Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rungwe kuhusu mikutano "Tumeondoka zama za kutishana"

Rungwe Er Hasim Rungwe

Tue, 3 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashim Rungwe, amesema zama alizoziita za kutishana zimeondoka na kwamba vyama vya siasa vitakuwa sawa mbele ya Serikali na vyombo vya dola.

Rungwe ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuondoa zuio la mikutano ya hadhara, wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa Ikulu jijini Dar es Salaam, leo tarehe 3 Januari 2023.

“Tumepata matangazo yake (Rais Samia), ni faraja sana tutakwenda kufanya mikutano ya hadhara bila vizuizi na wale mapolisi sio wa upande mmoja watakuja kutulinda wote hivyo ni jambo la kufurahisha tumeondoka zile zama za kutishana , hawa ni chama tawala hawa ni vyama vingine hawavijui,” amesema Rungwe.

Rungwe amesema “ nafikiri sasa ni jambo jema tunasubiri kuona upande wa utekelezaji itakuwaje, tutaelewa kama polisi wameelewa kivyake na sisi tumeelewa kivyetu. Sina la kusema zaidi ya kutoa pongezi kwa Rais sababu hii siku imechelewa sana tulikuwa tunaisubiri tuwe huru tufanye kazi ya kuijenga Tanzania nzima.”

Akizungumzia sakata la deni la taifa, Rungwe amesema Serikali kukopa si jambo baya, lakini inatakiwa fedha hizo ziguse maisha ya wananchi moja kwa moja.

“Kukopa sio jambo baya, tangu zamani mtu anakopa na alichokopa anafanyia kazi. Kama kukopa bila kuwa na lengo si jambo zuri, watu wanalalamika mikopo imekuwa mingi na wananchi hali zao mbaya za maisha kwa hiyo nafikiri wangekopa halafu wakaangalia wananchi,” amesema Rungwe.

Rais Samia ameondoa zuio la vyama vya siasa lililowekwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, na kuvitaka vyama vya siasa kuitumia fursa hiyo vyema kwa kufanya siasa za kistaarabu na zenye lengo la kuleta maendeleo kwa taifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live