufanyika uchaguzi.
Baada ya kanuni na tarehe ya uchaguzi kuwekwa wazi, yakaibuka malalamiko mengine yaliyohusu wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ambao walidaiwa kukimbia ofisi wakati wagombea wa upinzani walipokwenda kuchukua fomu, kutoa fomu zenye kasoro na wagombea wa upinzani kuenguliwa katika uchaguzi kwa sababu zisizo na mashiko.
Mfano chama cha ACT Wazalendo kilisema kati ya wagombea 173,573 waliochukua fomu za uteuzi na kurejesha, wagombea 6,944 ndio waliopitishwa sawa na asilimia nne huku 166,649 wakienguliwa.
Mwenyekiti wa Chauma, Hashim Rungwe alisema wagombea zaidi ya 259 wa chama hicho walienguliwa bila sababu za msingi.
Maoni ya viongozi
Askofu Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kikutheri (KKKT) anasema mambo yaliyokuwa yakifanyika wakati wa maandalizi ya uchaguzi na kuenguliwa kwa wagombea wa vyama vingine hayakuwa ya afya kwa jamii.
“Nchi imegawanyika katika itikadi za kichama na kuna mambo yako dhahiri huhitaji miwani ya ziada au darubini kwamba hapa mambo hayajaenda sawa. Yametugawa,” alisema Askofu Munga hivi karibuni baada ya uzinduzi wa ripoti ya haki za binadamu.
Anasema jambo la msingi ni haki kutendeka kwa kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na kwamba kama kulikuwa na sababu za mtu kukosa sifa za kugombea kuna taratibu, lakini kilichotokea hakikuwa cha lazima.
“Usipotenda haki utagawa, haki ndio inayounganisha. Njia ya kutoka hapa ni haki itendeke, uchaguzi uwe wa haki ndipo haya mambo yanaweza kutulia.
“Tukiendelea hivi tunaweza kuiingiza nchi katika migogoro isiyokuwa na sababu na tukiingia katika migogoro hata hao wanaodhani wanataka kutawala hawatatawala kwa furaha,” anasema.
Askofu Munga anasema penye nia njema utawala wa sheria unapaswa kuwapo badala ya kuadhibu, hivyo wanaweza kukaa chini kwa maridhiano.
Anasema huu si uchaguzi wa kwanza, na kuhoji kwa nini safari hii yametokea mambo hayo kwa kishindo kikubwa na kusema kuwa anaona ile roho ya kukaa pamoja na kufanya jambo kama taifa imepungua.
“Njia yoyote ya hila haitatusaidia, mwaka ujao kuna uchaguzi mkubwa yakifanyika yatatokea magumu zaidi ya haya. Mimi nadhani tujifunze kuheshimu haki za watu, tujifunze kuona amani hii ina gharama na wakati mwingine ni kujikana hata kwenye ‘interest’ zako ili kuona tunaijenga amani,”anasema.
Naye Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Benson Bagonza anahoji watu kukosa furaha na kutaja makundi 14 ya watu.
Katika andiko lake la jana Askofu Bagonza anasema waliopiga kura hawana furaha na waliosusa au kususwa hawana furaha.
Anasema waliopita bila kupingwa nao hawana furaha, waliosimamia kura hawana furaha, walioshinda hawana furaha na hata walioshindwa pia hawana furaha na uchaguzi.
Pia anasema waliopanga yaliyotokea hawana furaha, waliopangiwa yaliyotokea hawana furaha na walioshauri hekima hawana furaha.
Askofu Bagonza anasema kutokana na uchaguzi huo, waliokaa kimya hawana furaha, wanaounga mkono alichoandika hawana furaha na wanaopinga alichoandika hawana furaha.