Jiji la Dodoma liligubikwa na rangi za kijani, njano na nyeusi, lakini wengi walishuhudia ambacho hakikutarajiwa, hasa katika uchaguzi huo.
Mbali ya kuwapo kwa mabadiliko kadhaa, yakiwamo ya kiuongozi na uendeshaji wa mkutano, kifupi zilikuwa ni siku za vijembe na uvumilivu wa hali ya juu kutoka kwa badhi ya wajumbe, licha ya wengine kuamua kusemana hadharani kwa walichoamini hakikuwa kimekwenda sawasawa.
Matumbo ya wagombea zaidi ya 370 yalikuwa moto, kila mmoja alipiga moyo konde kwamba anakwenda Dodoma kushinda, ingawa kazi kubwa ilikuwa ni kunyang’anyana wajumbe 1,928.
Mabadiliko ya Katiba ya CCM Mkutano huo ulipitisha mabadiliko ndani ya chama hicho ambayo yameongeza idadi ya wajumbe katika vikao vya maamuzi, ikiwemo wajumbe wa NEC kutoka 30 hadi 40.
Awali kulikuwa na nafasi 15 za wajumbe wa NEC kutoka Tanzania Bara na nafasi kama hizo kwa upande wa Zanzibar, lakini marekebisho hayo yameongeza nafasi tano kila upande.
Katika mabadiliko hayo, katibu wa itikadi, siasa na uenezi imekuwa ni nafasi ya kuajiriwa kwa mkataba, badala ya kuchaguliwa kama awali ambapo ilielezwa kuwa hatua hiyo italeta maboresho, huku nafasi za uteuzi kwa NEC zikiongezeka kutoka saba hadi 10.
Nafasi nyingine ni kuwatambua makatibu wa jumuiya kuwa wajumbe wa halmashauri kuu, nafasi ambazo hazikuwepo awali na wajumbe walipitisha mabadiliko hayo kwa kura za ndiyo.
Katika nafasi za wajumbe wa ya chama hicho kikongwe nchini na barani Afrika, katika nafasi za NEC, kulishuhudiwa mchuano kwa mawaziri, viongozi wa zamani serikalini, waandishi wa habari, wanamichezo ambapo wagombea jumla bara na visiwani walikuwa 374, wakiwania nafasi 40.
Ukiondoa mabadiliko hayo ya kiuongozi, CCM ni kama iliamua kufanya mapinduzi ya aina yake mwaka huu, kwani pia ilishuhudiwa kwa mara ya kwanza, wajumbe wa mkutano huo wakitoa michango yao baada ya kuwasilishwa kwa ripoti za utekeleza wa chama na jumuiya zake.
Wajumbe wengi walipokuwa wakichangia, hawakusita kuonyesha dukuduku lao kuhusu huduma zisizoridhsiha za maji, umeme, barabara na upatikanaji wa vifaa tiba hospitalini.
Siku ya Mkutano Ulinzi uliimarishwa na kila kona waliwekwa watu wa kusimamia na kuzuia wavamizi, lakini pia kupunguza munkari wa wagombea.
Nyimbo zilitungwa na kuimbwa kwa wagombea, hasa mawaziri Januari Makamba, Dk Mwigulu Nchemba na Nape Nnauye ambapo hata hivyo walishinda kwenye kinyang’anyiro hicho.
Mapema asubuhi idadi ya wapambe ilionekana kuwa kubwa kuliko wagombea, kila mmoja alipeleka wapambe wake kutoka mikoani, lakini kazi kubwa ilifanywa na vijana wa Dodoma ambao walitumika kuzifahamu korido za kupita na kuwasaka wapiga kura.
Licha ya ulinzi kuimarishwa kuwa wapambe na wagombea wasiingize vipeperushi ndani ya ukumbi, watu wengi waliingia navyo hata vikatapakaa ukumbi walimokuwa wapiga kura.
Katika ukumbi wa White House, kelele zilikuwa nyingi huku wapambe wa wagombea wakiendelea kupigana vikumbo katika nyimbo za shangwe kwa ajili ya kuwanadi wagombea wao.
Wapo waliokuwa na kampeni za ndoa ili kuunganisha nguvu, lakini wengine walikuwa wakipambana peke yao.
Vimbwanga kwa wasanii Katika uchaguzi huu kulikuwa na wasanii ambao majina yao yalikuwa yamepitishwa kwa ajili ya kugombea ujumbe wa halmashauri kuu ya CCM.
Wajumbe wengi walikuwa wakizungumza na wasanii hao na kutaka wapige nao picha, huku kauli za tuko pamoja zikionekana kutawala zaidi. Kama zingehesabiwa kauli za tuko pamoja, huenda wasanii wote wangepita kwenye chekeche la uchaguzi huo, lakini bahati mbaya kura haikuendana na hoja za tuko pamoja.
Ilivyokuwa mtaani Kila mtaa ulijaza watu, wageni waliojipambanua kwa kupanga vyumba vya kulala, lakini wenyeji walijitahidi kuongoza wageni wao hasa kwa kutumia usafiri wa pikipiki kuwafikia wajumbe walikopanga.
Haikufahamika mara moja kwamba wajumbe walikuwa wanafuata nini katika nyumba na vyumba walivyokuwa wamefikia wengine ambako waliweza kuamshana.
Kumbi za starehe katikati ya jiji zilifurika, watu walikula na kustarehe, watu walikosa vyumba vya kulala, miziki ilipigwa na chupa zilifunguliwa kwa kila aliyeweza kutumia alifanya hivyo, ingawa si wote walikuwa watumiaji.
Bodaboda walivuna Kama kuna watu wangeombea Mkutano Mkuu uendelee walau kwa siku nyingine kadhaa, walikuwa ni waendesha pikipiki. Hawa watu waliendesha vyombo vyao usiku na mchana na hakukuwa na mahali waliposhindwa kufika, badala yake walikuwa ni watu wa mbio. Bodaboda walikuwa wakiulizwa swali jepesi ambalo ni mahali fulani unapafahamu? Akijibu ndiyo basi kinachofuta ni kuondoka bila kuuliza umbali na gharama ambazo mhusika angechajiwa.
Vijembe kwa baadhi ya wajumbe Mmoja wa wajumbe ambaye aliitwa shemeji, alipata wakati mgumu karibu kwa kila mjumbe, hasa viongozi waliposimama mbele ya kadamnasi hiyo kuzungumza. Wazee wastaafu walizungumza kwa mafumbo bila kumtaja jina kabla ya Katibu Mkuu Mstaafu Yusufu Makamba kumtaja hadharani, akianza kwa jina la shemeji kisha akamuita Dk Bashiru Ali. Dk Bashiru huenda akawa miongoni mwa watu wenye ngozi ngumu kutokana na mashambulizi ya mdomo aliyoyapata, lakini yeye hakujibu zaidi alionekana kutabasamu wakati wote. Mbali na Makamba aliyemtaja kwa jina, wengine waliongea kwa mafumbo lakini yakionekana kumlenga moja kwa moja Dk Bashiru, hasa kuhusu kauli yake ya hivi karibuni iliyopinga msemo wa Mama kaupiga mwingi. Hata hivyo, kauli ya Rais Samia ya kuomba kibali cha kwenda kuisuka Serikali yake kiliwaacha matumbo moto baadhi ya vigogo kwenye nafasi za uteuzi ambao wanaamini wakati wowote huenda vitumbua vyao vitaingia mchanga. Rais Samia alikoleza moto zaidi baada ya kuitisha kikao cha Halmashauri Kuu usiku na wajumbe waliamini anakwenda kuisuka upya Sekretarieti ya CCM, lakini Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka akasema, suala hilo limesogezwa mbele.