Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruzuku kwa vyama vyote ni wimbo wa sherehe kwenye msiba

Vyama Siasaaaa.png Ruzuku kwa vyama vyote ni wimbo wa sherehe kwenye msiba

Wed, 10 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba wakijadili jambo katika mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoshirikisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Vyama vyote vya siasa vipewe ruzuku. Huo ndio mjadala. Ni mapendekezo yaliyoanzia kwenye ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa kuchunguza mazingira ya shughuli za kisiasa. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amepigilia msumari.

Zitto amesema, vyama vikipewa ruzuku, itasaidia kuviondoa kwenye mifuko ya wenye fedha. Hii ni hoja ya upande mmoja. Nyingine ambayo hakuisema ni kuwa ruzuku ikiwa holela, itashawishi watu kuanzisha vyama, kwa kuona ni tobo la fedha za bure.

Hoja ya Zitto si dhaifu. UK, Karne ya 19, waliandika sheria ya kwanza ya kudhibiti rushwa kwenye siasa. Inaitwa Sheria ya Kuzuia Rushwa na Vitendo Haramu ya mwaka 1883. Robo ya kwanza ya Karne ya 19, UK, wakapitisha sheria ya kudhibiti ugawaji vyeo vya heshima.

Mwaka 2006, UK ikakumbwa na kashfa kubwa ya uuzaji vyeo vya kudumu vya heshima (life peerages). Tume ya Uteuzi Chemba ya Juu ya Bunge (House of Lords), ilikataa majina yote yaliyopendekezwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Tony Blair.

Watunukiwa wa vyeo vya kudumu vya heshima, huitwa barons kwa wanaume, na baroness akiwa ni mwanamke. Huteuliwa na Mfalme au Malkia, baada ya kupendekezwa na Waziri Mkuu, kisha kuhakikiwa na Tume ya Uteuzi. Barons na Baronesses ni wajumbe wa House of Lords na hushiriki uamuzi wa mambo nyeti ya nchi.

Baada ya Tume ya Uteuzi House of Lords kukataa majina yote yaliyopendekezwa na Blair, ilibainika kuwa wapendekezwa wote walikuwa wamekikopesha fedha nyingi kilichokuwa chama tawala, Labour, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2005. Hali hiyo iliashiria kwamba ulikuwa uteuzi wa nipe nikupe (quid pro quo).

Ipe uzito hoja ya Zitto katika eneo hili; ikiwa vyama vya siasa havijiwezi kiuchumi, wenye fedha wanaweza kuvitumia kuendesha nchi. Mfano hai ni UK, jinsi matajiri walivyoishawishi Labour kwa fedha, ili waingie chemba ya juu ya Bunge na kufanya uamuzi muhimu kuhusu nchi.

Ipe changamoto hoja ya Zitto

Asili ya binadamu ni kukimbilia palipo na fedha rahisi. Kama kuanzisha chama cha siasa na kufanikisha usajili, kutawezesha kujipatia ruzuku, kuna watakaokimbilia kwa bidii kubwa. Wataona ni fedha za bure.

Hakuna fedha hutoka bila masharti. Ruzuku kwa kila chama, maana yake sheria zitatungwa zenye kuelekeza matumizi sahihi ya fedha za umma. Hata kama vyama vitafutwa baada ya kushindwa kukidhi masharti ya matumizi sahihi ya fedha, bado hasara haitafidiwa.

Vyama vitachipua kama uyoga. Itadhaniwa ni kukua kwa demokrasia, kumbe ni mawindo ya fedha za bwerere. Badala ya kujenga mazingira bora ya kisiasa, itakuwa ni ujenzi wa magenge ya wezi wa fedha za umma, kupitia dirisha la vyama.

Usimamizi wa matumizi sahihi ya fedha za umma, unaweza kwenda sambamba na kumwongezea makali Msajili wa Vyama vya Siasa. Naye atayatumia makali yake kuvifungia na kuvifuta vyama anavyoona havikidhi masharti ya matumizi ya fedha za umma. Hiyo haitakuwa demokrasia.

Changamoto nyingine ni kiasi cha fedha za ruzuku. Mathalan, chama ruzuku yake ni Sh50 milioni kwa mwezi. Wakitokea matajiri wenye kumwaga Sh100 milioni kwa mwezi? Vipo vyama vilikuwa vinapokea mamia milioni, na vilidai fedha hazikutosha. Wimbo wa ruzuku kila chama, mashairi yake yanapaswa kupata mzani wa pembe nne. Nyuzi 360.

Kipimo gani kinaonesha kuwa vyama vikipewa ruzuku, vitafanya kazi kwa weledi? UK, chama chenye wabunge kuanzia wawili, kinapewa ruzuku. Labour walishinda viti 412 vya ubunge, Uchaguzi Mkuu UK 2001. Hiyo maana yake walikuwa na ruzuku ya kutosha, ila uchaguzi uliofuata ikabainika chama kilipewa fedha na matajiri ili wapewe vyeo vya kudumu chemba ya juu ya Bunge, House of Lords.

Tuupitie mfumo wa sasa

Sehemu ya V ya Sheria ya Vyama vya Siasa, imeainisha njia tatu za vyama kupokea mgawo wa ruzuku kutoka serikalini. Njia mbili kupitia Serikali Kuu. Sheria inaelekeza Serikali kutenga mpaka asilimia mbili ya bajeti yake ya matumizi ya kawaida (recurrent expenditure), kuhudumia vyama vya siasa.

Hizo fedha zinagawanywa hivi; asilimia 50, vyama vinapokea kwa uwiano wa idadi ya wabunge wa kuchaguliwa. Asilimia 50, hutolewa kwa uwiano wa kura za ubunge majimboni. Chama kinachostahili kupokea mgawo lazima angalau kiwe kimefikia asilimia tano ya kura zote za ubunge.

Njia ya tatu ya ruzuku ni kupitia Tamisemi. Vyama hupewa mgawo wa mwaka, kulingana na uwiano wa idadi ya madiwani kwenye halmashauri nchi nzima. Hivyo, chama cha siasa Tanzania, kikiwa na mbunge japo mmoja au hata diwani, kinapata ruzuku.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 1995, kila chama cha siasa Tanzania kilipewa ruzuku. Kilikuwa kipindi cha neema ili vyama viweze kumudu kufanya kampeni. Baada ya hapo yalifanyika mabadiliko kadhaa hadi kufikia sasa ruzuku zinatoka kwa idadi ya wabunge, uwiano wa kura za ubunge na idadi ya madiwani.

Vipo vyama vya siasa vilinufaika katika kipindi cha neema kuelekea Uchaguzi Mkuu 1995. Vilipewa ruzuku, lakini havikushawishi wapigakura. Vina umri wa miaka 30 au zaidi. Je, hivi vipewe ruzuku nyingine hivi sasa kwa masilahi gani na kwa faida ipi?

Vyama vingine vilifanikiwa kujenga ushawishi. Vikapata wabunge na ruzuku. Vikapita kwenye migogoro mikubwa, tena sababu ikiwa ni hizo fedha za ruzuku. Kisha, vikapoteza ushawishi. Je, leo vipewe ruzuku tena ili iwe nini?

NCCR-Mageuzi ni chama kilichojenga msingi mzuri Uchaguzi Mkuu 1995. Kilipata wabunge 19 na ruzuku juu. Uchaguzi Mkuu 2000, kikaambulia mbunge mmoja. Uchaguzi Mkuu 2005, kikatoka patupu. Uchaguzi Mkuu 2010 kikapata wabunge wanne.

Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, alimteua aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kuwa mbunge. Hivyo, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, chama hicho kikawa na wabunge watano. Uchaguzi uliofuata kikabaki na mbunge mmoja. Sasa ni sifuri.

Pandashuka ya NCCR, inafanana na vyama vya TLP na UDP. Mwaka 1995 mpaka 2010, vimekuwa na wabunge kwa idadi tofauti. UDP kilikuwa na wabunge wanne mwaka 1995. Kisha wakawa watano baada ya Mwenyekiti wake, John Cheyo, kushinda uchaguzi mdogo, Magu mwaka 1996.

Uchaguzi Mkuu 2000, UDP walikuwa na wabunge wanne. Mwaka 2005, akabaki mmoja, vivyo hivyo mwaka 2010. TLP walipata wabunge watano Uchaguzi Mkuu 2000. Uchaguzi uliofuata (mwaka 2005), wakabaki na mmoja, iliendelea hivyo mwaka 2010. Si TLP wala UDP chenye mbunge leo.

Hoja zipi zinaweza kujengwa leo kuhalalisha ruzuku kwa vyama ambavyo viliwahi kupokea na vikafanikiwa kuwa na wabunge. Baadaye, vikapoteza viti vyote. Hizo fedha zinazozungumzwa ni za wavuja jasho wa nchi.

Kifikirie chama kama Chadema, kilichoanza na wabunge wanne mwaka 1995. Kikafikisha watano mwaka 2000. Halafu wabunge 11 mwaka 2005. Ilipofika mwaka 2010, kikawa chama kikuu cha upinzani.

Chama cha Wananchi (Cuf), kiliongoza kwa idadi ya wabunge kuanzia mwaka 1995 mpaka 2005. Kilipoteza uongozi wa kambi ya upinzani mwaka 2010, lakini kiliendelea kupata idadi nzuri ya wabunge na ruzuku. Baada ya Uchaguzi Mkuu 2015, chama kikaingia kwenye mgogoro.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020, Cuf ilisambaratika. Yakawepo madai ya kugombea ruzuku. Sasa jiulize, ni usahihi upi wa kutoa ruzuku kwa kila chama, bila kuzingatia matokeo ya uchaguzi, ikiwa fedha za umma zinagombanisha vyama?

Tafakari kuhusu ACT-Wazalendo, kikiwa chama kilichosajiliwa miezi kadhaa kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015, kilipata mbunge mmoja na mamlaka moja ya halmashauri ya manispaa. Kisha wabunge watano. Wakati huohuo, kuna ambavyo vina miaka 30, havina uwakilishi kabisa bungeni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live