Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu Chadema kususia mkutano zawa gumzo

Samia Samiaaa Samiaaaa Mkutano Cdm.jpeg Sababu Chadema kususia mkutano zawa gumzo

Fri, 15 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati wadau wa siasa nchini wakikosoa uamuzi wa Chadema kutoshiriki mikutano ya Baraza la Vyama vya Siasa kuwa unakwamisha jitihada za maridhiano, chama hicho kimesema lawama hizo si za kweli, bali Serikali ndiyo haitaki kufanya mabadiliko.

Mkutano maalumu wa vyama vya siasa na wadau wa demokrasia umefanyika kwa siku tatu ukishirikisha wadau wa demokrasia zaidi ya 700, ukiwa na lengo la kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi na hali ya siasa nchini.

Miongoni mwa wadau walioshiriki mkutano huo uliofunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ni pamoja na vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, isipokuwa Chadema ambayo iliendeleza msimamo wake wa kususia shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Said Issa Mohamed aliyehudhuria mkutano huo, alisema hakuwa anawakilisha chama hicho, bali alishiriki kupitia Kikosi Kazi cha Zanzibar, ambako Chadema inashiriki.

Mohamed alisisitiza kwamba msimamo wa Chadema uko palepale kutoshiriki mikutano ya Baraza la Vyama vya Siasa.

Kuhusu msimamo huo, Katibu wa wanawake wa Chama cha DP, Neema Mwakitwange alisema vyama vya siasa havijalazimishwa kushiriki mkutano huo, ni jambo la hiari, lakini anadhani kama Chadema ingeshiriki ingesaidia kutoa mawazo yake kwa ajili ya kujenga.

"Chadema kuamua kuja au kutokuja ni uamuzi wao binafsi, lakini nafikiri kwa uamuzi wa busara, ni vizuri tungekuwa pamoja kwa sababu wote tunajenga nyumba moja, hatuna haja ya kugombea fito. Kama lengo letu ni kujenga mustakabali mwema wa uchaguzi ujao na Katiba mpya, ni vizuri wangekuja tukabadilishana mawazo," alisema Mwakitwange.

Alisema Chadema wana matakwa yao kama chama na kama Watanzania, ambayo wangetamani Serikali iyasikie ili wapate majawabu moja kwa moja na kuona yanafanyiwa kazi kama wanavyohitaji.

"Kutoshiriki mikutano kama hii si jambo jema kwa sababu yale wanayoyalalamikia wangeweza kuyatoa, huenda yanaweza kufanyiwa kazi," alisema katibu huyo.

Akifafanua msimamo wa Chadema, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema si kweli kwamba chama chake hakitoi ushirikiano kwenye maridhiano kupitia majukwaa mbalimbali ya kisiasa, bali Serikali ndiyo haitaki kufanya mabadiliko na kuleta mwafaka wa kitaifa na kuwa ipo siku wataweka wazi ukweli kuhusu hatua zote za maridhiano.

“Wanadanganya, Serikali ndiyo haitaki reforms (mabadiliko), haitaki kutoa ushirikiano wa kufikia mwafaka wa masuala ya kitaifa, ipo siku tutaweka wazi hatua zote za majadiliano tuliyofanya na Serikali kwa mwaka mzima, ndiyo mtaelewa,” alisema Mnyika.

“Serikali inachokifanya kwa sasa ni manipulations (ghiliba) kwa njia ya majukwaa na makongamano ili tuonekane sisi hatuna utayari wa maridhiano ya kitaifa, wanadhani mikutano hiyo ndiyo itasaidia, na sisi tumekuwa wastaarabu, hivyo wanatumia mwanya huo kuaminisha watu kwamba hatuna ushirikiano.”

Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini alisema yeye si muumini wa kususa kwa sababu anajua katika siasa watu wanaweza kutofautiana lakini wakaendelea kufanya kazi pamoja.

"Kwa mfano, kutoshiriki kwenye mkutano mkubwa kama huu, sioni kama ni jambo la busara. Msimamo wao ni kutoshiriki mikutano ya Baraza la Vyama vya Siasa, lakini wakumbuke kuwa washiriki wa mikutano hii wanatoka katika makundi mbalimbali.

"Mfano huu hapa, tumejadili suala zito la Katiba, sasa unashindwa kutoa maoni yako hapa ndani lakini huko nje unazungumza. Sasa hawa wa ndani wanaweza wakachukua msimamo ambao wewe huna, wakafanya uamuzi ambao wewe hungeweza kufanya," alisema Selasini.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo, Ismail Jussa alisema kwa jambo kubwa kama mkutano huo, ingependeza vyama vyote vikawepo na kwamba, hiyo haina maana kila anayefika anakuwa ameridhika na kila linalosemwa kwenye majadiliano hayo.

"Ninachoweza kuwashauri ndugu zetu wa Chadema ni kwamba, ndiyo, kususia ni moja ya silaha za kisiasa lakini unapima unasusia nini. Kususia jukwaa la majadiliano kama hili maana yake unapunguza sauti,” alisema Jussa.

Alisema ACT-Wazalendo imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha mawazo ya upinzani yanaingizwa kwenye mapendekezo ya Kikosi Kazi, pengine Chadema nao wangekuwepo wangetoa mchango wao na sauti za upinzani zingejenga sauti moja yenye nguvu.

Makamu Mwenyekiti wa TLP, Dominata Rwechungura alisema hatua ya Chadema ni kuwakosesha wanachama wao fursa ya kuwa sehemu ya mabadiliko ambayo vyama vya siasa pamoja na wapenda demokrasia wangependa kuyaona.

“Nadhani walikuwa na fursa ya kipekee ya kuja kueleza wanayotaka yafanyike na kwa njia gani. Huwa tunawasikia wakizungumza kwenye mikutano yao lakini mikutano ya wadau kama hii pia ni muhimu kuliko kujifungia wenyewe,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live