Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Saa za Meya Dar zahesabika, awaangukia viongozi wa dini

90853 Pic+meya Saa za Meya Dar zahesabika, awaangukia viongozi wa dini

Sun, 5 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ni kama meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita anapumulia mashine katika kiti chake, na anaona kimbilio pekee sasa ni viongozi wa dini wa mkoa ambao amewaomba wamuombee.

Mwita ametoa kauli hiyo kutokana na uwezekano wa kuendelea kushikilia nafasi hiyo kuwa njiapanda wakati huu akisubiri ripoti ya kamati iliyoundwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwasilishwa baraza la madiwani wa halmashauri ya jiji.

Kamati hiyo imewahoji madiwani wa CCM ambao ni wajumbe wa baraza hilo, huku madiwani wa Chadema, akiwamo wa Tabata, Patrick Asenga na meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob hawakwenda kuhojiwa licha ya kupewa barua za wito.

Meya huyo aliyechaguliwa mwaka 2016, anakabiliwa na tuhuma za kutotumia Sh5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda.

Tuhuma nyingine ni kutumia vibaya gari ya ofisi ambayo alipata nalo ajali, kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kusababisha meya Jacob kugombana na meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo na kudaiwa kuwapendelea baadhi ya mameya kuingia kamati za fedha.

Tayari, Mwita, ambaye pia mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alishajibu tuhuma hizo akisisitiza hahusiki na jambo hilo.

Mwananchi imedokezwa na vyanzo vyake kwamba tayari kamati imeshakamilisha ripoti na kuiwasilisha kwa mkuu wa mkoa na kinachosubiriwa ni kuitishwa kwa kikao cha baraza ili kuiwasilisha na kufanyia maamuzi.

Jana, Mwananchi ilimuuliza Mwita kuhusu kinachoendelea na kwa sauti ya chini na upole alisema: “Naomba masheikh, wachungaji na viongozi wengine wa kiroho waniombee. Nipo katika kipindi kigumu sana kuhusu nafasi yangu ya umeya wa jiji hili.”

Mwita, ambaye ni diwani wa Vijibweni (Chadema), alisema taarifa alizonazo tayari kamati ya kuchunguza tuhuma zake imeshamaliza kazi na kwamba kuna kila dalili ya kuondolewa katika nafasi hiyo.

Lakini mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Spora Liana aliiambia Mwananchi kuwa hafahamu lolote kwa kuwa alikuwa likizo na atarudi kazini Jumatatu.

Meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo ambaye alikiri kuongoza kampeni ya wajumbe wa CCM kusaini ombi la kutokuwa na imani na Mwita kutokana na tuhuma hizo, alidai bado hajahojiwa na tume hiyo kwa kuwa alikuwa nje ya nchi.

Akizungumzia taratibu za kumng’oa meya, Meya Jacob alisema huanza kwa madiwani kujiorodhesha kwamba hawana imani naye na baadaye kumpelekea mkurugenzi malalamiko. Alisema mkurugenzi huangalia kama akidi imetimia na ndipo huitaarifu ofisi ya mkuu wa mkoa.

“Akishafikisha ofisi ya mkuu wa mkoa, anamtaarifu na mlalamikiwa kwamba unalalamikiwa kwa makosa moja, mbili au tatu na kutakiwa kujibu ndani ya siku saba au 14,” alisema Meya Jacob.

Alisema majibu ya uchunguzi hurudishwa kwa mkurugenzi ambaye huyapeleka ofisi ya mkuu wa mkoa ambaye akiona hayana msingi hataendelea na kama ataona yana msingi ataunda kamati.

Alisema wajumbe wa kamati watateuliwa na mkuu wa mkoa ambao ataona wanafaa.

“Watakapokuwa wamehoji wataandaa ripoti na kuirudisha kwa mkuu wa mkoa ambaye yeye sasa anakuja kuiwasilisha Baraza la Halmashauri ya jiji,” alisema Jacob na kuongeza kuwa madiwani huweza kumuondoa wakiwa zaidi ya nusu.

Kwa mujibu wa Jacob, kwa sasa CCM ina madiwani tisa na wapinzani saba na kwamba mmoja wa CUF anaweza kuwa upande wa kumuondoa meya.

Iwapo meya ataondolewa haitawezekana kufanya uchaguzi mwingine kwa kuwa imebaki chini ya miezi minne kabla ya mabaraza ya madiwani kuvunjwa, na hivyo naibu meya, ambaye anatoka CCM, atashika hatamu iwapo Mwita atang’olewa.

Alipoulizwa sababu ya kumng’oa meya wa jiji, Jacob alisema: “Hawataki tu kuongozwa na meya wa upinzani kwa kuwa uwezo wa kumng’oa wanao.”

Hata hivyo kulikuwa na tetesi kuwa huenda meya huyo angetangaza kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM, lakini baadaye habari hizo zikatoweka.

Madiwani wengi waliojivua uanachama wa upinzani na kurudi CCM, walipewa fursa ya kutetea nafasi zao wakiwa CCM, jambo lililoibua tuhuma kuwa walikuwa wakifanya makubaliano na chama hicho kabla ya kufanya uamuzi huo.

Desemba 22 mwaka jana gazeti hili lilichapisha habari inayoeleza meya huyo kujibu tuhuma hizo kikinukuu mojawapo chanzo kikieleza kuwa Mwita hahusiki na kukwamisha matumizi ya Sh5.8 bilioni kwa kuwa fedha hizo zinaidhinishwa na kamati ya fedha.

“Kuhusu tuhuma za gari anadai haimhusu kwa sababu yeye si dereva. Alizungumzia kuhusu ajali ya gari akidai hakuwepo bali dereva aliliegesha sehemu na kwenda kula likagongwa. Pia suala la Jacob na Chaurembo kufanya vurugu, hilo amesema halimhusu maana walikuwa wakigombea kura katika uchaguzi,” kilieleza chanzo hicho.

Katika mazungumzo yake jana Mwita alisisitiza kutohusika na tuhuma hizo huku akisisitiza kuwa tume hiyo iliyoundwa huenda ikatoa majibu ya kukumkuta na tuhuma au la “ndiyo maana nawaomba viongozi wa dini waniombee katika suala hili lolote linaweza kutokea.

“Ukweli ni kwamba sihuki hata kidogo, kwa sababu nimekuwa nikifanya kazi bega kwa bega na Serikali na Mwananchi mmekuwa mkiniandika na kunipiga picha kwenye hafla za kitaifa ninazohudhuria. Naomba waniombee imebaki miezi mitatu na nusu kabla ya mabaraza haya kuvunjwa,” alisema Mwita.

Chanzo: mwananchi.co.tz